Matokeo ya uchaguzi wachache tuliona kilichowashinda wengi

08Nov 2020
Nkwazi Mhango
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Matokeo ya uchaguzi wachache tuliona kilichowashinda wengi

NILIPOANDIKA makala “Kwa mtaji huu upinzani utashindwa tu” muda mfupi kabla ya kupiga kura kuwa wapinzani wangeshindwa vibaya, wapo walioniona kama mtu anayejipendekeza kwa chama tawala wasijue ukweli utasimama tena si baada ya kitambo kirefu. Sasa matokeo yametoka, na ukweli umejulikana.

Uyakubali hata uyakatae, waliodhani nilikuwa nakipendelea chama tawala hawana la kusema bali kushangaa ilikuwaje japo ilikuwa rahisi kutabiri kipigo kilichotokea. Hata kama hupendi kitu, kusema ukweli ni sehemu mojawapo ya kukusaidia kufikisha kile unachoamini au kutaka kuwasilisha. Pia kuukubali ukweli husaidia kimkakati kupambana na kile unachotaka kupambana nacho kisayansi na si kwa kujilisha pepo au kutegemea miujiza.

Kwa wanaojua namna Watanzania walio maskini wanavyomuunga mkono Rais John Pombe Magufuli, hawakushangaa kwangu kutabiri kuwa chama tawala kingeshinda ki-Tsunami. Hii ni kutokana na sababu zifuatazo:

Mosi, wengi wa wapiga kura ni wakazi wa vijijini wakilinganishwa na wasomi wachache wa mijini ambao mara nyingi ndiyo wanaounga mkono upinzani ukiachia mbali kuwa uzoefu unaonyesha kuwa wengi hawapigi kura. Mfano, mzazi ambaye mtoto wake sasa anasoma bure huwezi kumshawishi akuchague na kumuacha aliyewezesha mwanawe kupata huduma hii. Raia ambaye tangu taifa lipate uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita bila kuona barabara ya lami au bomba la maji, huwezi kumshawishi akuchague amuache aliyewezesha kupatikana kwa huduma hizi tena ndani ya miaka mitano tu?

Pili, mwanakijiji ambaye tangu tupate uhuru ameishi kwa kibatari halafu ghafla, ndani ya miaka mitano, akapata umeme huwezi kumwambia kitu. Kama kuna siri ya wapinzani kuangusha vibaya, si nyingine bali hii. Wapo waliokejeli kuwa Watanzania sasa wanasifia, barabara, flyover, kusambazwa umeme, mabwawa ya kuzalisha umeme, madaraja, meli, ndege, reli, umeme na mengine mengi. Je, walitaka wasifie nini wakati hizi ni nyenzo za maendeleo?

Tatu, mama aliyekuwa akijifungulia nyumbani au kwenye zahanati inayotegemea kibatari asingeweza kuchagua yeyote zaidi ya yule aliyewezesha kupatikana huduma ya uhakika. Mamantilie aliyekuwa akimwagiwa chakula chake na migambo au machinga akifukuzwa na kukamatwa ovyo ovyo asingemchagua yeyote zaidi ya aliyekomesha kadhia hizi. Mwananchi mchukia rushwa asingeweza kumchagua mwingine zaidi ya yule aliyeikomesha. Aliyekuwa akisafiri kupitia nchi jirani kwenda Dar asingemchagua yeyote zaidi ya aliyetatua tatizo lake.

Nne, mwananchi aliyekuwa amekosa kazi tokana na ajira nyingi kuchukuliwa na walioghushi au kutolewa kikabila, asingeacha kuchagua aliyekomesha kadhia hizi. Hapa hatujaongelea usalama kwa ujumla. Mikoa iliyozoea kutekwa kwa magari usiku na kushamiri kwa vitendo vya ujambazi asingechagua wapinzani hata wangemwimbia mashairi mazuri kiasi gani.

Tano, ukizingatia ukweli hapo juu, utagundua kuwa hata malalamiko juu ya matokeo ya uchaguzi uliokwisha na kukipa chama tawala ushindi mnono, yatahitaji ushahidi wa nguvu kweli kweli kusimamisha kesi ya msingi. Kwani, madai yanayotolewa kwa sasa, kimahesabu ya kura na matokeo, yanakosa uzito japo hatupingi kulikuwa na matukio yaliyoripotiwa bila kutolewa ushahidi. Hii ni kazi ya mahakama; si kazi ya uchambuzi. Tunaambiwa kura za urais za Magufuli ameshinda kwa kura zaidi ya 12,000,000 dhidi ya mpinzani wake wa karibu aliyepata kura takriban 1,000,000. Hii maana yake nini? Je, mshindi alipewa kura ngapi feki au tuseme mshindwa aliibiwa kura ngapi? Wangepishana kura kama elfu kadhaa, madai ya wizi wa kura yangeweza kujenga ushawishi hata kama yangekuwa ya kuzua. Kwa hali ilivyo, tukubali, upinzani umeshindwa vibaya ikilinganishwa na uchaguzi wa kabla.

Tulishaeleza ni kwanini upinzani ulifanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambazo tunaweza kufupisha kuwa ni kama ifuatavyo:

Mosi, chama tawala kilikuwa kinamekumbwa na kashfa kibao ukiachia mbali kutamalaki kwa rushwa wakati ule ikilinganishwa na sasa ambapo serikali iliyochukua madaraka baada ya hapo ilifanya mageuzi makubwa kisiasa na kiuchumi hata ndani na nje ya chama tawala na serikali yake.

Pili, katika uchaguzi wa mwaka 2015, mgombea wa chama tawala aliyeshinda alikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kupitishwa kugombea nafasi hiyo tena akishindana na mgombea wa upinzani aliyekuwa na uzoefu na jina kubwa kuliko yeye.

Tatu, Watanzania walikuwa wamezoea siasa za mazoea. Baada ya kuonja mafanikio ya muda mfupi kama vile kuingia kwenye uchumi wa kati, kurejesha tunu zilizokuwa zimepotea muda mrefu kama Shirika la Ndege la Taifa la Air Tanzania, kufumua mfumo uliokuwa umeoza kwa ufisadi, ukabila, mazoea na wizi, huwezi kuwaambia kitu wala kuwarudisha nyuma.

Nne, kimsingi Watanzania hawakuwa na mahitaji au maswali mengi kwa serikali au anayetaka kuwaongoza ikizingatiwa ukweli kuwa serikali iliyokuwa imemaliza muda wake ilikuwa imejibu karibu maswali yote na ya ziada kiasi cha kuwafanya waridhike nayo; na hivyo kuiamini miaka mitano mingine.

Mwisho, chama tawala kiliendesha kampeni za kisayansi kikiahidi ‘maajabu’ zaidi ya yale ambayo Watanzania wengi walikuwa wamekishangaa na kuridhika nayo. Kimsingi, badala ya wapinzani kulalamika, wajipange upya kutegemeana na mambo yatakavyo kuwa kwenye miaka mitano ijayo. Ni ushauri wa bure.