Mashabiki wanapopenda wachezaji kuliko klabu

15Jul 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mashabiki wanapopenda wachezaji kuliko klabu

KATIKA miaka ya hivi karibuni, kumezuka kizazi cha baadhi ya mashabiki wa soka kupenda zaidi wachezaji kuliko klabu zao.

Haijulikani kwa nini, lakini baadhi ya mashabiki kwa sasa wameonekana wakiumia mno baadhi ya wachezaji wakiondoka kwenye klabu zao kwenda kutafuta malisho sehemu nyingine.

Kwa kawaida mchezaji ni kama mfanyakazi ambaye analetwa kwenye kampuni kuitumikia kwa muda ambao wamekubaliana na mwajiri wake, na mkataba ukimalizika, wanaweza kukaa na kuamua kuendelea au kutoendelea.

Na hapa inawezekana mwajiri asiridhishwe na huduma ya mfanyakazi wake akaamua kumuacha, au mfanyakazi asitake tena kuendelea hapo, ama kuamua kubadilisha upepo na kwenda sehemu nyingine.

Hiyo ndiyo ipo hata kwenye soka. Lakini kwa Tanzania sasa eti linaanza kuonekana jambo la ajabu na baadhi ya mashabiki kuanza kuwalaumu na kuwashutumu wachezaji wanaoondoka, kuhama, pia wapo wanaowalaumu viongozi wa klabu eti kwa nini wamewaacha wachezaji.

Nitoe mifano ya hili. Ibrahim Ajibu na Gadiel Michael wameondoka Yanga baada ya kumaliza mikataba yao, na wakajiunga na klabu ya Simba.

Kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitoa maneno ya kejeli, shutuma kisa kwa nini nyota hao wamehama.

Hii ikasababisha mpaka Gadiel aandike waraka wa kuwaomba radhi baadhi ya mashabiki wa Yanga wenye 'nongwa'. Sidhani kama mchezaji huyo alipaswa kufanya hivyo kwa sababu hakuna lolote baya ambalo amelifanya.

Ni kwamba mkataba na klabu umekwisha na yeye binafsi hakuwa na mpango wa kuongeza, akili yake tayari ilikuwa kwingine.

Tunakwenda kwenye klabu ya Simba. Emmanuel Okwi ameamua kuondoka. Baadhi ya mashabiki wamekuwa akimwandikia waraka mkali kuwa hajaitendea haki klabu ya Simba kwa sababu ndiyo iliyompa jina na kwa nini ameiacha kwa staili hiyo? Ni kwamba amemaliza mkataba na Simba na ameamua kufuata malisho sehemu nyingine.

James Kotei na Haruna Niyonzima wameondoka baada ya kumaliza mikataba yao, lakini baadhi ya mashabiki wanawashutumu viongozi kwa nini wamewaacha.

Ukiangalia haya yote, sababu yake ni moja tu. Imefikia wakati mashabiki wanawapenda zaidi wachezaji kuliko klabu. Ndiyo maana wakiondoka wanaumia. Wanatoa maneno ambayo hayastahili.

Yeyote anayependa klabu, anajua kuwa watakuja wachezaji wazuri, wenye vipaji, wanaoweza kuwa tegemeo kwa timu, lakini mwisho wa siku wataondoka na kuiacha klabu ikiwa pale pale, ikisajili wachezaji wengine na maisha yanaendelea.

Ndiyo maana leo Yanga haina kina Mbuyu Twite, Vicent Bossou ambao walikuwa tegemeo kubwa, lakini kwa sasa hata kuna baadhi ya mashabiki wameshaanza kuwasahau.

Walikuwapo kina Ben Mwalala na Boniface Ambani, mastraika hatari sana ambao Yanga iliwahi kuwa nao miaka ya hivi karibuni tu, lakini wamesahaulika, hivyo kuondoka kwa Heritier Makambo na Ajibu hakuwezi kuiathiri, Yanga, itaendelea kuwapo.

Mashabiki wa Simba wakumbuke kuwa timu yao ilishawahi kuifunga Yanga mabao 3-1, Okwi akiichezea Yanga, hivyo sidhani kama kuondoka kwake kunaweza kuwa pengo kubwa na haiwezi kufanya chochote bila yeye.

Niyonzima hakucheza kipindi kirefu kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na Simba ilipata matokeo, alianza kuonekana kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, leo hii baadhi yao wanaona kama hakuna maisha ya Simba bila mchezaji huyo.

Hata kwenye miaka ya '70, '80 hata '90 kumetokea wachezaji bora kabisa wa klabu hizo na kuzipa sifa kubwa zilizonazo kwa sasa, lakini kwa sasa hawapo, lakini zenyewe zipo na zinaendelea kupata wachezaji bora kila kukicha.

Kikubwa ni kuzisapoti klabu na kuachana na tabia ya kupenda zaidi wachezaji, kwani wao wanaingia na kutoka, lakini zenyewe zinabaki vile vile.