Meza ya majadiliano tiba ustawi ‘bustani’ demokrasia

25Nov 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Meza ya majadiliano tiba ustawi ‘bustani’ demokrasia

TANGU kumalizika kwa uchaguzi mkuu, baadhi ya vyama vya siasa vya   upinzani vimetoa matamko mbalimbali yakiwamo kuunga mkono uchaguzi huo kwamba ulikuwa huru na wa haki.

Vingine vimegoma kuutambua vikidai haukuwa huru na haki, hivyo havioni sababu ya kushirikiana na serikali, badala yake vinajiweka pembeni na kuiachia CCM.

Hata hivyo, Chama cha NCCR Mageuzi, chenyewe kinajipambanua kuwa kinaweka mbele  zaidi maslahi ya taifa kwa kujali mazungumzo ya pamoja ili kuja na muafaka kuhusu uchaguzi huo.

NCCR-Mageuzi inaamini kwamba ingawa yapo madai ya 'figisufigisu' kwenye uchaguzi huo, lakini njia pekee kwa wanasiasa ni kuwekana sawa na kuwapo kwa meza ya mazungumzo, kwa ajili ya muafaka wa kitaifa.

Hivi karibuni mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, anatoa  rai hiyo mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam, kuwa, asili ya kutatua matatizo huanzia kwenye mazungumzo na kuishia katika makubaliano ya kindugu.

Mbatia anaamini kuwa, kwa miaka 59 ya uhuru, Watanzania hawajatumia vizuri Tanzania ili wajipatie mahitaji ya msingi kwa wote na kuwa na furaha ya kweli.

Lakini, chama hicho kinakiri kwamba ni miongoni mwa vyama ambavyo kwa miaka 28 vinaimba wimbo wa kupata katiba mpya ya kubeba tume huru ya uchaguzi, na kwamba gharama zimekuwa kubwa kwa chama hicho.

Kinachoshauriwa na NCCR- Mageuzi ni sahihi, kutokana na ukweli kwamba, hata nchi zilizoendelea zinatumia njia hiyo kumaliza tofauti za kisiasa kwa manufaa ya kila mmoja.

Ni muhimu wanasiasa kutetea ama kuweka mbele taifa badala ya vyama kwa kukubaliana kukaa meza moja ya mazungumzo ili kutafuta mwafaka wa pamoja kuliko kususa tu na kukaa pembeni.

Meza ya mazungumzo itasaidia kila chama kutoa dukuduku lake na hatimaye kufikia makubaliano ambayo msingi wake ni kuendelea kumlinda ‘mama Tanzania’ kama anavyoshauri Mbatia.

Suala la meza ya mazungumzo limewahi kuhimizwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mstaafu Francis Mutungi, baada ya CHADEMA kutaka kufanya maandamano nchi nzima Septemba mosi, mwaka 2016.

Lengo la maandamano lilikuwa ni kupinga hatua ya serikali kukataza kufanya mikutano ya kisiasa, lakini Mutungi, akashauri kuwapo kwa kikao cha pamoja kati yake na viongozi wa vyama vya siasa kupata muafaka.

Wakati CHADEMA wakiwa wamepanga kufanya maandamano waliyoitwa,  UKUTA, CCM nao kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM), walikuwa wameomba kibali cha kufanya maandamano.

Kufuatia mvutano huo wa hatua ya upinzani kusisitiza kufanya maandamano licha ya katazo la serikali, msajili aliamua kuitisha mazungumzo ili kupata maridhiano, hali ambayo ilisaidia kuwapo kwa utulivu.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba busara ya majadiliano ni njia sahihi kukabiliana na mizozo kama hiyo inayotokana na uchaguzi mkuu hadi baadhi ya vyama kutopeleka bungeni wabunge wa viti maalum.

Mwaka 2016, hata Spika Job Ndugai, aliwahi kuita wabunge wa upinzani katika meza ya mazungumzo baada ya kususia vikao.

Wakati akiitisha meza ya mazungumza, alisema, ili bunge lifanye kazi yake, linahitaji kuishinda changamoto iliyopo ya muhimili huo kutokuwa kitu kimoja, huku akielezea kuwa chanzo kikuu cha kusambaratika ni pamoja na "u-vyama" kuzidi na wabunge kutojali maslahi ya taifa.

Hayo ya Jaji Mutungi na Ndugai, ni machache yanayoonyesha umuhimu wa kukaa katika meza ya mazungumzo pale linapotokea jambo ambalo linaonekana halijakaa sawa.

Lakini, iwapo kila chama kitaendelea kuvutia upande wake bila kujali maslahi ya taifa, bado kutakuwapo na malalamiko yasiyofikia mwisho, ambayo huenda yangetatuliwa na meza ya mazungumzo.

Hivyo, ni vyema wanasiasa wakalipa uzito suala la kukutana katika meza ya mazungumzo ili kuwekana sawa na kumaliza sintofahamu iliyopo baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.