Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

22Sep 2018
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

‘MATAO’ ni mbwembwe na machachari. Maana yake mtu anayecheza ngoma hawi kilema kwa kuwa uchezaji ngoma una machachari mengi. Hapana shaka mchezo wa kandanda huwa na machachari mengi zaidi ya ngoma.

 Hii ni nasaha kwamba tuazimiapo kufanya jambo fulani (kwa muktadha huu kandanda), lazima tujitolee na kufanya juhudi kubwa. Hatupaswi kuwa na ulegevu au ajizi.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ndio kwanza imeanza huku timu zinazoitwa ‘kubwa’ zikionjeshwa chungu ya kandanda. Kwamba mchezo huo unaopendwa sana duniani, hauchezwi kwa maneno na vitisho, bali huchezwa kwa miguu, kichwa na kufuata kanuni zake na mafunzo ya walimu.

Kabla na baada ya ligi kuanza, kulikuwa na maneno mengi mno ya vitisho kwa kila timu (hasa Azam, Simba na Yanga) kuwa timu zitakazokumbana nazo zijiweke tayari kufungwa.

Maneno hayo yalisemwa na yangali yasemwa bila kutambua kuwa ‘mashindano’ ni matendo ya kupimana uwezo yaani makabiliano yenye lengo la kuwania jambo baina ya pande mbili au zaidi.

Azam, Simba na Yanga huvishwa vilemba vya ukoka na waandishi wetu wa magazeti ya michezo. Pengine hufanya hivyo ili kuuza magazeti yao lakini kwa upande mwingine ni kuzipotosha kuwa hakuna timu za kuzishinda, kumbe sivyo.

“Aussems amaliza kazi mapemaaaaa” ni kichwa cha habari cha moja ya magazeti ya michezo nchini kikifuatiwa na maelezo yafuatayo kabla ya mechi ya Simba na Mbao jijini Mwanza:

“Hakuna namna. Lazima Simba leo ishinde ili kutuliza hali ya mambo kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo kuchukizwa na suluhu ya mjini Mtwara dhidi ya Ndanda na Kocha Patrick Aussems ametamba kitaeleweka (kitendo cha kuweza kufahamika bila matatizo) tu leo jijini Mwanza.”

Gazeti lingine la michezo likaandika: “Licha ya  kwamba hawakuambatana na kocha wao msaidizi, Masoud Djuma aliyebaki Dar es Salaam kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kazi maalumu, Wekundu hao wa Msimbazi wamesema wataibuka na ushindi mnono.”

“Ushindi mnono” uligeuka kuwa machungu kwa Simba ilipofungwa bao 1-0 na kuwapa mashabiki wa wapinzani wao, (Yanga) nafasi ya kutoa maneno mengi ya kuwabeza bila kujua pia kuwa nao wamo kwenye msitari huohuo.

Nawakumbusha wenzangu kuwa: “Leo kwako kesho kwa mwenzio.) Jambo linalokupata leo liwe la shida au la raha huweza kumpata mwenzio kesho.

Nakumbuka walivyosema wahenga kuwa “Kinywa ni jumba la maneno.” Kinywa cha binadamu ni kama jumba la maneno. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kuwa binadamu ana uwezo wa kusema maneno yoyote yawe mazuri au mabaya. Kwa hiyo tusishangae tusikiapo fulani kasema maneno fulani.

Methali hii hutumiwa kumnasihi mtu aliyeazimia kufanya jambo asikate tamaa au asivunjwe na maneno ya watu ambayo hayamdhuru kwa namna yoyote. Huweza pia kutumiwa na mtu aliyeazimia kufanya jambo fulani kujitetea dhidi ya maneno ya binadamu.

Nakumbuka kuandika kwa msisitizo kuwa hakuna timu inayoingia uwanjani kwa lengo la kushindwa bali lengo na nia ni kushinda.

 Katika timu zote zilizo Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hakuna inayoitwa ‘kubwa’ ambayo haijaonja kipigo au kunusurika kwa suluhu au sare. Yanga wakumbuke kuwa timu yao bado iko nyumbani, haijatoka nje ya Dar es Salaam. Kwa hiyo si ajabu yaliyowapata wenzao huko nje pia yakawakuta wao. Ikiwa hivyo watakuwa wageni wa nani?

“Halahala mti na macho.” Maana yake jitunze au angalia usijitie kijiti machoni. Vilevile ieleweke kuwa “Hakuna mume wa waume.” Hakuna mtu mmoja anayeweza kuwashinda wanaume wenzake wote. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayejitia ubabe au anayejidai kuwa na nguvu kama njia ya kumnyamazisha.

Methali ifuatayo yazifaa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania bara:

“Usishindwe na kupika ukasingizia jiko lina moshi.” Maana yake usishindwe na kupika kisha ukaanza kulilaumu jiko kwa kusema lina moshuweza kutumiwa kupigia mfano wa mtu anayeshindwa kulifanya jambo kisha akaanza kutafuta kisingizio.

[email protected]