Mbadala wa elimu ya Uzazi ni nini?

12Apr 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Mbadala wa elimu ya Uzazi ni nini?

Nimekuwa nikisoma maoni mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwepo au kutokuwepo kwa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi na vijana wa chini ya umri wa miaka kumi na nane.

Hoja ya wanaopinga kutolewa kwa elimu hii ni kuwa, itawaharibu watoto wetu zaidi kwa sababu itawafundisha mambo mabaya kuhusiana na matendo ya ndoa.

Nadhani kupunguza maudhui ya elimu ya afya ya uzazi hadi kudhani kuwa somo litahusu ngono tu ni udhaifu wa hoja yenyewe na kuonyesha kuwa hatufahamu elimu ya afya ya uzazi maana yake nini.Pia kuonyesha kuwa hatujui kwa undani mazingira ya sasa wanayoishi vijana wetu.

Naanza na hili la mwisho kuwa, wazaz hasa wale wa umri wangu na kuendelea wakumbuke kuwa, nyakati hizi ni za uhuru mpana wa kupata habari.

Wakati ule zaidi ya wazazi kulikuwa na viongozi wa dini wanaoweza utoa taarifa za ziada kuhusu maisha na hasa mahusiano ya mapenzi kwa msingi wa dini. Na shuleni, kulikuwa na walimu waliokuwa wakitoa elimu ya mfumo wa uzazi, na kwa makabila mengine unyagona jando.

Elimu ile ilikuwa imedhibitiwa kikwelikweli kiasi kwamba, haikuwa rahisi mwanafunzi kujua mengi zaidi ya kile alichojifundisha.

Lakini ngono na maumbile yake vilikuwa vitu vilivyojenga udadisi mkubwa miongoni mwetu kiasi kuwa tuliendelea na mjadala nje ya madarasa. Lakini tulikuwa na vyanzo finyu vya taarifa.

Lakini siku hizi, watoto na vijana wamepanuliwa wigo wao wa taarifa kwa kuwa na vifaa vya mawasiliano vyenye kujenga demokrasia ya kupata habari bila kudhibitiwa na wazazi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Wakiwa shuleni au barabarani au katika maeneo ya burudani watoto wanaweza kutumia kompyuta, simu za kiganjani au tabs na kufungua taarifa za mapenzi na ngono na kuona filamu zinazoonyesha tendo la ngono na hakuna anayeweza kumzuia.

Ni jambo la kawaida sana sasa… inaweza kuwa mwanao hujamnunulia simu ya mkononi ya namna hiyo, lakini jirani yake anayo, au shuleni kuna mwanafunzi mwenzao anayo hivyo wanakaa kuangalia. na wanapoangalia kwa mtindo huu si rahisi kumdhibiti mtoto kwani sasa wanafundishana wenyewe kwa wenyewe, na sasa huwezi jua nini wanafundishana.

Mzazi utakuwa hutaki mwanao afundishwe shuleni, na shuleni hakuna mtaala wa hivyo, lakini mtoto anapata maarifa kupitia kwa mtoto mwenzake na wengi watashauriana kuwa ni heri wajaribu wanachokiona. Aidha wazazi watambue kuwa mfumo wa maadili- value system, hubadilika.

Kile ambacho wazazi waliona ni haramu na sumu miaka yao ya ujana, haiangaliwi kwa jicho la namna hiyo tena katika nyakati hizi- zamani bikra ilikuwa kigezo cha uanamke.

Lakini siku hizi sio kigezo tena.Na msichana au mvulana anajiriwa mbali na wazazi wake, anakaa mbali na wazazi tangu akiwa shule, chini ya usimamizi wa mfumo mwingine wa maadili na kujihusisha na tendo la ndoa sio jambo geni
Mjini kila mtu na lake. Na kuishi msichana na mvulana chumba kimoja kabla ya ndoa sio jambo geni tena…

Kwa sababu hiyo, unaweza kuona kuwa kuna umuhimu wa kuwa na elimu ya afya ya uzazi, kwa sababu ya kuwaonyesha watoto usahihi wa mahusiano, wakati bora na kujua tafsiri sahihi ya kile wanachoona kwenye vyombo vya habari.

Ni muhimu sababu wasichana na wavulana watafundishwa hasara za kujihusisha kabla ya umri fulani na kabla ya ndoa(ikitegemea aina ya dini); kwa kipindi hichi cha kansa, na maradhi mengine ni vizuri wasichana wakaenda kupima kujua kama wana maambukizi ya maradhi au hapana na kufundishwa namna bora ya kujilinda nayo wasiambukizwe.

Elimu ya uzazi itamwonyesha mtoto anachoweza kufanya kabla ya ndoa na baada ya ndoa. Na anaweza kupata hasara gani akijihusisha na tendo la ndoa mapema akiwa mtoto.

Mtoto anapaswa kujifunza mapema maana ya maisha na namna wazazi, walezi na shule watakavyoweza kumsaidia kuweka malengo ya maana katika maisha yake.

Mtoto akisha jua kuwa, akikua atawajibika kujilinda na kuacha utegemezi, atajifunza pia kuishi kwa kujihami na kujilinda dhidi ya matendo, makundi na vishawishi vitakavyomuingiza kwenye mfereji wa kuelekea kwenye kufeli kimaisha.

Elimu ya uzazi itasaidia mwanafunzi kujua kuwa bila elimu yake, kuwa na kazi inayoeleweka, na bila kuachana na tabia mbaya, atabaki kuwa maskini kwani kupata mimba, au maradhi ya ngono, ni kuharibu mwelekeo wa maisha yake na ya kizazi chake.

Kwa ujumla naweza kusema kuwa ikiwa na maudhui mazuri na ya kuzingatia hali halisi ya sasa hivi, elimu ya afya ya uzazi itamfundisha mtoto namna ya kujilinda, na kuweza kutambua kuwa, bila yeye mwenyewe kujilinda hakuna atakayemlinda na kuwa mwangalifu katika kile anachokiona au kusikia kutoka kwa vijana wenzake…!