Mbinu hizi mbili muhimu kukabili janga la saratani

24Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mbinu hizi mbili muhimu kukabili janga la saratani

CHANZO kikubwa cha watu kukumbwa na saratani mbalimbali zikiwamo za koo, ngozi na nyingine nyingi, ikiwamo mlo: Kimsingi, ulaji kwa kanuni duni una hatari kubwa.

Inaelezwa kuwa ni muhimu watu kufuata kanuni bora za lishe, ili kuepuka kukumbwa na ugonjwa huo hatari na pia kuwa tayari kufuatilia ushauri unaotolewa na watalaamu wa afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaselage, anasema saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa wagonjwa wengi, huku jijini Dar es Salaam, saratani ya matiti ndio kinara,

Nyingine zinazotajwa kuwasumbua Watanzania ni saratani za koo, ngozi, matezi, damu, kibofu cha mkojo na tezi dume, ambazo cha muhimu kinachohimizwa juu yake ni umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Hadi sasa imeshawekwa wazi kuwa utoaji huduma za matibabu ya ugonjwa wa saratani upo katika hospitali zote nchini, lengo ni kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na wataalamu wengine wa saratani.

Hapo kuna mawili muhimu yanayopaswa kuzingatiwa, ili kukabiliana na ugonjwa huo. Kuna sulala la lishe bora, kwenda hospitalini na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Ni bahati mbaya, baadhi ya watu huwa wazito kuzingatia lishe bora inayohusisha ulaji mboga za majani ambazo wengi wanazipuuza, wakiangukia mbadala kama chipsi vingine vinavyofanana navyo.

Inaelezwa kuwa vyakula ambavyo baadhi ya watu wanavidharau, ndivyo vinavyofaa kwenye afya. Hivyo, kuna haja ya kubadilika kwa kuacha kula kwa mazoea na kuhamia kwenye miongozo ya lishe bora.

Wavutaji wa sigara ndiyo wanaoelezwa kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa na wapo baadhi yao, kwa kawaida ni wazito kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa mwaka uliopita, kuna wagonjwa wapya saratani duniani milioni 18.1 na kuna wagonjwa milioni 9.6 waliopoteza maisha.

Pia, kunatajwa asilimia 70 (sawa na watu milioni 6.7) ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo wanatoka nchi maskini.
WHO inaelezea umuhimu wa kuongezwa huduma za kukabiliana na saratani katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani.

Wakati kukiwa na juhudi hizo, siyo vibaya jamii pia ikajiongeza kwa kuzingatia maelekezo ya watalaamu wa afya, kuanzia ulaji unaotakiwa na hospitalini, kwa ajili ya ushauri na matibabu pale inapobidi.

Njia hizo mbili ni muhimu katika kukabiliana ugonjwa huo, ili kupunguza tatizo hilo, kama siyo kulimaliza kabisa ndani ya jamii, kwa vile linatajwa kuwa watu wa jinsia zote nchini wanaathirika.

Hatua hizo zikichukuliwa, zitasaidia kukabiliana na tatizo hilo, kwani WHO inatahadharisha kwamba bila ya hatua kuchukuliwa, duniani kutashuhudiwa ongezeko kubwa la asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani katika miongo miwili ijayo.

Kwani shirika hilo la afya, lina ufafanuzi wake kwamba Takriban ongezeko kubwa kwa kiwango 81 vitatokea katika nchi zenye kipato cha chini, ambako uhalisia ngazi ya kumudu maisha ya kila siku iko chini mno.

Ni ukweli kwamba, iwapo watu wote watazingatia maelekezo ya lishe na kwenda kupata huduma za msingi, kitabibu, saratani inaweza kugundulika mapema, kutibiwa vizuri na wagonjwa wake kupona.

Wataalamu wa afya wameshaweka wazi kuwa ugonjwa huo haupaswi kuwa katika sura ya adhabu ya kifo kwa kila anayepatwa, bali kama ni bahati mbaya ataugua, bado awe na nafasi ya kuhudumiwa baada ya kugundunliwa mapema afike hatua ya kupona.

Hivyo, kushugulikia saratani kwa kuzingatia lishe bora ni jambo muhimu na kwenda kwenye vituo vya afya mapema kupata ushauri wa kitaalamu au matibabu ina ulazima.