Mamlaka zielimishe raia kujenga utamaduni wa kubeba kitambulisho

21May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mamlaka zielimishe raia kujenga utamaduni wa kubeba kitambulisho

KILA raia ana wajibu wa kutekeleza katika suala zima la kuhakikisha ustawi wake na taifa kwa ujumla.

Wajibu ambao kimsingi unaangukia katika uga wa kisheria pia kwenye mizania ya mila na tamaduni za jamii anayoishi.

Kwa mfano kutii sheria, kulipa kodi, kulinda usalama wa nchi, amani ya jamii yake, yote haya ni wajibu wa raia mwema kwa taifa lake.

Pamoja na hayo, kuna wajibu wa kawaida katika maisha ya kila siku ambao hata hivyo bado haujatiliwa maanani kwa uzito unaostahili na wananchi walio wengi.

Si wananchi tu, lakini hata mamlaka za serikali zinazohusika na jukumu la kutoa elimu ili raia wawe na utamaduni wa kutimiza wajibu huo kwa minajili ya kuepuka usumbufu na mazonge mbalimbali wanayoweza kukumbana nayo.

Muungwana anazungumzia utamaduni wa kutembea na kitambulisho cha taifa ama kingine kinachotambulika na mamlaka, kikiwamo cha mpigakura ama hati ya kusafiria kwa wale walio nazo.

Amechukua fursa ya kuandika hili baada ya kukumbana na operesheni ya Idara ya Uhamiaji katika safari aliyoifanya mwezi Machi mwaka huu kwenda Mpanda, mkoani Katavi, kusalimia ndugu na jamaa.

Safari yake ya kurejea jijini kutoka Mpanda ilikuwa ni ya basi na ilianzia Sumbawanga mkoani Rukwa kupitia mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Morogoro, Pwani kisha jijini.

Sasa baada ya kutoka Mbeya mjiniĀ  mwendo kama wa saa moja alikutana na kizuizi cha uhamiaji ambacho baadaye alijifunza kutoka kwa abiria wengine wanaofanya safari za mara kwa mara wakitumia barabara hiyo kwamba kumbe ni cha kawaida.

Maofisa Uhamiaji wawili waliingia ndani ya basi alilokuwa akisafiria ambao katika lugha ya heshima lakini yenye mamlaka, walitaka kila abiria ndani ya gari hilo kuonyesha kitambulisho cha taifa kwa ajili ya utambulisho.

Hata hivyo, hawakutaka cha taifa tu, kwamba kwa wale ambao hawakuwa nacho, walitakiwa kuonyesha cha mpiga kura ama hati ya kusafiria kama mbadala.

Kwa Muungwana ambaye anajua umuhimu wa kutembea na kitambulisho si kwa safari za mbali kama hii aliyoifanya bali hata anapoenda kazini, katika miadi yoyote ama kwenye burudani hubeba kitambulisho, haikuwa shida kwake.

Hubeba kitambulisho cha taifa, ama cha kupigia kura au cha kazini ili ajitambulishe wakati wowote kikihitajika.

Na hasa ikichukuliwa kwamba vyombo vya usalama huwa na operesheni mbalimbali za kiusalama, zinazohitaji raia wajitambulishe wakati mwingine.

Hivyo alikitoa kwa maofisa hao wa uhamiaji kama ilivyokuwa kwa abiria wengine wenye utamaduni wa kutembea na kitambulisho, kwa sababu wanajua ni wajibu wao wa msingi kufanya hivyo.

Ilikuwa ni bahati mbaya kwa ambao hawakuwa navyo, kwani walitumia muda mrefu kujieleza ili kuwaridhisha maofisa hao kutokana na maswali waliyokuwa wakiulizwa.

Chenye maslahi katika operesheni hiyo ni kwamba, maofisa hao waliweza kukamata abiria watatu ambao hawakuwa raia wa Tanzania kutoka nchi jirani walioingia nchini isivyo halali.

Ni maoni ya Muungwana basi kwa kila raia mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuwa na utamaduni wa kutembea na kitambulisho kinachokubalika na vyombo vya dola, kuepuka mazonge yanayoweza kujitokeza.

Mazonge kama ya kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kutokuwa na kitambulisho, hivyo kukatishwa ama kucheleweshwa safarini au pale mtu anapokuwa katika shughuli zake za kila siku za kimaisha.

Aidha, Muungwana anatoa rai kwa mamlaka zinazohusika ikiwamo Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara ya Uhamiaji kwa maana hiyo kutoa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa raia kutembea na vitambulisho vinavyokubalika.

Kwamba pamoja na mambo mengine vitambulisho, hasa cha taifa vina umuhimu kwa usalama wa nchi katika kubaini wahamiaji haramu kama ilivyotokea katika safari ya Muungwana.