Maneno ni kama fumo.

03Aug 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maneno ni kama fumo.

HUSEMWA “Maneno ni kama fumo, yakitoka mdomoni hayarudi.” Maana yake neno analotamka mtu ni kama mkuki (fumo), likitoka halirudi na huweza kuleta madhara.

Twanasihiwa tuwe na tabia ya kuyatafakari maneno tuyasemayo. Ni vizuri kulipima neno kabla ya kulisema na kujiletea majuto baadaye.

“Hadhari kabla ya hatari” maana yake ni vizuri kutahadhari kabla ya kufanya jambo tusije kufikwa na hatari au maangamizo. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na hadhari kabla ya kutenda mambo. Aidha, yatufunza tusiwe na tabia ya kudakia mambo bila ya tahadhari.

“Poteza” ni kitendo cha kusababisha kitu kuwa mahali kisipoonekana; sababisha kitu kipotee; pia tumia wakati vibaya. Hapa twapata potezana, potezea, potezeana, potezesha, potezewa na potezwa.

Gazeti fulani la michezo liliandika: “Kakolanya: Nitampoteza vibaya Manula.” Kichwa cha habari hiyo kilinishitua na kufanya nisome kwa makini ili nipate maana yake. Paragrafu ya nane kati ya 12 ndiyo iliyonivutia zaidi.

Aliongeza (Kakolanya): “Yanga nilikuwa namba moja, sikuwa napata ushindani, kitu ambacho kilinifanya nione nipo bora, kumbe nilijidanganya, lakini uwapo wa Manula Simba, utanifanya nipambane zaidi ili niwe bora zaidi na kumpora namba.”

Ukurasa wa mbele wa gazeti hilo kuna picha ya Kakolanya akitia saini kuthibitisha sasa ni mchezaji halali wa Simba. Chini ya picha hiyo kuna maneno haya: “Kakolanya: Nitampoteza vibaya Manula.”

Hapa ndipo paliponishitua. Mbona paragrafu zote 12 sikuona mstari wowote ulioandikwa Kakolanya kasema “Nitampoteza vibaya Manula?” Kama ndivyo, Kakolanya ana maana gani kusema “atampoteza vibaya Manula?” Maana ya ‘poteza’ ni kitendo cha kusababisha kitu kuwa mahali kusipoonekana. Maana ya ‘vibaya’ ni kisichokuwa katika hali nzuri.

Kama ni maneno ya mwandishi, yaweza kuleta chuki kati ya Kakolanya na Manula; kila mmoja kudhani mwenziye ni mshirikina anayetaka kumnyang’anya tonge mdomoni!

Hata hivyo, katika paragrafu ya tisa Kakolanya alinukuliwa kusema: “Yanga nilikuwa namba moja, sikuwa napata ushindani, kitu ambacho kilinifanya nione niko bora, kumbe nilijidanganya, lakini uwapo wa Manula Simba utanifanya nipambane zaidi ili niwe bora zaidi na kumpora namba.” Maneno ya “Nitampoteza vibaya Manula” yalitokea wapi?

“Hadhari kabla ya hatari.” Ni vizuri kutahadhari kabla ya kufanya jambo tusije kufikwa na hatari au maangamizo. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na hadhari kabla ya kutenda mambo. Tusiwe na tabia ya kudakia mambo bila ya tahadhari. Tuandike maneno yanayotamkwa na msemaji bila kuongeza yetu au kutia chumvi. Ni kumtilia mdomoni maneno ambayo msemaji hakuyasema!

‘Chama’ ni neno lenye maana tatu lakini nitaeleza moja tu ambayo ni muungano wa watu wenye lengo moja. Kundi lenye kufuata kaida au silka fulani zenye kuegemea dini, siasa, misimamo ya jamii, uchumi, michezo au jambo lingine lolote lenye maazimio maalumu.

Kila mkoa nchini una vyama vinavyosimamia maendeleo ya mchezo wa kandanda, navyo vipo chini ya uangalizi wa Shirikisho la Vyama vya Kandanda nchini, TFF. Hata hivyo Shirikisho hilo limejikita zaidi kwenye klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hasa Simba na Yanga!

Yanga walikuwa na shughuli maalumu iliyoitwa ‘Kubwa Kuliko’ (kuliko nini?) kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Lengo lilikuwa kupata shilingi bilioni 1.5 zitakazowasaidia kufanya usajili mzuri msimu ujao.

Kilichoshangaza wengi ni kutoonekana kiongozi yeyote wa juu wa TFF, ingawa walialikwa! Badala yake shirikisho hilo liliwakilishwa na Mwenyekiti wake wa Kamati ya Uchaguzi, Ally Mchungahela, jambo lililowahuzunisha wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga.

Yakatokea manung’uniko na malalamiko miongoni mwa waliokuwapo, wakisema hata Iftar iliyoandaliwa na klabu hiyo kwenye Hoteli ya Serena wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, viongozi wa TFF hawakuhudhuria, ingawa walialikwa! Kuna madai kuwa Simba ilipowaalika viongozi hao kushiriki Iftar walihudhuria.

Hali hii yaleta picha gani kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga kuona baba mmoja (TFF) akiwabagua wanawe? Nadhani hii ndio sababu iliyomfanya Rais mstafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwanasihi viongozi mbalimbali wa kandanda nchini kufanya uamuzi wa usawa bila kujali timu wanazozipenda.

Pia alizitaka klabu kubadilika ili kuwaendeleza vijana na wachezaji wazawa badala ya kuwajenga wachezaji wa kigeni wasiokuwa na faida kwa Tanzania.

“Chako ni chako, cha mwenzako sio chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nacho kuliko cha mtu mwingine. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuvitegemea vitu vyetu kuliko vya wengine. Kinachoishinda TFF kuwa na chuo maalum cha kukuza vipaji vya vijana watakaokuwa wawakilishi wetu kwenye michezo ya kimataifa ni kitu gani?

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alikemea ratiba ya ligi na kuitaka TFF kuifanyia mabadiliko ili kuleta usawa kwa timu zote bila upendeleo.

Hii ilitokea kwenye Ligi Kuu ya Bara ya msimu uliomalizika hivi karibuni. Ajabu mzunguko wa kwanza ulimalizika huku baadhi ya timu zikiingia mzunguko wa pili bila kukamilisha mzunguko wa kwanza!

Vilevile baadhi ya waamuzi walionesha dhahiri kutojua sheria 17 za mchezo wa kandanda au kufanya upendeleo kwa baadhi ya timu! Hii haishangazi Tanzania kutopeleka mwamuzi hata mmoja kwenye michuano ya Afcon iliyochezwa nchini Misri mwaka huu na Taifa Stars kutoka bila kushinda timu yoyote na kusababisha kocha Mnigeria Emmanuel Amunike kufukuzwa!

[email protected]

0784  334 096