Mchimba Kisima huingia mwenyewe

13Nov 2021
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mchimba Kisima huingia mwenyewe

MTU anayemchimbia mwengine shimo kwa dhamira mbaya huishia kuingia yeye mwenyewe!

Methali hii huweza kutumiwa kumshauri mtu anayekusudia kumfanyia ubaya mwenzake huenda ubaya huo ukamrudia yeye.

Nchi ni eneo la ardhi lenye utawala wake dola, yaani utawala wa nchi. Bendera ni kitambaa mahususi chenye rangi na alama maalumu ikiwa ni kitambulisho cha mamlaka fulani kama vile nchi au chama.

Ndio maana kila nchi duniani ina bendera ya aina tofauti zenye maana tofauti na za nchi zingine.

Bendera ya Tanzania ina rangi nne tofauti : Rangi ya bluu ina maana ya bahari kumaanisha Tanzania inapakana na Bahari ya Hindi. Rangi nyembamba ya njano maana yake ni madini yaliyo nchini mwetu ilhali rangi nyeusi inawatambulisha wananchi wa Tanzania kisha rangi ya kijani yaonyesha hali ya nchi ilivyo.

Hii yanikumbusha walivyosema wahenga kuwa: “Kila mlango una wimbile.” Kwa kawaida kila mlango wa bahari una wimbi lake. Ni methali ya kutumiwa kutukumbusha kila kitu kina sifa zake tofauti hamna kinachofanana na kingine. Hatuwezi kufananisha hali tofauti.

Hukereka (sumbuliwa na jambo; chukizwa) sana nionapo timu zetu za taifa zinapopambana na timu ngeni zinapokuja nchini, wanaohudhuria kuwashangilia wachezaji wetu huwa wachache sana.

Kinachoshangaza ni kwamba Yanga na Simba zinapopambana kwenye uwanja wowote humu nchini baadhi ya mashabiki na wanachama wao huenda mkoa wowote ili kuzishangilia. Wengine hutumia baiskeli kwa mwendo unaowachukua siku kadhaa!

Ina maana Yanga na Simba ni bora kuliko timu za Taifa ambazo nazo huwa na mchanganyiko wa wachezaji wa timu nilizotaja hapo juu? Kama Yanga , Simba na Taifa Stars ni timu za nchi moja iitwayo Tanzania kwa nini twazithamini Yanga na Simba za mkoa mmoja tu kati ya mikoa takribani (kwa kukisia) 31?

Neno “Ujahili” lina maana ya ukatili; unyama; uonevu; upumbavu na ujinga. Kumbe baadhi yetu ndivyo tulivyo!

Timu ngeni zinapokuja kucheza kwetu na kuona jinsi tunavyozishangilia ilhali Simba na Yanga ni zetu hutucheka kimoyomoyo na kuwaongezea nguvu za kucheza dhidi ya timu zetu. Pukachaka! (neno lenye kuashiria kutema mate ambalo humaanisha kukidharau kitu kilichotajwa.)

Kwa nini Simba na Yanga zinawekeana chuki yaani hali ya kutokuwepo upendo, hali ya kuwa na roho mbaya hali ya kuwa na kinyongo ilhali zote ni timu za mkoa wa nchi moja?

Kufarikiana (kitendo cha watu kutengana kutokana na kutoelewana) isiwe sababu ya kuwekeana chuki na kushangilia mojawapo zinaposhindwa na timu ngeni kutoka nnje ya Tanzania!

Tunapaswa kutambua “wajinga ndio waliwao.” Kwamba ndio wanaopumbazwa au kuliwa. Methali hii huweza kutumiwa kumpigia mfano mtu ambaye ameishia kudanganywa kwa njia inayoonekana kuwa rahisi sana.

Simba na Yanga zapaswa kusoma kwa makini methali hii: “Ulimwengu ni dhaifu siuoneni sheshe” (kivumishi chenye maana ya kizuri kama vile ‘nguo sheshe’ ni nguo nzuri.)

Maana yake dunia au ulimwengu ni kitu dhaifu tusivutwe na sura yake ya uzuri. Methali hii hutumiwa kumtaadharisha mtu anayejisifu na kujigamba kutokana na uwezo au nguvu alizonazo ajue kwamba ulimwengu unaweza kumwangamiza.

“Chako ni chako, cha mwenzako si chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nancho kuliko cha mtu mwingine.

Tunafunzwa tuvitegemee vitu vyetu wala sio vya watu wengine. Pia tunakumbushwa kuvithamini vitu vyetu ingawa sio vizuri kama vya wengine.

[email protected]
0784 334 096