Maslahi wenye mahitaji maalumu yaingizwe kwenye miradi ya maendeleo

14Nov 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maslahi wenye mahitaji maalumu yaingizwe kwenye miradi ya maendeleo

KUNA sura mbalimbali za kundi la watu ‘wanyonge’ ama walioko pembezoni katika jamii kihistoria.

Wapo watoto ama vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu maarufu kwa jina la ‘watoto wa mitaani’.

Kazi yao kimsingi huwa ni kuombaomba kila siku katika mitaa na makutano tofauti ya majiji na miji kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga, Dodoma na miji mingine.

Lipo kundi la vijana wanaoshinda kwenye vituo vya mabasi wakipiga debe au watu wanaoishi maeneo duni ya miji ambayo kwa sehemu kubwa yamejengwa bila ramani ya mipango miji.

Makundi yote haya yanachukuliwa kuwa ni watu walio pembezoni.

Ni kawaida kukuta nyumba katika maeneo haya zimebanana, vyoo vyake vikisitiri sehemu tu ya mwili wa binadamu na mazingira yake kwa ujumla kiafya si ya kuridhisha.

Aidha, kinamama na watoto wanaingia pia kwenye kundi hili na ndiyo maana kampeni nyingi zimekuwa zikiendeshwa kwa minajili ya kunyanyua makundi haya kiuchumi kupitia programu mbalimbali za maendeleo.

Sasa sambamba, lipo kundi jingine lenye mahitaji maalumu linalohusiana na walemavu wa aina mbalimbali za viungo kama vile wenye ulemavu wa macho, kutosikia, ngozi, miguu na mikono.

Kimsingi makundi yote haya nayo yanahitaji kufurahia fursa za kijamii katika kiwango sawa na wengine kwa ajili ya maendeleo yao.

Ukitizama mifumo inayotawala katika jamii zetu linapokuja suala la kufaidi huduma za kijamii, kupitia programu na miradi mingi inayoendeshwa kwa manufaa ya wananchi, mara nyingi huwa haizingatii mahitaji ya walioko pembezoni.

Na ndiyo maana si ajabu kukuta majengo mengi yanayotoa huduma za kijamii hayana huduma za watu wenye mahitaji maalumu.
Utakuta baadhi ya ghorofa au vyoo vya umma kwa mfano havikuzingatia maslahi ya makundi yenye mahitaji maalumu.

Aidha, nyingi ya shule zilizojengwa na baadhi ya zinazoendelea kujengwa hazitilii maanani mahitaji ya makundi haya.

Nimesema yote haya nikidhamiria kuonyesha kwamba jamii kama jamii bado haijatoa kipaumbele kwa maslahi ya makundi haya kwenye miradi na programu zinazohusu maslahi ya wananchi.

Muungwana ameamua kuangazia upungufu huu unaoonekana kuendelea ndani ya jamii, baada ya kubainishwa pia hata kwenye eneo la miundombinu ya barabara.

Aliyelibainisha upungufu huu ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika Ripoti yake ya Ukaguzi aliyoitoa mwezi Machi mwaka huu, CAG amebainisha namna barabara nyingi nchini zisivyo na alama za barabarani kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu.

CAG anasema kwamba katika barabara alizozitembelea nchini kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya na Mtwara, nyingi hazikuwa na alama za barabarani zinazozingatia usalama wa watu wenye mahitaji maalumu.

Hiyo ni pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) anayehusika na uwekaji wa alama hizi kuwa na bajeti ya kuweka alama kwa ajili ya kundi hilo katika jamii.

CAG anasema kwa mfano kwamba katika Mwaka wa Fedha wa 2015/ 2016, TANROADS ilitenga kiasi cha Shilingi milioni 309.7 kwa ajili ya kuweka alama za barabarani za kundi hilo, lakini anasema ni asilimia 15 tu za alama zilizotakiwa kuwekwa ndizo ziliwekwa.

Anabainisha kwamba ofisi za TANROADS za mikoa ambazo zina jukumu la kufanya kazi hiyo, zilitumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli zingine kutegemeana na kipaumbele cha wakati huo.

Kwa maana nyingine, kama ilivyo katika maeneo mengine niliyoyataja hapo juu, kipaumbele kwa ajili ya kundi la walioko pembezoni hakitiliwi maanani linapokuja suala la huduma za kijamii au miradi mbalimbali ya wananchi.

Muungwana anaona wakati sasa umefika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kugharimiwa nchini ikazingatia kipengele cha watu wenye mahitaji maalumu.

Hii itasaidia kuifanya miradi hiyo iwe jumuishi, badala ya kupendelea kundi fulani katika jamii kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.