Masomo yanavyoanza wanafunzi mmejipanga?

23Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Masomo yanavyoanza wanafunzi mmejipanga?

WAKATI shule za msingi na sekondari zikitarajia kuanza masomo wiki ijayo, tayari serikali imeshatoa ratiba ya kuwezesha wanafunzi kufidia muda ambao walikaa nyumbani kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Katika ratiba za masomo za kila siku, zimeongezwa saa mbili mara tu shule zitakapofunguliwa, huku walimu na wafanyakazi wakitakiwa kuzingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi.

Pamoja na lengo hilo zuri la serikali, ni wajibu wa wanafunzi wenyewe kutambua umuhimu wa elimu ili saa hizo mbili zilizoongezwa zisipotee na badala yake ziwe na manufaa kwao.

Nafasi hii kama wataitumia vizuri, wanaweza kusoma kwa bidii, ili kuhakikisha wanafaulu mitihani yao na kufanikiwa kwenda mbele kana kwamba hawakuwa na likizo ndefu iliyotokana na tishio la corona.

Kwa zaidi ya miezi mitatu ambayo wanafunzi walikuwa nyumbani wakisoma kwa njia ya televisheni na mitandao ya kijamii, huku wengine wakipelekewa masomo nyumbani na walimu wao.

Lakini, ujifunzaji huo ni wazi kwamba hauwezi kuwa kama ambavyo mwanafunzi anapokuwa darasani na mwalimu wake, hivyo kuongeza muda wa saa mbili kunakusudia kuwaweka wanafunzi sawa zaidi.

Kwa hiyo kama ambavyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alitangaza ratiba za mitihani ya taifa darasa la saba, kidato cha nne na upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili.

Hivyo utaratibu huo uliotangazwa na serikali ni wa muhimu iwapo utazingatiwa ili kuhakikisha wanafunzi wanafaidika na masomo, hasa wale wanaojiandaa kufanya mitihani ya taifa.

Lakini, anasisitiza kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kuhakikisha shule zinanunua vifaa vya kutosha kwa ajili ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Waziri anatoa ratiba hiyo baada ya Rais John Magufuli, kuagiza shule zote za msingi na sekondari kufunguliwa Jumatatu Juni 29, na kuruhusu shughuli nyingine za kijamii zilizokuwa zimezuiwa kuendelea kama kawaida.

Kwamba wanafunzi watalazimika kusoma saa mbili zaidi katika ratiba za masomo, angalau kufidia muda ambao walikaa nyumbani wakati wa sakata la kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Hivyo hiyo ni nafasi nzuri kwa wanafunzi kuchangamkia hizo saa mbili zilizoongezwa katika ratiba za masomo ili kujiandaa vizuri kwa ajili ya mitihani ya taifa ambayo iko mbele yao.

Saa hizo zimeongezwa kwa kusudi maalum hivyo ni vyema wanafunzi wakazingatia ratiba hiyo ili mwisho wa siku iwanufaishe, kwa kuwa ni muhimu wawe na maandalizi ya kutosha kabla ya mitihani.

Ratiba iko wazi kwamba shule za msingi na sekondari wanafunzi watarejea shuleni Juni 29, mwaka huu na kumaliza muhula wa kwanza wa masomo Agosti 28, na kuanza muhula wa pili ambao utaisha Desemba 18.

Kwa mujibu wa wizara husika, ratiba ya mitihani ya darasa la saba itaanza Oktoba 7 hadi Oktoba 8 mwaka huu, huku kidato cha pili ikianza Novemba 9 hadi Novemba 20 mwaka huu.

Nao kidato cha nne wanatarajia kuanza mitihani Novemba 23 hadi Desemba 11 mwaka huu na darasa la nne wataanza Oktoba 25 hadi Oktoba 26 mwaka huu, hivyo umuhimu wa saa mbili za ziada upo palepale.

Hii inatokana na ukweli kwamba, ili kukamilisha muhtasari wa masomo, shule zitalazimika kuongeza saa mbili za masomo kwa ajili ya kufidia muda uliopotea kama ambavyo Prof. Ndalichako anasema.

Ni wajibu wa wanafunzi kuzingatia ratiba hiyo ili iwe na manufaa kwao, kwani baadhi yao huwa wana kawaida ya kukwepa vipindi vya masomo ni wepesi wa kujificha wakikwepa masomo na kwenda kucheza.

Wanafunzi wa aina hiyo wadhibitiwe na inawezekana ndiyo hao ambao hata wakati wa likizo walikuwa hawafuatilii masomo kupitia televisheni, redio au mitandao ya kijamii, hivyo wasaidiwe kuachana na mtindo huo.

Kuzingatia ratiba ya masomo kunaweza kusaidia kuboreshwa na hasa wakati huu ambao Tanzania inajipanga kufikia uchumi wa viwanda 2025, kwa kuandaa wataalamu wa baadaye.