Mbao ilivyosahau kuwa biashara huwa ni asubuhi

03Aug 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mbao ilivyosahau kuwa biashara huwa ni asubuhi

KIPENGA cha mwisho kilipopulizwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jumamosi iliyopita, wachezaji wote wa Mbao FC walianguka chini, wengine wakiangua kilio kwa uchungu.

Ni baada ya dakika 90 za machozi jasho na damu, ilipocheza dhidi ya Ihefu FC kutoka Mbarali mkoani Mbeya. Pamoja na ushindi mnono wa mabao 4-2, Mbao FC ilijikuta ikishuka daraja. Hii imetokana na mechi ya kwanza iliyocheza ugenini kukubali kipigo cha mabao 2-0. Ukichanganya na matokeo hayo ni kwamba Mbao na Ihefu zilikuwa zimefungana 4-4, hivyo Ihefu imetinga Ligi Kuu kwa kanuni ya bao la ugenini.

Ilikuwa ni mechi kali ya mchujo kutafuta timu itayokwenda Ligi Kuu, kati ya timu ya Ligi Kuu Mbao FC na timu ya Daraja la Kwanza, Ihefu FC.

Hakika ilikuwa ni siku mbaya si kwa wachezaji na viongozi wa Mbao FC tu, bali ni kwa mashabiki wa soka wa Mwanza, ambao siku si nyingi zilizopita waliipoteza timu ya Alliance FC ambayo yenyewe ilishuka moja kwa moja licha ya kuichapa Namungo FC mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Ilikuwa ni kama marudio tu, kwani Mbao nayo ikiwa nyumbani, licha ya ushindi wa mabao 4-2 nayo ikashuka. Kwanza nikayakumbuka maneno ya straika hatari wa Mbao FC, Waziri Junior, ambaye kwenye Ligi Kuu alifunga ma mabao 13 na katika mechi hiyo ikifunga mawili.

Baada ya mechi ya kwanza huko Mbarali, aliwaonya Ihefu FC kuwa wasitarajie kuwa watapata mteremko au itakuwa rahisi kwao kupanda Ligi Kuu, kwani watakutana na wakati mgumu wakiwa CCM Kirumba na itakuwa ni mechi ngumu kwao kuliko yeyote ile waliowahi kucheza msimu huu.

"Tunakubali tumefungwa, lakini ukiangalia uwanja haukuwa rafiki kwetu, una mabonde mengi tu, kwa hiyo ilikuwa inatupa tabu sana, lakini nawaambia Ihefu hivi, wao wameshinda kwao na sisi tunawakaribisha kwetu CCM Kirumba, haitokuwa mechi rahisi kwao," alisema Waziri.

Na kweli ilikuwa hivyo. Waziri Junior mwenyewe aliwapa tabu sana mabeki wa Ihefu na kufunga mabao mawili. Lakini wachezaji wa Mbao FC walikuwa wakicheza kana kwamba ni fainali ya Kombe la Dunia. Ikanishangaza sana, ni kwa nini Mbao FC kwa sasa imekuwa ikicheza vizuri na wachezaji wake kujituma kwenye mechi za mwisho, hasa hizi za kuamua matokeo.

Nikajiuliza hivi kweli Mbao FC ingeanza kucheza hivi tangu Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza, si ingekuwa inawania nafasi ya pili au ya tatu?

Nikamkumbuka Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda ambaye katika tathmini yake baada ya Ligi Kuu kumalizika, aliziambia timu zingine za ligi kuwa zisizubiri hadi kwenye mechi za mwisho za ligi ili zikaze msuli, badala yake zianze tangu mwanzo kama wao, Coastal Union walivyofanya, ndiyo maana hata mechi za mwisho pamoja na kutofanya vizuri sana, lakini ilikuwa salama.

"Tumejifunza kuwa tukianza kushindana basi anza mwanzo, usisubiri mwisho. Unaona sisi tulianza kupambana mwanzo hatukupata matatizo mwishoni mwa ligi, lakini angalia timu zilizokuwa zikiona kama ligi bado, zilivyopata shida mwishoni," alisema Mgunda.
Hiki ndicho kilichoikuta Alliance FC, Ndanda FC na Lipuli, lakini mwisho wake ikaja kuikuta Mbao FC.

Mfano Mbao FC ilicheza mechi saba za Ligi Kuu, ikashinda sita na kutoka sare moja, ilichowasaidia ni kutoshuka moja kwa moja tu, badala yake ikawa kucheza mechi ya mchujo.

Unajiuliza kama Mbao FC ingeshinda mechi hizo mwanzoni mwa ligi, halafu wachezaji wa timu hiyo wangekuwa wanacheza kwa kujituma kama hizi mechi za hivi karibuni, sidhani kama ingefikiriwa hata kucheza mechi ya mchujo, achilia mbali kushuka.

Kilichotokea CCM Kirumba ni somo kwa timu zingine zilizopo Ligi Kuu na zilizopanda kupambana kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa ligi na si kusubiri mechi za mwisho. Waswahili wanasema biashara asubuhi, jioni mahesabu. Lakini Mbao kwao jioni ndiyo walikuwa wanaanza biashara.