Mfumo nyumba kumikumi urejeshwe kudhibiti wahalifu katika maeneo yetu

28Jun 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mfumo nyumba kumikumi urejeshwe kudhibiti wahalifu katika maeneo yetu

MOJAWAPO ya changamoto kubwa zinazoyakabili maeneo yetu kwa sasa ni tatizo la uhalifu.

Kuna uhalifu wa aina mbalimbali lakini kwa muktadha wa Tulonge hii, uhalifu unaorejewa ni ule wa ukabaji, uporaji, ujambazi, wizi wa kutumia nguvu na mauaji ambao sana yameukumba mkoa wa Pwani, siku za karibuni.

Mauaji ambayo kimsingi ni ya kuchagua, ukiangalia mtiririko mzima wa namna yalivyofanyika kwa kuwa wahalifu waliotekeleza mauaji hayo waliwalenga watu ambao kwa njia moja ama nyingine ni wanachama au wapenzi wa chama tawala.

Kimsingi Muungwana anajadili aina hii ya uhalifu kwa sababu kama alivyosema hapo juu, umekuwa ni changamoto kwa serikali, lakini hata kwa wananchi wenyewe.

Suala la watu kukabwa si jipya tena katika baadhi ya maeneo iwe mijini au vijijini, kwani kuna maeneo yaliyo maarufu kwa jinai hii ya ukabaji kiasi kwamba wakati mwingine hufanyika hata mchana kweupe na tena mbele ya watu.

Kwa mfano katika jiji la Dar es Salaam, kuna maeneo ambayo mtu hawezi kupita amevaa vitu vya thamani kama cheni au ameweka kompyuta mpakato yake nyuma ya gari na madirisha yakiwa wazi, ni lazima ataibiwa tu.

Vivyo hivyo kwa upande wa jinai zingine yaani uporaji, ujambazi na jinai ya mauaji.

Kinachosikitisha ni kuwa watu wanaofanya jinai hizi wako ndani ya jamii zetu, tunaishi nao, ni watoto, ndugu, jamaa zetu.

Lakini si hivyo tu, wakati mwingine wananchi tumekuwa tukiona wageni wakija kufanya makazi katika maeneo yetu, tusijue wanashughulika na nini, wala tusiwe na shauku ya kudadisi ni akina nani hasa na wametoka wapi.

Uzembe wote huu wa kutochukua hatua stahiki kwa kufumbia macho wahalifu, ndio ambao kimsingi umepalilia na unazidi kupalilia aina hii ya uhalifu ambayo mwisho wa siku inasababisha tupoteze wapendwa wetu, mbali na hasara ya kupoteza mali.

Muungwana anaona pengine kuna haja sasa ya kurudi kwenye mfumo wa zamani uliohakikisha usalama katika maeneo yetu mijini na vijijini.

Mfumo huo ni ule wa kuhakikisha mabalozi wa nyumba kumikumi wanakuwapo kila mahali na wanafanya kazi zao kama ilivyokuwa enzi hizo.

Enzi ambazo kila mgeni aliyefika kwenye eneo la balozi alipaswa kwenda kuripoti kwake kujitambulisha kwamba ni mgeni wa nani na amekuja kufanya nini.

Enzi ambazo kila aliyehamia kwenye eneo la balozi husika alipaswa kwenda kujitambulisha kuwa amehamia hapo na akafahamika kuwa ni mmoja wa wakazi wa balozi huyo.

Kipindi ambacho kila kijana katika eneo alifahamika vizuri na aina ya shughuli za kumuingizia kipato anazofanya zilifahamika vizuri.

Kipindi ambacho kila mhalifu alifahamika na hatua stahiki zikachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kumripoti kwenye mamlaka husika.

Kwa utaraibu wa aina hii, ndiyo maana usalama wa watu na mali zao ulihakikishwa, tofauti na ilivyo sasa ambapo mfumo huu umepewa kisogo na hasa baada ya mfumo wa vyama vingi nchini kuanzishwa.

Na ndiyo maana sasa katika maeneo yetu tunakuwa na watu wasiofahamika wanakaa kwa nani na wanafanya shughuli gani.

Hali hii ndiyo imepalilia vitendo vya ukabaji, uporaji, ujambazi na kuwapo kwa watu wanaofanya mauaji kama ilivyo katika maeneo ya Kibiti na Mkuranga.

Ni kwa muktadha huo Muungwana anaona wakati umefika sasa wa kuruhusu tena mfumo wa nyumba kumikumi urejee na kufanya kazi yake kikamilifu.

Muungwana anaamini kuwa hatua hiyo itasaidia sana kudhibiti jinai zilizorejewa na Tulonge kwa leo.