Maneno yawapayo watu shida

23Jul 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Maneno yawapayo watu shida

KWA mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha (Zanzibar), lugha ya Kiswahili imepanuka sana na matumizi yake yameenea kwa kasi duniani kuliko watu wengi walivyotarajia. Imevuka kiwango cha kuwa lugha ya taifa na kuwa na hadhi ya kimataifa.

Sasa Kiswahili kimevuka mipaka ya Afrika Mashariki na kusambaa katika mabara yote ulimwenguni. Tayari kimekuwa miongoni mwa lugha zinazotumika katika mikutano ya kimataifa na mawasiliano ya intaneti (mtandao wa mawasiliano kimataifa wa kikompyuta).

Kutokana na mabadiliko na maendeleo hayo, pameibuka matumizi ambayo si fasaha, na mara nyingine si sahihi, katika mfumo wa sarufi, matamshi na hata maana ya maneno ya lugha hiyo.

Kwa mfano neno ‘kwa’ hutumiwa mno na wazungumzaji kama ilivyo vyombo vyetu vya habari. Neno hili lina maana nne: Linaunganisha sentensi mbili; neno linalotumika kuhusisha tendo na kifaa kinachotumika kutendea.

Neno linaloeleza namna tendo lilivyofanyika k.m. (“Amesoma kwa shida sana;” anaishi kwa mashaka (shida zinazompata mtu katika maisha); neno linaloeleza pahali tendo lilipofanyika: “Amepelekwa kwa daktari; ingawa ni mbali lakini amekwenda kwa miguu.”

Neno linaloonesha kwenda, kutoka au kukaa mahali panapomilikiwa na mtu mwingine: “Atakwenda kwa baba yake.” Namna, jinsi ya kutenda jambo: “Tembea kwa maringo.” Neno linalobainisha uwiano baina ya mambo mbalimbali: “Wamefungana mabao mawili kwa mawili.” Neno linaloonesha sehemu za hesabu kitarakimu kwa mfano: “Nne kwa tano (4/5).”

Neno linalotumika kuunganisha vitu viwili katika kulinganisha: “Walishindana nyumba kwa gari;” neno linalounganisha kitu kimoja na kingine katika utendaji. Pamoja na ufafanuzi huu, bado neno ‘kwa’ hutumiwa tofauti na maudhui (mambo yanayoelezwa katika hadithi, riwaya, hotuba, tamthilia au masimulizi yoyote yale) yake.

Hukereka (sumbuliwa na jambo; chukizwa) kila nisikiapo redioni, kwenye runinga au kusoma magazetini jinsi wanadamu wanavyolinganishwa na mtambo/mitambo! Mfano: “Bony atupia Ivory Coast ikitesti mitambo.” Neno ‘tupia’ nilikwisha eleza jinsi linavyotumika kwa hiyo niwieni radhi kwa kutolitanzua tena.

‘Testi’ si Kiswahili ingawa hutumiwa sana na magazeti yetu ya michezo. Maana yake ni jaribu, tahini; pima. Aidha ‘mtambo’ ni kifaa chenye kutoa nguvu za kuendesha vitu vinavyofanya kazi mbalimbali; kamba inayotengenezwa kwa chane za miyaa na hutumiwa kuvutia mtego wa samaki.

‘tupia’ nililitolea maana yake kwenye matoleo yaliyopita. Neno hilo latokana na ‘tupa’ lenye maana ya peleka au vugumiza kitu kisichohitajika kwenye kikapu au shimo la taka; acha bila kutunza; rusha kitu kutoka ulipo kwenda mbali. Pia ni kifaa kigumu cha chuma cha kukerezea au kunolea vitu vingine, mfano kisu, panga, jembe n.k.

“Yanga mpya balaa” ni kichwa kilichofuatiwa na habari ifuatayo: “Licha ya maneno ya kejeli kutokana kwa watani zao, Yanga wametamba kujua wanachokifanya kuhusiana na usajili wanaoendelea nao, hasa wa wachezaji wa kigeni.”

‘Balaa’ ni jambo, kitu au mtu anayefikiriwa kuleta maafa, mkosi au hasara; kisirani, nuksi. Pia ni jambo lenye kuleta hali ya kutoelewana; kizaazaa, mtafaruku, beluwa. Je, ni kweli kuwa Yanga mpya ni ‘hasara, kisirani au nuksi?’

Aidha sentensi ya mwandishi imeandikwa shaghalabaghala (shelabela; upogoupogo; bila mpango). Ingeandikwa: “Licha ya maneno ya watani wao, Yanga wanasema wanajua wanachofanya kuhusu usajili, hasa wachezaji wa kigeni.”

“Okwi: Sina bifu na Simba.” Wasiwasi wangu ni waandishi wa leo kushabikia sana maneno ya mitaani ambayo Waingereza huyaita ‘slang.’ Imenilazimu kutumia neno la Kiingereza ili kuwazindua waandishi wanaopenda sana matumizi ya kigeni ingawa yapo ya Kiswahili! Mwandishi angeandika: “Okwi hana kinyongo na Simba kwa kutoshirikishwa kwenye tuzo za MO Simba Award msimu huu.

Hata hivyo habari hiyo yenye aya (paragrafu) tano, mwandishi haelezi mtu aliyesema au wanaosema Okwi ana kinyongo kwa kutoshirikishwa kwenye tuzo za MO Simba Award. Malalamiko hufuatiwa na kinyongo. Mwandishi haelezi jinsi Okwi anavyolalamika hata kuwa na kinyongo alichokiita ‘bifu.’

Maana ya ‘beef’ ni nyama ya ng’ombe lakini pia kwa maana nyingine (kwa Waingereza wenyewe), ni maneno ya mitaani yakimaanisha kuwa na dukuduku, lalamika. Kwa mfano maana ya ‘beef up’ ni imarisha.

Jambo lingine lililonishangaza ni mwandishi wa habari husika kuandika sentensi moja iliyoelemewa (kwa muktadha huu, zidiwa na wingi wa maneno) na maneno 66 bila kidoto (nukta)!

Nimekuwa nikieleza kuna maneno ya kuandika na yanayozungumzwa lakini nafanywa ‘punguani’ (upungufu wa akili)!

“Straika mpya Yanga tema mate chini!” Hiki ni kichwa cha habari katika gazeti la michezo. ‘Straika’ si neno la Kiswahili ingawa latumiwa sana na waandishi wa habari za michezo. Neno hili kwa Kiingereza latokana na ‘strike’ na maana yake ni piga, gonga, bisha, chapa, mgomo. ‘strike at the roof of something’ yaani kata mzizi wa fitina; ondoa kiini cha tatizo. ‘Strike while the iron is hot” (methali). Maana yake chuma kikunje kingali na moto au samaki mkunje angali m-bichi.

Paragrafu ya tatu imeandikwa: “Mnamibia huyo mwenye miaka 27 ambaye amesaini Yanga mkataba wa miaka miwili ana kiasili ni straika lakini ana uwezo wa kucheza winga zote lakini pia kumbe ni mtamu akicheza kama kiungo mkabaji.”

Sentensi imeandikwa kwa haraka mno kiasi cha kutoeleweka! “ … ana kiasili ni straika” (haieleweki) “… ni mtamu akicheza kama kiungo mkabaji.” Mnyama ndiye ‘mtamu’ kutokana na nyama yake lakini mtu kusemwa ‘mtamu’ napata kigugumizi cha ghafla!

Methali: Maji ya pondo hayataki tanga.

[email protected]

0784 334 096