Maofisa elimu, wapangieni shule za karibu wanafunzi

17Mar 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mjadala
Maofisa elimu, wapangieni shule za karibu wanafunzi

KATIKA historia ya maisha ya binadamu, tofauti ya mawazo kati ya mtu na mtu, mtu na jamii na kinyume chake ni jambo la kawaida.

Ni jambo la kawaida kama ilivyo tofauti kati ya jamii moja na nyingine ama taifa na taifa au taifa na mataifa mengine.

Si jambo la ajabu kutokana na asili ya binadamu, kwamba ni vigumu sana kukuta watu wote au jamii nzima ina mtazamo unaofanana kuhusiana na jambo fulani, liwe la manufaa ama la.

Hata hivyo, katika mlolongo huo, kuna mambo ambayo kimsingi jamii pana hukubaliana kwa pamoja ama huwa na mtizamo unaofanana kwa kiwango kikubwa.

Sasa kati ya mambo ambayo watu wengi ama jamii pana hukubaliana au huwa na mtizamo mmoja, ni suala la elimu.

Wengi wanakubaliana kwamba, elimu ni ufunguo wa maisha na chanzo cha maendeleo ya mtu, watu, jamii, taifa, kanda na katika ngazi ya kimataifa kwa ujumla wake.

Na ndiyo maana watu na mataifa kwa upande mwingine yamekuwa wakiwekeza vya kutosha kwa ajili ya elimu ya watoto wao, na kwa hali hiyo wananchi wao.

Mfano halisi na ulio karibu ni ule wa serikali yetu, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

Serikali ya Dk. Magufuli inapeleka shilingi zaidi ya bilioni 18 kila mwezi kwa shule za sekondari na za msingi nchini, kugharimia mpango wa elimu bure.

Fedha ambazo zinatokana na kodi ya wananchi, na kwa kuwa zinafanya kazi inayokubalika na wengi, ndiyo maana karibu watu wote wanauunga mkono mpango huo.

Hawalalamiki kuwa serikali inapoteza fedha bure za wananchi kwa ajili ya kugharimia mpango wake huo.

Kwa nini, kwa sababu kama nilivyosema hapo juu, watu wengi wanaelewa umuhimu wa taifa kuwa na watu waliosoma, walioelimika.

Na ukitaka kujua namna ya wanavyotoa kipaumbele kwa elimu, angalia kwa mfano jinsi wanavyofuatilia matokeo ya ya mitihani ya taifa, ile ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na hata vyuo wakati mwingine.

Angalia namna shule zilizofeli zinavyopondwa au kunangwa, lakini kwa upande mwingine angalia shule zilizofaulisha watoto wengi zinavyopongezwa katika maeneo mbalimbali.

Yote hayo ni katika dhana ile ile kuwa watu wengi wanakubaliana juu ya umuhimu wa elimu na wangependa ikiwezekana kila mwanafunzi afaulu mitihani, tena kwa kiwango cha juu.

Kila mzazi, mwalimu na hata viongozi wa serikali wangependa watoto wafaulu mitihani yao ili taifa lipate wataalamu wa kada mbalimbali.

Lipate madaktari, wataalamu wa madawa, mainjinia, wataalamu wa miamba, madaktari, wataalamu wa kilimo, wahasabu, waandsihi wa habari, wanajeshi, mameneja, mawaziri na kadhalika.

Sasa ukiangalia shule nyingi na hasa za kata, bado hazijawa na mazingira mazuri ya kimiundombinu ya kuwawezesha wanafunzi walio wengi kufaulu vizuri.

Na ndiyo maana serikali na wadau wanajitolea kuhakikisha kuwa miundombinu kama vile maktaba, maabara, viwanja vya michezo, vyoo, nyumba za walimu na walimu wanakuwapo kama ikama ya shule inavyotaka.

Hata hivyo kuna ugumu wa mazingira mwingine ambao kimsingi unaweza ukatatuliwa kwa mipango tu ya kawaida ya viongozi wa elimu, kama maofisa elimu.

Kwa mfano wanafunzi wengi wanaofaulu kwenda sekondari hujikuta wanapangwa shule zilizo mbali na maeneo yao wanayoishi,
Unakuta mwanafunzi anaishi Tegeta jijini Dar es Slaam, amepangiwa shule iliyoko Mbezimwisho, hali inayomlazimu ili afike apande zaidi ya magari mawili.

Kuna shule ambazo humlazimu mwanafunzi asafiri umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwa siku, tena sehemu ambazo wakati mwingine hazina usafiri wa uhakika.

Analazimika kwenda shule zilizo mbali kiasi hicho kwa sababu ya kupangiwa tu, wakati huo huo jirani na kwao kuna shule ya sekondari ambayo angeweza kwenda kusoma na hivyo kumuondolea adha ya umbali kila siku.

Sasa umbali kama huo kwa vyovyote vile humchosha mwanafunzi, kwani ni lazima atachelewa kufika shuleni, lakini ni lazima vilevile atachelewa kurudi nyumbani.

Uchovu wa aina hiyo kimsingi huchangia kufeli katika mitihani yake na kwa kweli ni moja ya sababu zinazochangia wanafunzi walio wengi kufeli mitihani yao.

Lakini vilevile umbali kama huo, maana yake ni gharama kwa mzazi, kwa kuwa analazimika kugharimia zaidi upande wa nauli na hata fedha ya kula kila siku.

Nimesema hapo juu kuwa, hili linaweza kutatuliwa kirahisi zaidi na viongozi wa elimu, kama maofisa elimu, lakini kwa ushirikiano na wakurugenzi wa halmashauri za miji, wilaya, manispaa ama majiji.

Kwa hali hiyo mjadala unaona basi ni vizuri kwa viongozi hawa wakasaidia kwa hili, kwa kuwabadilishia shule zilizo mbali na makazi yao na kuwapangia za karibu ili kuwajengea moja ya mazingira yatakayowasaidia kufaulu mitihani kwa ustawi wao na taifa kwa ujumla.