Mazingira ya usafi biashara  ya mamalishe ni muhimu

05Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Mazingira ya usafi biashara  ya mamalishe ni muhimu

KWA kawaida msingi wa maisha ya afya ya binadamu ni usafi wake wa mwili na mazingira, hivyo usafi ni dhana shirikishi ikijumuisha kuanzia mtu mmoja mmoja, familia na hata kwingineko.

Hivyo mmoja wetu akishiriki kikamilifu kwa nafasi yake katika usafi wa mazingira itakuwa ni rahisi kumuondoa adui maradhi ambaye alitangaziwa vita mara tu baada ya nchi hii kupata uhuru mwaka 1961.

Kwa mfano ugonjwa wa kipindupindu ni tatizo kubwa la kiafya kwa nchi zinazoendelea, ambako milipuko yake hutokea kufuatana na misimu ya hali ya hewa na kuhusishwa na suala la umaskini na usafi duni. 

Ninajikita katika suala hili muhimu kwa lengo la kutaka kujadili kidogo kuhusu biashara ya mamalishe na babalishe ambayo baadhi yao wamekuwa wakiifanya bila kuzingatia usafi wa mazingira, na hivyo kuhatarisha afya zao za wateja wao.

Kimsingi ni kwamba ili kufanikiwa katika biashara yoyote ile ni lazima mtu awe mbunifu, lakini pamoja na ubunifu huo kuna mambo mengine ya kuzingatia na hasa kuuza chakula katika mazingira safi.

Ninaamini kwamba hakuna mtu mwenye akili timamu anayependa kula uchafu, hivyo ni muhimu wahusika kuandaa chakula katika mazingira safi ambayo yatamsaidia kufanya chakula chake kivutie wateja.

Katika biashara hii yapo mambo mengi ambayo wahusika wanapaswa kuzingatia, lakini jambo kubwa likiwa ni usafi kwa lengo la kuepuka magonjwa ya mlipuko na hasa kipindupindu ambacho kimekuwa kikiibuka mara kwa mara.

Kwa kawaida maeneo ya kufanyia biashara za mamalishe na babalishe yanatakiwa kuwa yale ambayo yamekaguliwa na kuruhusiwa na mamlaka husika, lakini bahati mbaya baadhi ya wanaofanya biashara hii huwazingatii hilo.

Wakati mwingine inaonekana kama ni jambo la kawaida kukuta mamalishe au babalishe anaandaa chakula katika mazingira ambayo si salama kwa afya yake na ya wateja, lakini wala hashtuki.

Umefika wakati sasa wahusika waendelee kupewa elimu ya kutosha kuhusu afya, ili kuwaepusha wateja wao kukumbwa na maambukizi ya magonjwa ya milipuko yanayotokana na uchafu.

Ikumbukwe kuwa kila kukicha mamalishe na babalishe wapya wamekuwa wakiongezeka, ndiyo maana nikasema kuwa elimu ya usafi iendelee kutolewa ili wajue jinsi ya kuzingatia usafi katika mazingira wanayofanyia biashara.

Kwa maana hiyo mapambano dhidi ya uchafu yanahitaji uelewa mkubwa na wa jumla na pia kanuni za usafi ni muhimu zifahamike kwa wote.Vilevile madhara ya uchafu na faida za usafi navyo vinatakiwa kufahamika.

Niseme tu kwamba kipindupindu hakiwezi kumalizika nchini iwapo kila mmoja wetu atashindwa kuzingatia usafi unaotakiwa.

Nimegusia zaidi mamalishe na babalishe kwa kutambua kuwa wao ndio wanaohudumia wateja wengi kutokana na mzunguko mkubwa wa watu, ambao husababisha baadhi yao kulazimika kujipatia chakula cha mchana au usiku kutoka katika makundi haya.

Hivyo ni vyema wakawa makini kwa kuzingatia ubora wa mazingira ya kuandalia vyakula.

Wafanye hivyo huku wakitambua kuwa usafi wa mazingira ni njia ya kuendeleza afya kwa kuzuia mawasiliano ya binadamu na athari za taka ambazo zinasababisha maradhi mwilini.

Ninadhani ipo haja pia mamalishe na babalishe wakatengewa maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao yakiwa na huduma zote za msingi badala ya kuwaacha kila mmoja akiibuka na kuuza chakula hata kwenye mazingira hatari kwao na kwa wateja wao.

Nakumbuka Juni mwaka huu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na WHO iligawa aproni 257 zenye thamani ya Sh. 2,929,800 kwa mamalishe na babalishe wa soko la Buguruni na Stereo ili kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

Awali Ofisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dennis Kamuzora akawaambia wahusika kuzingatia usafi katika maeneo yao ya biashara vinginevyo watakumbwa na kipindupindu ambacho kitasababisha vifo na hata biashara zao kufungwa.

Pamoja na kupewa hizo aproni, msisitizo mkubwa ulikuwa ni kwenye usafi wa mazingira, kwani walikumbushwa kuweka vyakula katika mazingira safi na salama. kwa vile inaeleweka kuwa baadhi yao wamekuwa hawazingatii hilo.