Maneno makali hayavunji mfupa,,,

26Sep 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maneno makali hayavunji mfupa,,,

MANENO tu hayawezi kuivunja mifupa, hata yakawa makali jinsi gani. Methali hii hutumiwa na mtu anayepuuza maneno yaliyosemwa na mtu mwingine na ambayo hayawezi kumdhuru kwa namna yoyote au hayamzuii kutekeleza jambo alitakalo. Watu wengine huamini kwamba, maneno ya kuudhi huweza kumtia uchungu mkali

Aidha, maneno ni kama fumo, yakitoka mdomoni hayarudi. Maana yake neno analotamka mtu ni kama mkuki, likitoka halirudi na huweza kuleta madhara.

Methali hii yatusihi tuwe na tabia ya kuyatafakari maneno tuyasemayo kabla. Ni vizuri kulipima neno, kabla ya kulisema na kujiletea majuto baadaye.

Mashabiki ni watu wenye mapenzi na hamasa kubwa ya jambo au kitu. Mara nyingi mashabiki wa kandanda, hasa kwa timu wazipendazo ni wepesi wa kusema maneno ya maudhi na hata kuwatukana wapinzani wao hadharani, bila kujali tofauti zao kiumri.

Idadi kubwa ya watu wa tabia hii si wanachama wa klabu husika, ila hufuata mkondo baada ya ushindi wa timu za kandanda, hasa Simba au Yanga inapoishinda ingine. Hawana wajualo kuhusu uendeshaji wa klabu zao, wala usajili wa wachezaji na makocha wao. Wahenga walisema “Mdomo siri ya gunda (baragumu).”

Maana yake siri yoyote aliyo nayo binadamu hujulikana na gunda kwa vile mdomo na gunda huhusiana sana. Mtu anayeweza kuzijua siri za mwengine ni yule anayehusiana naye kwa karibu. Mathalani, siri za mume azijua mkewe, kama mume anavyozijua siri za mkewe.

Husemwa na kuandikwa kwenye vyombo vya habari za michezo kuwa, Simba na Yanga ni ‘watani wa jadi.’ Sikubaliani na hilo kwani timu hizo, nionavyo, zastahili kuitwa ‘wapinzani wa jadi’ kwa jinsi zilivyo na uhasama kama walivyo Waarabu na Wayahudi!

Kisa ni gozi la ng’ombe. Ebo! (tamko linaloonesha hisia ya dharau inayotokana na kukasirika au kutoridhika). Ndivyo zinavyohasimiana Simba na Yanga ingawa zamani zilikuwa moja. Ni wanachama wachache wanaofungua vinywa vyao na kutoa maneno ya matusi wakati timu zao zinaposhinda, lakini wengi wao ni mashabiki wasiojua ‘be’ wala ‘te’ kuhusu klabu zao.

Waungwana hawaonekani mitaani wakiropoka na kuwatukana wenzao matusi ya nguoni! Kama timu mojawapo katika hizo ikitoa sare kwa timu ingine na kushangiliwa kuna ubaya gani hata mama zao watukanwe hadharani?

Msimu uliopita wakati Simba ilipotangulia kuifunga Yanga mabao 2-0, lakini ikasawazisha na kuwa sare ya mabao 2-2 mpaka mchezo ulipomalizika, wanachama na mashabiki wa Yanga walifurahi sana. Siku iliyofuata nikiwa maeneo ya Kariakoo barabara ya Sikukuu, nilimsikia shabiki wa Simba akisema:

“Hiyo sare Yanga wanachonga sana kwani kwao ni ushindi ...” kisha akatukana tusi la nguoni, ambalo hata yeye alipitia njia hiyo hiyo kuiona dunia! Naishi eneo la Kipunguni ‘A’ kupitia Banana, kuelekea maeneo ya Kitunda na kwingineko.

Pale Banana nafahamika na wauza matunda na mboga za aina mbalimbali; hata kwenye kituo cha daladala na bodaboda huniita kwa jina langu la mchezo wa maigizo (Mambo hayo) yaani ‘Baba Bishanga’ au ‘Mzee Kambaulaya.’

Wote hao wanajua uanachama na mapenzi yangu kwa Yanga; hivyo timu yangu inaposhindwa hunipa pole na wengine hunitania kwa maneno ya kawaida. Mimi huwafuata wapinzani wangu (Simba) walio waungwana na kuwapongeza kwa ushindi nao hunipongeza Yanga, inapoishinda timu yao.

Huo ndio uungwana, yaani hali ya mtu kuwa tayari kumfanyia mwingine wema na insafu (moyo wa ushirikiano). Sikatai kutaniwa na watani wangu (Simba) timu yangu inaposhindwa.

Huwapa nafasi ya kusema watakavyo, bila matusi na wanapomaliza tambo zao, huwaaga kwa kuwapongeza huku nikijitapa kuwa Yanga ndo kiboko kwao, kwani imetwaa Kombe la Ligi Kuu mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote nchini ikiwemo Simba yao.

Kwa kuwa Watanzania twaitana ndugu, ni vema nitumie methali ya wahenga wetu waliosema: “Kuishi na ndugu ni kuvumiliana.”

Kwamba mtu anayeishi na ndugu yake lazima amvumilie. Twafunzwa tuwe na subira na watu wanaotuhusu kama vile jamaa wa karibu. Pia “Kuishi kwingi ni kuona mengi.” Angalau Mungu ameniwezesha kufikisha umri wa miaka 82 tangu nilipozaliwa tarehe 24/8/1938. Mtu anayeishi kwa muda mrefu huwa ameshuhudia mengi. Methali hii yatunasihi kutowadharau wazee kwa kuwa wana busara inayotokana na uzoefu wa miaka mingi maishani.

Alhamdulillahi! (Tamko la kuonesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa mema anayoendelea kunifanyia.) Sasa niwazindue baadhi ya wacheza kandanda wa Tanzania, hasa waliojisajili au wanaotaka kujisajili kwenye timu za Yanga, Simba na Azam.

Wanapaswa kutambua kuwa gari ni chombo cha usafiri wa nchi kavu chenye magurudumu kinachotumia injini.

Kwa hiyo mtu anapokuwa na gari anapaswa kujua, bila hela gari haliendi kwani linahitaji petroli au dizeli, oili, mafuta ya breki, maji, matairi na uangalizi wa mara kwa mara ndipo liwe barabarani kila siku. Yote haya yanahitaji fedha.

Nyumba ni jengo la kuishi watu; manzili. Utunzaji wa nyumba ni rahisi kuliko gari. Nyumba inayotunzwa vizuri hudumu miaka mingi ndipo ifanyiwe marekebisho, hasa mabati au vigae. Wachezaji wasio na nyumba wasikubali kununuliwa magari ya kutembelea, bali waombe

kujengewa nyumba zitakazowafaa na familia zao badala ya magari. [email protected] 0784 334 096