Maridhiano ya kisiasa yapewe nafasi kabla ya mikutano

18Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maridhiano ya kisiasa yapewe nafasi kabla ya mikutano

MSINGI wa demokrasia unatajwa kwamba ni ushirika wa maridhiano, ambao unaweza kuunganisha pande mbili zinazotofautiana na hatimaye kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kutokana na hilo, hata wanasiasa wanapotofautiana katika mtazamo au jambo ambalo wanadhani linatakiwa kupatiwa ufumbuzi, hawana budi kutafuta maridhiano pale wanapoona mambo hayaendi sawa.

Nimeanza kwa kuelezea hayo kidogo, kufuatia kile ambacho kimetangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwamba kinatarajia kuanza mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia mwezi ujao.

Lengo la mikutano hiyo ni kudai tume huru ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria, hasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, ndiye aliyekaririwa na vyombo vya habari akisema hayo kwenye makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam hivi karibuni, lakini akagusia umuhimu wa suala la maridhiano.

Mbowe anasema kwamba kabla ya chama chake kuanza mikutano ya hadhara nchi nzima, anaona bado kuna nafasi ya kuchukuliwa kwa hatua za kutafuta maridhiano ya kisiasa.

Yapo mengi ambayo kiongozi huyo ameyaongea, lakini hili la maridhiano lingepewa uzito zaidi ili wadau wote wa siasa wakutane na kuweka mambo sawa kuliko kulazimisha kuwapo kwa mikutano.

Lakini, nikirejea kwenye hoja ni kwamba kutafuta maridhiano ni moja ya hatua za ukomavu wa kisiasa ambao unatakiwa kuendelezwa na zinaweza kusaidia kumaliza sintofahamu hiyo wanayolalamikia.

Pamoja na hayo, wanasiasa wanatakiwa kutambua kuwa umoja wa kitaifa ni muhimu kuliko vyama vya siasa, hivyo ulindwe ili usije kuwatenganisha Watanzania kwa itikadi za vyama vya siasa.

Ni muhimu kutambua kuwa maridhiano ndiyo njia pekee ya kumaliza mkwamo wowote ambao unaweza kujitokeza badala ya kutumia njia ambayo wakati mwingine inaweza isizae matunda mazuri.

Umuhimu wa maridhiano ni kwamba yanaepusha malumbano ambayo kwa kawaida huwa hayajengi, hivyo msuguano wa kisiasa uwe wa nguvu ya hoja siyo hoja za nguvu.

Vyama vya siasa vimekuja na vitapita, lakini Tanzania itaendelea kuwapo, hivyo jambo la kukazania ni kutafuta maridhiano ya kisiasa ili hatimaye sintofahamu, ambayo wanaiona imalizike.

Maridhiano au meza ya mzungumzo, mara nyingi huwa inasaidia kupata muafaka, kuliko kukaa pembeni na kulalamika au kususa ama kufanya jambo ambalo wakati mwingine halina afya kwa umma.

Hatua ya viongozi wa upinzani kutoa wito wa kuwapo maridhiano ya kisiasa mbele ya Rais John Magufuli, ninaitafsiri kuwa ni dalili za kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa siasa za maridhiano.

Siasa hizo ndizo ambazo zinaweza kujenga umoja wa kitaifa, kwa kutanguliza maslahi ya nchi kwanza badala ya vyama, hasa kwa kutambua kuwa vyama vya siasa vinapita, lakini Tanzania itaendelea kuwapo hadi ukamilifu wa dahari.

Kwa hiyo juhudi za wadau wa siasa kutafuta namna ya kukutana kwenye meza ya mazungumzo ni za muhimu kwa ajili ya maridhiano ya kisiasa kwa manufaa ya taifa na watu wake.

Lakini pamoja na hayo, subira na uvumilivu ni mambo ya msingi na ndivyo ambavyo vinaweza kuzaa muafaka iwapo suala la meza ya mazungumzo kwa ajili ya maridhiano litapewa nafasi.

Kwa sababu Mbowe ameonyesha bado anahitaji maridhiano, basi asichoke kuyatafuta, kwani kuna msemo wa Kiswahili kwamba; Mvumilivu hula mbivu na atafutaye hachoki, hivyo yote yanahitajika.