Matumizi mitandao yawabadilishe vijana

17Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Matumizi mitandao yawabadilishe vijana

KATIKA miaka ya hivi karibuni kasi ya matumizi ya teknolojia ya mitandao ya kijamii, imekuwa ni kubwa, lakini ikiwa imegawanyika katika sura mbili, ambazo ni nzuri na mbaya.

Nikianzia na nzuri, kukua kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, watu wengi zaidi wanaweza kupata habari na elimu juu ya mambo mbalimbali kirahisi tofauti na enzi hizo.

Kimsingi ongezeko la watumiaji wa mitandao ya kijamii ni jambo zuri kwa maendeleo ya nchi, kwani inasaidia katika upashanaji habari na taarifa muhimu za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Lakini pamoja na faida hizo na nyingine nyingi, jamii imeshuhudia uholela wa matumizi ya mitandao jambo ambalo limeathiri baadhi ya vijana kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao hiyo.

Ni vyema ikaeleweka kuwa mitandao hiyo si tu sehemu ya mawasiliano, bali pia kimaendeleo katika jamii nyingi, hasa kwa vijana, ambao inasemekana wengi ni ndiyo watumia wakubwa.

Hivyo wanatakiwa kuitumia inavyotakiwa, kwani imekuwa ikidaiwa kuwa kuwa wapo baadhi ya vijana wanaoutumia vibaya na kujikuta katika mazingira ya hatari bila wao kujua au wakiwa wanajua.

Mitandao ya kijamii inadaiwa kuchochea vitendo vya ngono miongoni mwa vijana na kuwasababisha kuwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwamo hata Ukimwi.

Hii inaelezwa kuwa inatokana na matumizi mabaya, na kwamba iwapo vijana wataitumia mitandao hiyo vizuri, wanaweza kupata manufaa makubwa kwa ajili ya maendeleo yao ya baadaye.

Vijana wanakumbushwa kuwa kuna faida nyingi kutumia mitandao ya kijamii inavyotakiwa, kwa vile ina fursa nyingi ikiwamo kupata nafasi za kujiendeleza kielimu.

Huu ni wito kwa vijana unaotolewa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP, Lilian Liundi, wakati akizungumza na wasichana kutoka vyuo mbalimbali vya vijijini Dar es Salaam.

Aidha, anawaambia wanatakiwa kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili waweze kujiendeleza kielimu, kupata ajira na hata kufanyabiashara kwa ajili ya maendeleo yao ya baadaye.

Anawakumbusha kuwa wao ni kizazi ambacho kinatakiwa kuwa makini katika matumizi ya mitandao hiyo kwa kutojiingiza kwenye mambo yasiyofaa, ambayo mwisho wa siku ni matatizo.

Kinachosemwa na mkurugenzi huyu ni ukweli kwani kumekuwapo na malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ambayo imechangia kuwaharibu baadhi ya vijana.

Yaani ni kwamba umefika wakati mitandao ya kijamii iwe ni faida kwa vijana badala ya hasara, kwa sababu tu ya kutoelewa au kuzembea matumizi ya sahihi yanayotakiwa kuzingatiwa.

Siyo siri kwamba vijana wengi wakiwamo wanafunzi, ndiyo wanaotumia mitandao ya kijamii na inaweza kuwasaidia katika masuala mbalimbali yakiwamo ya elimu, lakini wakienda kinyume wajue kuwa watakwama.

Wakumbuke kuwa mitandao hiyo inaweza kuwasaidia wanafunzi kupata hata ufadhili wa kielimu katika nchi mbalimbali na pia kuunganisha watu wa rika mbalimbali katika kujadili masuala muhimu.

Kimsingi mitandao ya kijamii ni muhimu kwa vijana kwa kuwasaidia kujadili masuala ya maendeleo na ndiyo maana mkurugenzi wa TGNP anasisitiza umuhimu wa kuitumia vizuri ili iwanufaishe.

Vilevile mitandao ya kijamii inawajengea uwezo vijana, inawasaidia kuibua vipawa na vipaji vyao na kuvitumia katika kujiingizia vipato, hivyo umuhimu wa matumizi sahihi ni mkubwa.

Inaelezwa kuwa mitandao yote ya kijamii hutoa maelekezo na makatazo muhimu kwa mtumiaji juu ya mambo ya kuzingatia wakati wa kujiunga lakini baadhi ya watumiaji huwa wanayapuuza.

Badala ya kuitumia kwa mambo ya elimu na maendeleo, wao huitumia kwa mambo yasiyo na dira wala muelekeo na hiyo ndiyo imemuibua Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP na kutoa somo kwa vijana.

Anakumbusha kuwa mitandao hii ya kijamii kama mawasiliano ni maendeleo na kwamba matumizi ya mitandao siyo mabaya ila watumiaji ndiyo wanafanya vitu vibaya na kuharibu lengo la mitandao hiyo.