Marufuku mifuko ya plastiki jamii isome ishara za nyakati

22May 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Marufuku mifuko ya plastiki jamii isome ishara za nyakati

MWISHO wa matumizi ya mifuko ya plastiki ni Juni Mosi mwaka huu, na serikali imeshatangaza kuwa haitarudi nyuma katika hilo na kuwataka watu wote kuzingatia tarehe hiyo.

Hata hivyo, kumekuwapo na upotoshaji wa mitaani ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakijifariji kuwa ni masuala ya kisiasa tu na kwamba mifuko hiyo itaendelea kuuzwa kama kawaida.

Watu wa aina hiyo wanapaswa kupuuzwa kwani wanaweza kusababisha wenzao wakaingia kwenye matatizo kwa kutozwa faini watakapokutwa na mifuko hiyo, baada ya muda ulioweka kumalizika.

Msimamo wa serikali ni kwamba haina mpango wa kuongeza muda kwa wamiliki wa viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki iliyopigwa mafuruku, hilo ndilo jambo la msingi la kuzingatia.

Ni vyema watu wakasoma ishara za nyakati na kutambua kwamba serikali hii hailembi, kwa kuwa ikishaamua, kinachofuata ni utekelezaji tu, hivyo ni muhimu Watanzania kuzingatia hilo.

Itashangaza iwapo Juni 2 mwaka huu kutakuwa na watu ambao watakutwa na mifuko hiyo, wakiamini kwamba serikali imetangaza na kisha italegeza msimamo au itaongeza muda.

Siyo vyema kukumbana na hali hiyo kwasababu tu ya uzembe na hasa kwa kuzingatia kwamba zimebaki siku chache ule muda uliowekwa na serikali wa kupiga marufuku mifuko hiyo utumie.

Yale ambayo yamekuwa yakiwakuta baadhi ya watu kwa uzembe wa kutozingatia muda, hayapaswi kufanywa kwenye suala hili la marufuku ya mifuko ya plastiki ambalo lina faini yake.

Kwa mfano wakati uandikishaji wa vitambulisho vya taifa unaanza, baadhi walikosa, kutokana na mtindo wao wa kusubiri hadi siku ya mwisho na kukuta msururu mrefu wa watu na hivyo wakakwama kuhudumiwa.

Siyo vitambulisho tu bali hata kuhama kwenda kwenye televisheni za ving'amuzi, wengine walizembea na kushindwa kubadilisha zao kwa wakati na kujikuta zikizimwa.

Mimi ninaamini kwamba mtu atakayekutwa na mifuko hiyo kuanzia Juni 2 mwaka huu, basi atakuwa ni mzembe au atakuwa miongoni mwa wale wanaosikiliza maneno ya mitaani.

Wakumbuke kuwa kwa sasa kuna matangazo ya mara kwa mara kwenye vyombo vya habari na hata ujumbe unaotumwa katika simu ukisisitiza kwamba mifuko hiyo ni marufuku ifikapo Juni Mosi.

Kwa maana hiyo sidhani kuna mtu atakayejitetea kwamba hajui marufuku hiyo, kwani atakuwa hana ujanja wa kujitetea, kwa sababu kumekuwapo na njia nyingi za kufikisha ujumbe kuhusu suala hilo.

Kama hana TV, redio au simu, basi atakuwa amepata ujumbe kupitia kwa ndugu, rafiki au jirani, vinginevyo atakuwa ni miongoni mwa wale wanaosubiri hadi dakika ya mwisho ili 'waibipu' serikali.

Kila mmoja aepuke kutozwa faini ambayo imetangazwa kuwa ni Sh. 30,000 kwa yule atakayekutwa akitumia mifuko hiyo baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa na serikali.

Wakati serikali ikiweka faini hiyo, Baraza la Madiwani Manispaa ya Moshi limepitisha sheria ndogo itakayodhibiti mifuko hiyo.

Kwamba kwa wale watakaokamatwa nayo, watalipa faini ya Sh. 50,000.

Bado wapo wafanyabiashara wa maduka ya jumla na rejareja, ambao wanataka jamii ipewe elimu kuhusu mifuko hiyo, lakini sidhani kama haijawahi kutolewa tangu serikali ilipotangaza marufuku miaka kadhaa iliyopita.

Nakumbuka siyo mara ya kwanza serikali kupiga marufuku mifuko hiyo, kwani miaka kadhaa iliyopita ilifanya hivyo lakini ikawa inaishia njiani na sasa imeamua kufanya kweli na ndio maana kumekuwapo na matangazo ya mara kwa mara yakisisitiza kuwa Juni Mosi ni mwisho.

Hatua hivyo inatosha kuwafanya Watanzania wajue kuwa imedhamiria kukomesha mifuko hiyo nchini, na kinachotakiwa ni jamii kutii.