Mazingira huchafuliwa pia na biashara holela

27Jun 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Mazingira huchafuliwa pia na biashara holela

UKIPATA nafasi ya kuzunguka maeneo ya jiji la Dar es Salaam, bila shaka utashuhudia taka za aina mbalimbali zikiwa zimeachwa kando ya barabara ama zimetupwa hata kwenye mitaro.

Mbali na hilo, utakuta maeneo ambayo yamezibwa kwa kuzungushiwa uzio wa vyuma ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Wapo baadhi ya wafanyabiashara wadogo ambao hupenya na kuendesha biashara zao kama kawaida.

Vitendo hivi vimekuwa vikifanywa na wafanyabiashara hawa, hasa wamachinga wakiwamo wale wanaotembeza biashara zao kandokando ya barabara.

Yaani kwa ujumla ni kwamba, kila mtu hufanya anavyoona inafaa machoni pake bila kujali kwamba anachafua na kufanya uharibifu wa mazingira, pamoja na kuwapo uwezekano wa kuzikusanya sehemu moja, kisha zikachukuliwa kwenda kutupwa jalalani.

Nimeanza kwa maelezo hayo kidogo ili kuzungumzia changamoto zinazotokana na kufanywa kwa biashara kiholela na jinsi ambavyo unachangia katika uchafuzi na uharibifu wa mazingira.

Kama nilivyosema awali, imekuwa ni kawaida kupita mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam na kukuta taka zimezagaa, ikiwa ni pamoja na maboksi ya kuwekea mizigo ya biashara na mengine ya kila aina.

Hayo utayakuta baada ya wafanyabiashara kumaliza shughuli zao, huku taka nyingine zikirushwa kwenye mitaro ya maji ya mvua kana kwamba hawajui umuhimu wa usafi wa mazingira.

Binafsi naamini kwamba, haya yote yanatokana na biashara kiholela, na kama aina hii ya biashara haitapigwa marufuku, itakuwa ni ndoto kukomesha uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika jiji la Dar es Salaam.

Utakuta watu wanafanya biashara hata kwenye maeneo ambayo hayana huduma muhimu, kama vile choo, maji, sehemu ya kukusanyia taka, hali ambayo wakati mwingine huwafanya watupe taka ovyo.

Ukosefu wa huduma wa vyoo huwafanya baadhi yao wajisaidie haja ndogo kwenye mitaro ama katika chupa na kuzitupa ovyo, hali inayochangia kuongezeka zaidi kwa uchafuzi wa mazingira, na ndiyo maana nikasema kuwa, kufanya biashara holela ni kuruhusu uchafuzi wa mazingira.

Ugumu uko wapi wa kuwatengea maeneo rasmi watu hawa ili wafanye biashara zao bila kuchafua mazingira kama ilivyo sasa?

Kama yapo kwa nini hawayatumii?

Kuna hatua gani zilizochukuliwa na mamlaka husika kuhakikisha hali hii inakomeshwa?

Jambo hili halihitaji elimu kwamba waanze kuelimishwa ili wajue umuhimu wa usafi wa mazingira, na kinachotakiwa ni kuamriwa wafanye biashara kwa kufuata taratibu na sheria.

Kwa mfano baadhi ya barabara jijini ikiwamo ya Sam Nujoma imezungushiwa uzio ili kutunza bustani inayogawa barabara hiyo, lakini wafanyabiashara wamekuwa wakipenya kwenye uzio na kuingia ndani kuendelea na biashara, kana kwamba hawajui kuwa ni makosa.

Huu ni uharibifu wa mazingira na hawajali gharama zilizotumika kuweka uzio huo ili mradi tu wafanye biashara zao!

Ninadhani kuna haja ya kuchukua hatua ili kulinda mazingira ya barabara na kujali gharama iliyotumika kuweka uzio.

Sijajua ni kwa nini wanashindwa kuelewa kuwa wanachokifanya ni makosa.

Uzio umewekwa halafu mtu anainama anaingia ndani na kuendelea na biashara kama kawaida!

Maana yake ni kwamba, anajua hakuna njia, lakini analazimisha kuweka njia yake inayomwezesha kuingia katika eneo ambalo haruhusiwi.

Ni vyema hatua zikachukuliwa dhidi ya watu wa aina hii ili wajue kwamba sheria zipo.

Sijajua kwamba wanataka wawekewe uzio wa aina gani ndipo waheshimu, ama wanataka kama ule wa Kimara Mwisho ambao sasa unawalazimisha abiria kutumia daraja la waenda kwa miguu?

Hao nao waliilazimisha serikali kutumia gharama kuweka uzio huo baada ya kukaidi kutumia daraja wakidai kuwa wanachoka wakawa wanalazimisha kuvuka barabara katika mazingira, ambayo ni hatari kwa usalama wao.

Kufanya biashara kiholela kusiwe kigezo cha kutotii taratibu, kanuni na sheria, wafanyabiashara watambue kuwa kama kuna sehemu ambayo hawaruhusiwi kufanyia shughuli zao, basi waachane nayo.

Wakiendelea kuingia kwenye bustani inayotenga barabara ya Sam Nujoma, maana yake ni kwamba gharama zilizotumika kuweka uzio hazina umuhimu wowote, mamlaka husika ziwadhibiti na pia wao wenyewe watambue kuwa wanafanya makosa.

Umefika wakati sasa hatua zichukuliwe kwa ajili ya kuliokoa jiji la Dar es Salaam kutoka katika mazingira machafu kwa kuhakikisha hakuna biashara holela kama ilivyo sasa.