Mengi, mbele yetu nyuma yako

04May 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mengi, mbele yetu nyuma yako

NI vigumu kukumbuka mambo mengi aliyofanya Dk. Reginald Mengi wakati wa uhai wake. Kwa hakika ni mengi kama lilivyo jina lake.

Kama kumbukumbu zangu ni sahihi, nilianza kufahamiana na Dk. Mengi mwanzoni mwa miaka ya 80 wakati ule nikiwa Mhariri wa Habari wa gazeti la Kiongozi linalochapishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Wakati ule pia nilikuwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Waandishi wa habari nchini.

    Tulikutana na Dk.Reginald Mengi mara kwa mara kila viongozi wa chama cha waandishi wa habari tulipokutana. Nakumbuka wakati fulani tukiwa tunakula chakula cha mchana alichotuandalia kwenye hoteli maarufu ya jijini Dar es Salaam alituuliza kama tumesikia tetesi kuwa ameombwa awe na hisa katika gazeti la Kiingereza liitwalo Business Times.

    Wakati tukiendelea kumsikiliza, akasema kamwe hawezi kuchukua hisa kwenye vyombo vya habari, hasa magazeti. “Ukitaka kugombana na serikali, basi kuwa mmiliki wa gazeti… utakuwa na mivutano ya mara kwa mara na serikali,” alisema Mengi. Wakati ule alikuwa na biashara yake ya kalamu pembezoni mwa barabara ya Pugu Road ambayo sasa yaitwa Barabara ya Nyerere.

    Yaelekea Mengi hakukatishwa tamaa na jambo lolote hasa lililohusu maendeleo yake na ya wengine. Alianzisha kituo cha televisheni (runinga) cha ITV kisha magazeti ya kila siku ya Nipashe (Kiswahili) na The Guardian (Kiingereza) na baadaye magazeti ya mchana na ya kila wiki ambayo aliyasimamisha baadaye.

Nilipostaafu kuwa Mhariri wa gazeti la Mwanachi lililomilikiwa na mhindi ambaye sasa anaishi Canada, Dk. Mengi aliniita kusaidia kazi katika gazeti lake la Nipashe. Nilifanya pale kwa muda wa takriban miaka miwili alipotaka kununua jina la Mwananchi ambalo wakati ule lilikwisha simamishwa. Alinituma nimwombe aliyekuwa mmiliki wa gazeti hilo ili anunue jina na alikubaliwa ingawa hakufanya hivyo.

    Baada ya hapo alikuwa na mpango wa kuanzisha gazeti ambalo lingesomeka Kenya, Uganda na Tanzania kama gazeti la nchi moja. Ingawa ilifanyika mipango mingi, mwishowe niliondoka na mpango wa kufungua gazeti hilo ukaishia hewani. Mengi alikuwa mtu mwenye kuona mbele katika biashara zake. Alipoona biashara fulani inampotezea muda na kumwingizia hasara, aliiacha mara.

Hakuishia hapo kwenye biashara kwani alikuwa na kiwanda cha kutengenezea chupa za chai lakini akaachana nayo baada ya kutapeliwa kwa kuletewa vifaa bandia vya kutengenezea chupa za chai pale kilipo kiwanda cha Coca Cola jijini Dar es Salaam sasa.

Mengi pia alikuwa na kiwanda cha sabuni za Revola, dawa ya meno (Colgate) na karatasi za chooni. Aliachana na biashara zote alipoona hazimletei faida. Akajikita zaidi katika vyombo vya habari mpaka alipofikwa na mauti kule Dubai.

Kwa jumla ni mtu aliyejali zaidi maendeleo ya jamii na kuwapenda sana walemavu na kuwapa mikopo ya kufungua biashara mbalimbali. Tangu hapo alikuwa na tabia ya kuwaandalia chakula cha mchana kila mwaka na kujadiliana nao kuhusu jinsi ya kupambana na matatizo wanayokumbana nayo.

Nadhani wanamichezo wengi wameguswa na kusikitishwa na kifo cha Dk. Mengi kwani alikuwa mpenzi mkubwa wa michezo akionyesha wazi kuguswa zaidi na klabu ya Yanga. Kuna wakati alimweka mtaalamu wake mkuu wa uchumi kwenye klabu ya Yanga akitaka kuifanya Yanga iongozwe kisasa lakini kwa uroho wa baadhi ya viongozi hawakupenda mpango wake wakijua kama ungekubalika, basi wangekosa fursa ya kula hela za klabu.

Alipoona jitihada zake za kutaka kuifanya Yanga kuwa klabu inayojitegemea yenyewe zinapigwa vita na wasiopenda maendeleo, akaamua kujiweka kando. Bado alikuwa msaidizi mkubwa wa fedha kwa klabu za kandanda kama Taifa Stars, Serengeti Boys bila kuisahau Yanga. Nadhani Yanga watakuwa wakilia chini chini kwani hivi karibuni walipokosa nauli ya kuwapeleka kwenye mchezo fulani, walienda kumwomba Mengi aliyewawezesha kuendelea na safari yao.

Yanga ingekuwaje leo kama wanachama wangekubaliana na mpango wa Mengi wa kuifanya ijitegemee yenyewe badala ya kuwategemea watu binafsi na kuwa ombaomba? 

Mengi alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha kampeni ya kupanda miti mkoani Kilimanjaro na kweli miti iliyoonekana kupotea sehemu nyingi za mkoa huo ilirejeshwa kwa juhudi za Mengi aliyetoa zawadi kwa watu waliofanikiwa kupanda miti mingi.

Kwa bidii zake, Mengi alikuwa mwafrika wa kwanza kuanzisha biashara ya maji ya chupa yaitwayo Kilimanjaro yanayouzwa ndani na nje ya Tanzania kupitia kampuni ya Bonite iliyo katika kundi la makampuni ya IPP.

Pamoja na juhudi hizo, pia alikwisha tia saini ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza gesi itakayotumiwa na magari badala ya petroli kule Rwanda. Pia ameacha ujenzi wa viwanda vya madawa humu nchini akishirikiana na wawekezaji wa nnje.

Tangulia Mengi tuko nyuma yako. Pumzika kwa amani.

[email protected]

0784  334 096