Mfumo wa Kombe la Chalenji ubadilishwe

09Dec 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mfumo wa Kombe la Chalenji ubadilishwe

MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa wanaume kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inaendelea kutimua vumbi nchini Uganda, Tanzania Bara ikiwakilishwa na Kilimanjaro Stars, upande wa pili wa Muungano ukiwakilishwa na Zanzibar Heroes.

Ni michuano ambayo bila kupepesa macho ni kwamba kadri siku zinavyozidi kusonga mbele inaonekana kupungua msisimko wake.
Cha ajabu ni kwamba wakati michuano hiyo kwa upande wa wanaume msisimko wake umepungua, lakini umehamia kwa Chalenji ya Wanawake.

Tuliona hivi karibuni michuano hiyo iliyofanyika nchini kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo mbali na kandanda safi la kuvutia kwa wanawake, tumeshuhudia idadi kubwa ya mashabiki ikihudhuria bila kujali mvua wala jua.

Kwa upande wa wanaume michuano hii inapungua msisimko nadhani kutokana na muundo wake bado ni wa kizamani na haijafanyiwa marekebisho ili kuendana na mtazamo wa kisasa.

Kwa miaka mingi sasa michuano hiyo inaendeshwa kwa mtindo wa timu kukusanyika kwenye kituo kimoja na kuchezwa kwa muda wa wiki mbili.

Mfumo huu ambao unatumika pia kwenye michuano ya Kagame Cup unaonekana umepitwa na wakati na Cecafa inatakiwa ikae kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kubadilisha mfumo kuendana na wakati.

Ukiangalia hata huko nyuma, hata mfumo huu unaotumika sasa ulibadilishwa, hivyo kumbe inaonekana kabisa kuna uwezekano wa watu kukaa na kuangalia mfumo mbadala.

Zamani kabla ya mfumo huu wakati huo zikishiriki timu nne, hakukuwa na robo, nusu fainali au fainali, badala yake timu zilikuwa kundi moja na kucheza kwa mfumo wa ligi, inayokuwa na pointi nyingi ndiyo bingwa.

Nchi wanachama zilivyokuwa zikiongezeka ndipo mfumo ulipobadilishwa na kuwekwa makundi, huku timu mbili za juu zikitinga hatua ya nusu hadi fainali na zilipokuwa zinazidi kuongezeka ilifika hatua mtoano unaanzia robo fainali hadi fainali.

Ingeweza kuwa hata msimu huu hivyo, lakini kutokana na Ethiopia, DR Congo, Rwanda na Sudan Kusini kujitoa, makundi yamebaki mawili tu, hivyo kila kundi litatoa washindi wawili zitakaingia nusu fainali.

Ni wakati sasa wa Cecafa kubadilika na kuweka mfumo mpya kama ambavyo tayari nchi za Ulaya zimeanza kufanya.

Michuano kama hii sasa ingeweza kabisa kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ili kuepusha ligi kusimama, lakini kuifanya kuwa na mvuto zaidi.

Mfano kwa makundi yaliyopo sasa timu hizo zingekuwa zikisubiri Kalenda ya Fifa ndipo ziwe zinacheza na hiyo kuifanya michuano hiyo endelevu, badala kuwa ya wiki mbili tu.

Ni mfumo ambao unaweza kutumika hata kwenye michuano ya Kagame Cup ili kuipa thamani michuano ya Cecafa na kuzipa nguvu klabu zake pamoja na wachezaji kucheza mechi nyingi.

Cecafa ingeweka mechi za fainali tu kuwa iwe moja tena iwe inachagua nchi na uwanja wa kucheza fainali mapema kabisa wakati wa droo, lakini makundi, robo na nusu fainali ingekuwa inachezwa nyumbani na ugenini.

Ikifanya hivi, inawezekana kabisa michuano hii ya kwa upande wa wanaume kwa timu za taifa na Kagame Cup kwa klabu ikarejesha mvuto na msisimko wake wa miaka ya '80 hadi katikati ya '90, lakini hii ya kuzikusanya timu sehemu moja, imepitwa na wakati.