Mamlaka ziyamulike maduka yanayouza dawa za binadamu

07May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mamlaka ziyamulike maduka yanayouza dawa za binadamu

KUNA Janga kubwa linaloendelea kuzinyemelea afya za Watanzania walio wengi nchini, kwamba lisipodhibitiwa sasa na mamlaka zenye dhamana linaweka rehani maisha yao.

Janga ninalolizungumzia linatokana na uwapo wa maduka holela ya kuuza dawa yaliyotapakaa karibu kila kona ya nchi ambayo baadhi yake hutoa huduma hiyo bila kuzingatia kanuni, maadili na taratibu za kitabibu zilizowekwa.

Kimsingi maduka yanayouza dawa za binadamu yanapatikana karibu kila kijiji, miji na majiji yakiwa katika ngazi tofauti tofauti.

Kwamba maduka haya ni afya za watu, ni uhai na ustawi wa taifa kwani ukizungumzia maduka ya kuuza dawa vijijini kwa mfano, unagusa asilimia 70 ya Watanzania, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Muungwana anadiriki kusema kwamba baadhi ya maduka haya yamekuwa yakitenda kinyume cha sheria zilizoyaanzisha katika maeneo mengi.

Sababu kubwa ikiwa ni kujali fedha zaidi badala ya afya za watu na hivyo kukiuka taratibu na kanuni za kuanzishwa kwake.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi, iliruhusu kuanzishwa kwa maduka binafsi ya dawa katika dhima nzima ya kuboresha afya ya jamii.

Lakini mengi ya maduka haya yamekuwa hayaendi sambamba na sheria za uanzishwaji wake na hivyo kuipa kisogo dhima nzima hiyo ya serikali, inayolenga kuboresha afya ya jamii.

Sheria za uanzishwaji wa maduka haya zinataka mbali na usajili, ni lazima yawe na mtaalamu wa masuala ya famasia na yauze baadhi ya dawa za moto kwa kufuata maelekezo ya daktari yaliyoandikwa kwenye cheti cha mteja.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko ya visa vya muda mrefu dhidi ya wafanyakazi katika maduka haya kutofuata sheria za kuanzishwa kwake, huku wananchi na wadau wa afya zao wakitaka mamlaka zichukue hatua zaidi.

Hatua kali zitakazosaidia kuzuia janga la kiafya linaloendelea kutengenezwa kwa makusudi na wamiliki ama wafanyakazi wa maduka haya.

Mojawapo ya visa vinavyotishia afya za Watanzania, kilitokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam, ambapo mkazi mmoja aishie Tegeta alimpeleka mzazi wake mgonjwa katika zahanati moja ya serikali na kutibiwa.

Moja ya dawa alizoandikiwa na daktari haikuwapo katika zahanati hiyo na hivyo daktari akamshauri mkazi huyo akainunue kutoka maduka yanayouza dawa.

Mkazi huyo alienda katika duka moja la dawa akiwa na cheti cha daktari ambapo alipatiwa dawa na muuzaji kuwa ni dawa iliyoandikwa na daktari katika cheti alichokuwa nacho, na hivyo akaanza kumpatia mgonjwa wake.

Hata hivyo, baada ya siku nne kwisha bila hali ya mgonjwa kutengemaa, mkazi huyo alirudi kwa daktari ambapo daktari aliomba kuona dawa aliyokuwa akimpatia mgonjwa.

Kwa masikitiko makubwa daktari alikuta si ile aliyomwandikia mkazi katika cheti cha mgonjwa na akamshauri aende kwenye famasi yoyote kubwa katika eneo hilo la Tegeta, ambapo aliipata dawa halisi.

Dawa halisi iliyokuwa imeandikwa na daktari na kweli baada ya matumizi ya siku nne hali ya mgonjwa wake ilitengemaa.

Kuna mengi yanayoweza kuelezwa kutoka katika kisa hiki, lakini baadhi ni kuwa ama muuzaji katika duka hilo alijali pesa zaidi kuliko afya ya mgonjwa au hakuwa na taaluma ya famasia ambayo imeanishwa katika sheria, hivyo alishindwa kuelewa dawa iliyoandikwa na daktari.

Mojawapo ya mahitaji ya sheria ni kuwa na mwajiriwa aliye na utaalamu wa masuala ya famasia, kitu ambacho inawezekana hakifuatwi kwa mujibu wa kisa hiki.

Sasa kama hili lilitokea katika jiji la Dar es Salaam ambapo mamlaka zote zinazosimamia maduka haya zipo, vipi hali ilivyo vijijini?

Ni rai ya Muungwana kwa mamlaka zinazosimamia maduka haya zikachukua hatua sasa, vinginevyo kuna janga kubwa la kiafya linalowanyemelea Watanzania.