Mfumo Elimu ya Juu ni jipu

21Feb 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Mfumo Elimu ya Juu ni jipu

VIONGOZI duniani katika kufanikisha majukumu yao ya kiuongozi, wamejiwekea mifumo na taratibu za faragha na za wazi, za kupokea taarifa kwa siri au kwa kukutana ana kwa ana na wananchi.

Vipo vikosi maalumu ambavyo hupenyeza taarifa kwa kiongozi, lakini pia mbali na vyombo vya habari, viongozi hutumia wasaidizi wao wa chini kupata taarifa hizo.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mbali na kupata taarifa kwa siri, alikuwa na utaratibu wa kuzungumza na wazee wa Dar es Salaam, kila alipokuwa na jambo la kuzungumza na taifa.

Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alikuwa na utaratibu wa kusikiliza matatizo ya wananchi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, huku pia akialika wanahabari Ikulu kila mwisho wa wiki, kuzungumza nao au kupitia mwakilishi wake.

Benjamin Mkapa, alihutubia taifa kila mwisho wa mwezi, utaratibu ambao pia ulirithiwa na Dk. Jakaya Kikwete. Ili mradi kila mmoja kwa njia yake, alipata taarifa alizostahili au kuzitaka.

Dk. John Magufuli, amekuwa akizungumza na taifa katika karibu kila hafla au tukio linalofanyika Ikulu, lakini pia akisimama barabarani akiwa kwenye ziara kutoka au kwenda mkoa fulani nchini. Katika ziara hizo, amekuwa akisikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuchukua hatua wakati mwingine za papo hapo.

Hivi karibuni, akiwa katika ziara kama hizo, Rais Magufuli alikutana na kijana Yusufu Juma, aliyedai anatoka Musoma Vijijini, akijitambulisha kuwa amesoma ‘Udaktari Engineering’, huku akibabaika kueleza kasoma wapi, akidai Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), na alipoulizwa na Rais kiko wapi, akasema Dodoma!

Na katika hali ya kubabaika zaidi na kuonesha yawezekana kuwa ‘mwezi mchanga’, akang’ang’ania kuwa amesomea kutengeneza vifaa tiba na kulalamika kuwa wakati yeye ana shahada na hana ajira, wenzake waliomali za darasa la saba wana ajira na kudai anaogopa kuiba, kwani ataishia jela.

Huku Rais akionekana dhahiri kubaini tatizo la kijana huyo, au athari hasi kichwani, alimwuliza kiwango chake cha ufaulu kwa maana ya mitihani yake ya chuo kikuu (GPA), akamjibu alipata 32, na kuamshaki cheko na Rais kuwaambia hadhira kuwa duniani hakuna GPA ya kiwango hicho. Kawaida kiwango cha juu cha GPA ni kati ya 4.4 na 5.0.

Ili kuachana naye, Rais alimwambia apeleke vyeti vyake kwa Mkuu wa Wilaya na kuishia hapo. Ni dhahiri, kijana Yule kwa macho ya kawaida, alionekana hakuwa sawa kifikra ndiyo sababu hata aliyokuwa akiyasema haya kuwa na matinki licha ya kukosa hata mtiririko mzuri.

Pamoja na udhaifu huo, bado alikuwa na ujumbe kwa umma, kwamba kuna tatizo katika ajira kwa vijana hususan wanaomaliza elimu ya juu nchini na kurudi mitaani kutafuta ajira.

Akizungumza bungeni hivi karibuni, Mbunge wa Vunjo, Dk. Charles Kimei, aligusia tatizo hilo, akisema mfumo wa mafunzo kwa vijana wa vyuo vikuu nchini, hauwasaidii kupata ajira, na badala yake ni vizuri kuongezwa vyuo vya ufundi, ili kutoa vijana wanaoweza kutumia elimu yao kujiajiri na kuzalisha mali. Bila hivi, linatengenezwa bomu lisilozuilika katika jamii. Alamsiki!