Mavazi yasiyo na staha hayajengi taswira yetu

14May 2019
Frank Monyo
Nipashe
Mjadala
Mavazi yasiyo na staha hayajengi taswira yetu

MAVAZI ni moja ya vitambulisho vya taifa lolote lile, jamii, kabila na hata makundi mbalimbali katika jamii.

Na ndiyo maana ya maneno kama vazi la taifa, vazi la michezo, sare za mahitaji mbalimbali na hata kuna baadhi ya watu hujiwekea utambulisho binafsi kupitia mavazi.

Uzuri au ubaya wa kitu, ni tafsiri mbalimbali ambazo zinafanya nafsi ya mtu kujieleza, mara nyingi mavazi katika namna ya kipekee yana nafasi kubwa zaidi ya kuwasilisha ujumbe.

Pamoja na uzuri wa kitu au mambo, unaopatikana kupitia mavazi, katika sura ya pili matumizi mabaya au upotoshaji wa namna yoyote katika matumizi yake, yamezua matatizo makubwa katika jamii, hata kufarakanisha wanafamilia.

Sasa malalamiko yametawala, kiasi cha kwamba hata kwenye nyumba za ibada, ambako kunaheshimiwa kwa namna ya kipekee, matumizi mabaya ya mavazi moja kwa moja huwasilisha ujumbe wa kutoheshimu sehemu hizo.

Kimsingi, tafsiri ya mavazi ya heshima hutegemea imani, mila na desturi ya jamii husika.

Hivyo, mavazi ya heshima ni yale yanayozingatia mila na desturi za jamii katika hatua mbalimbali zilizoko, hadi ngazi ya taifa.

Vazi linaloendana na mahitaji ya jamii na miongozo ya ngazi hizo husika, yana maana kubwa sana.

Mathalani, katika sehemu nyingi staha ya mwanadamu ni kuvaa nguo inayohifadhi baadhi ya sehemu za maungo ya miili yao, ambayo kwa mujibu wa imani na desturi, si mahali pa kuachwa wazi.

Kwa kutumia kigezo hicho hicho, ndiyo inazaa marufuku kwa baadhi ya mavazi, ama yasivaliwe kabisa au hayapaswi kuvaliwa katika baadhi ya mazingira na maeneo mbalimbali, mfano hai ukiwa ni kutoruhusu mavazi ya michezo kuvaliwa na wafanyakazi katika sehemu wanakotumikia.

Tafsiri hiyo inaenda mbali zaidi kwa kina mama kuambiwa mavazi yanayobana, mafupi yanayoacha magoti na sehemu za mwili wazi, hali kadhalika kitovu na kifua.

Mwaka 1971, chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeshika hatamu za uongozi wa nchi wakati huo, kilitoa waraka maalumu wenye mwongozo kuhusu mavazi.

Madhumuni ya waraka huo, yalikuwa kuimarisha heshima ya taifa, kwa mujibu wa imani ya jamii yake, ikilenga kuhakikisha kuwa watumishi katika sehemu za kazi wanadumisha staha ya heshima wawapo kazini.

Tukichukua kinachojiri leo mbele ya umma kuhusu mavazi na kilichoagizwa kwenye waraka huo wa Tanu, tofauti ni ya kutisha.

Mitindo ya mavazi hivi sasa inaporomosha thamani ya jinsia zote mbili katika jamii. Kwa kifupi hali ni tete.

Pengine hali ingekuwa ni mbaya zaidi, lakini tunapaswa kuzishukuru asasi za kidini, sehemu ambako imani ya umma imeshikiliwa.

Kwa watoto wa kike, imekuwa sehemu ya maisha yao kuvaa nguo fupi zinazoonyesha umbile la miili yao.

Kwa tafsiri yao, wanajihisi wanakuwa warembo zaidi na wanakubalika katika jamii yao ya Kitanzania, kwa kukumbatia utashi huo wenye mzizi kwenye utandawazi.

Ni jambo linalowagharimu wengi katika jamii, baadhi wakifukuzwa au kuzuiwa kuingia kwenye ofisi na nyumba za ibada au hata kutokukubalika katika makazi binafsi.

Jumuiya ambayo msingi wake ni mkusanyiko wa watu kwa lengo maalumu ina tafsiri pana, pia huendana na haja ya mtu mmoja mmoja au kikundi kutaka kukubalika nayo.

Inaweza kuwa kwenye kituo cha basi, sokoni, hospitali, nyumba za ibada, shuleni au vyuoni.

Moja ya tiketi muhimu katika kujumuika nayo ni vazi linalokubalika, kama nguo ndefu kwa kinamama ambayo ina kawaida ya kumbandika alama ya kimantiki kuwa mvaaji ni mstaarabu. 

Katika mavazi kuna neno kujisitiri ambalo maana yake ni kuficha kitu mahali ili kisionekane.

Lakini kwa karne ya sasa wanaume kwa wanawake, wamekuwa wakivaa mavazi yasiyo na staha kwenye jamii.

Mjadala una rai kwa jamii ya sasa kujirekebisha kimavazi kwa kuvaa nguo zenye staha, na kujikita kwenye maadili kama jinsi mababu zetu walivyokuwa wakiishi, kwa kufuata mila na desturi za taifa letu.