Mamlaka zihakikishe wapigadebe wanaondolewa kabisa vituoni

14Nov 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Mamlaka zihakikishe wapigadebe wanaondolewa kabisa vituoni

KARIBU miji yote mikubwa na majiji yanakabiliwa na wingi wa vijana ambao wamekuwa wakishinda kwenye vituo vya daladala wakiomba fedha kwa makondakta kila wanapoita abiria.

Vijana hao, ambao ni maarufu kwa jina la 'wapigadebe', wamekuwa wakiita abiria ili waingie katika daladala, kazi ambayo kwa kawaida inapaswa kufanywa na makondakta wa magari hayo.

Kwa utaratibu huu ninadhani hawapaswi kuitwa 'wapigadebe', bali ombaomba kwa sababu hawana kazi ya kufanya zaidi ya kuomba pesa makondakta kana kwamba hawana uwezo wa kufanya kazi.

Hao wote ni vijana wenye afya ambao wangeweza kutumia nguvu zao vizuri kwa kufanya shughuli nyingine, ambazo zinaweza kuwapa manufaa katika maisha yao ya baadaye na badala ya kupoteza muda vituoni.

Nimesema ni vijana wenye afya, lakini pia katika kundi hilo wengine wanaitwa mateja kutokana na kile kinachodaiwa kuwa wanatumia dawa za kulevya, huku wakituhumiwa kukwapulia abiria vitu vyao.

Kwa ujumla, nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana inapotea bure na kwa hali hii ipo haja kwa mamlaka husika kuchukua hatua za kuiokoa badala ya kuiacha ikiendelea kuteketea.

Inasikitisha kuona kijana mwenye nguvu akishinda kwenye kituo cha daladala akiomba Sh. 200 ama 500, kwa kondakta eti kwa kisingizio kwamba anaitia abiria waingie katika gari!

Matokeo yake ndiyo hayo ya baadhi yao kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kuiba na wakati mwingine kushiriki karibu kwenye kila aina ya uhalifu.

Na ajabu zaidi ni kuwa hawahawa ndio wazee wa siku za usoni ambao inatarajiwa wawe hazina ya hekima na busara kwa vijana wa baadaye.
Mjadala unaona haina haja ya serikali kuendelea kuwafumbia macho, bali iwaokoe kwa kuangalia njia ya kuwasaidia waweze kujitambua na hivyo kufanya shughuli ambazo zinaweza kuwasaidia katika maisha yao.

Ninasema hivyo kwa sababu haiingii akilini kuona daladala yenye kondakta wanakuja watu wengine kuita abiria.

Na mbaya zaidi wakati mwingine wasipopewa chochote, hufanya vurugu kiasi cha kupasua hata vioo vya magari.

Utaona daladala inafika kituoni imejaa abiria, lakini wanakinga mikono kwa makondakta ili wapewe chochote kama vile ni ombaomba.

Nchi ina ombaomba wengi hivyo hakuna sababu ya kuzalisha kundi jingine la ombaomba kwa kivuli cha upigadebe, na badala yake mamlaka zinapaswa kuwaondoa watu hawa kwenye vituo vya daladala, ili wakafanye shughuli zenye tija.

Ninatambua wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitetea uwapo wa watu hawa kwenye vituo vya daladala kwa hoja kwamba kunapunguza vitendo vya wizi mitaani, mawazo kama haya binafsi sikubaliani nayo.

Ikumbukwe kuwa hao wanaoitwa 'wapigadebe' ndio ambao wamekuwa wakilalamikiwa kuibia abiria vituoni, sasa kuna haja gani wao kuwapo hapo kwa kisingizio kwamba wakiondolewa wataanza kupora mitaani?

Utetezi huo kwa 'wapigadebe' umewahi kutolewa na baadhi ya watu pale serikali ilipoendesha operesheni ya kuwatimua kwenye vituo na kujikuta ikipambana nao.

Katika mazingira haya ndio maana nikasema ipo haja kwa mamlaka husika kubuni mbinu za kuwasaidia ili waweze kufanya shughuli nyingine za kuwaletea maendeleo, badala ya kuendelea kushinda kwenye vituo wakiomba pesa na kuwaibia abiria.

Siyo vibaya yakaandaliwa mashamba na kisha wakapelekwa wakalime ama ukaandaliwa taratibu mwingine, ambao unaweza kuwa na manufaa kwa maisha yao badala ya kuwaacha wakiendelea na mtindo huo wa ombaomba.

Kingine cha kufanya ni kwa wamiliki wa daladala kuandaa utaratibu wa ajira kwa madereva na makondakta wao, ili wasiwe wanaingiliwa na wapigadebe ambao wametapakaa karibu vituo vyote vya daladala.

Nina uhakika iwapo madereva na makondakta watakuwa wameajiriwa haitakuwa rahisi kwao kugawa pesa kwa wapigadebe, kwa sababu watakuwa wanafanya kazi kwa kufuata taratibu za ajira.

Serikali itafakari na kisha ichukue hatua za kuwasaidia vijana hawa ambao wamegeuza vituo vya daladala kama vijiwe vyao ambavyo kimsingi haviwezi kuwasaidia zaidi ya kuwaharibia tu.