Mawakala wa dhamana za serikali

26Feb 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Mawakala wa dhamana za serikali

WASOMAJI na wapenzi wa safu hii ya ‘Mtazamo Kibiashara,’ kama ilivyo ada leo tunaendelea tena na somo letu linalohusiana na hati fungani za serikali ama dhamana za serikali ambazo tumeona ziko za aina mbili.

Yaani dhamana za serikali za muda mfupi (Treasury Bills) ambazo huiva kuanzia siku 35, 91, 182 hadi siku 364.
Pia zipo zile dhamana za serikali za muda mrefu (Treasury Bonds) ambazo huiva kuanzia miaka miwili, mitano, saba, 10 na miaka 15.

Lakini wiki iliyopita tuliona vilevile kuwa masoko ya fedha ambako dhamana hizi huuzwa yamegawanyika katika sehemu kuu mbili kwa mtazamo wa soko husika.

Tukasema sehemu ya kwanza ni ya soko la awali (Primary Market) ambako dhamana za serikali huuzwa kwa mara ya kwanza kwa njia ya mnada (Auction).

Aidha, tukaona kuwa mbali na soko hilo la awali, kuna soko la upili (Secondary Market), ambako dhamana za serikali baada ya kununuliwa kutoka kwenye soko la awali, huuzwa na kununuliwa na wawekezaji kabla ya muda wake kuiva.

Haya ndiyo tuliyokuwa tumeyaona mpaka sasa, na nimeona ni muhimu kuyakumbusha hayo kwa wafanyabiashara watakaotaka kushiriki kwenye ununuzi wa dhamana za serikali ili wayakumbuke vizuri.

Na hasa baada ya baashi ya wafanyabiashara na watu wengine wengi kunipigia simu wakitaka wafahamu mengi zaidi kuhusiana na aina hii ya uwekezaji ambayo kimsingi ina faida kubwa.

Sasa soko hilo la dhamana za serikali huendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia kurugenzi yake ya Masoko ya Fedha, ambayo huendesha minada ya dhamana za serikali.

Sasa mfanyabiashara wa ngazi zote, yaani yule mdogo, wa kati ama mkubwa anayo haki ya kushiriki kwenye minada hii inayouza dhamana za serikali kulingana na taratibu zilizopo.

Kimsingi, BoT ina mfumo ambao hufanya mchakato wa minada ya dhamana za serikali na unatunza kumbukumbu za minada hiyo kwa njia ya kielektroniki.

Mfumo huo hujulikana kwa kiingereza kama Central Depository System (CDS).

Lakini sambamba na kuwapo kwa mfumo huo unaofanya mchakato wa minada ya dhamana za serikali, yaani CDS, pia wapo mawakala maalumu.

Maakala hawa wameidhinishwa kushiriki kwenye minada hiyo moja kwa moja kwa niaba yao wenyewe na pia kwa niaba ya wateja wengine.

Mawakala hao maalum, wanajulikana kwa Kiingereza kama (Central Depository Participants).

Sasa mawakala hawa wako kwenye mikoa yote nchini, na kimsingi ndio hasa wanaoweza kufikiwa na wafanyabiashara wa aina zote wanaotaka kununua dhamana za serikali za aina zote.

Yaani zile za muda mfupi na za muda mrefu, kwa kuwa kama nilivyosema hapo juu, hawa wameidhinishwa kushiriki kwenye minada moja kwa moja kwa niaba yao wenyewe na pia kwa niaba ya wateja wengine.

Kwa hiyo mkoa wowote ulipo wewe mfanyabiashara unayetaka kununua dhamana za serikali, unapaswa kuwasiliana na mawakala hao ambao wamesajiliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Aidha taratibu zinataka mfanyabiashara ama mtu mwingine anayetaka kushiriki kwenye minada ya ununuzi wa dhamana za serikali afungue akaunti ya dhamana hizo kwa wakala atakayemchagua kati ya wengi waliosajiliwa walioko katika maeneo ama mikoa yao.

Tukutane Ijumaa ijayo