Mgogoro wa ardhi Mvemero ni 'jipu' hatari

14Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Mgogoro wa ardhi Mvemero ni 'jipu' hatari

TANZANIA ina ardhi yenye ukubwa wa hekta milioni 94.5, kwa ajili ya matumizi ya kilimo, ufugaji, makazi, hifadhi na matumizi mengine, lakini bahati mbaya migogoro ya ardhi ni tishio kubwa la amani ya nchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Chanzo kikubwa cha migogoro hiyo kinaweza kuwa ni ardhi hiyo kuwa haijatengwa maalum kwa ajili ya wakulima kwa upande mmoja na malisho ya mifugo kwa upande mwingine.

Kuna ongezeko kubwa la wafugaji ambao hawazingatii mbinu za ufugaji bora, na hii inatokana na kushindwa kuwabadilisha kuwa wafugaji wenye kuzingatia mbinu na stadi za kisasa zilizo na tija.

Inawezekana kuna usimamizi duni na usioridhisha wa matumizi bora ya ardhi miongoni mwa watendaji waliokabidhiwa dhamana na majukumu ya uongozi juu ya ardhi, na uelewa mdogo wa sera na sheria.

Hata dhana ya uwekezaji na wawekezaji inawezekana bado haijafahamika vya kutosha kwa taifa, kwani taifa linahitaji wawekezaji ili kukuza mitaji na uchumi wa nchi kwa ujumla na wawe wawekezaji makini na wabia katika maendeleo ya nchi.

Hivyo ni vyema wawekezaji wasipewe ardhi inayohitajika kwa matumizi ya wananchi katika maeneo husika na ikibidi, sera na sheria zinazosimamia umiliki na matumizi ya ardhi zifanyiwe marekebisho.

Lengo liwe ni kuhakikisha wawekezaji kutoka nje ya nchi wanashirikiana na wazawa, mamlaka za serikali za mitaa na vyama vya ushirika katika kuanzisha miradi ya pamoja ama katika umiliki na uendelezaji ardhi.

Lakini bahati mbaya hayo yamekuwa hayafanyiki na matokeo yake kila kukicha ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kati ya wananchi na wawekezaji hadi kusababisha umwagaji wa damu!

Nakumbuka enzi la utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa ili taifa liendelee linahitaji vitu vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Hivyo vyote vipo na ardhi ndiyo msingi wa uchumi wa taifa na msingi wa maisha ya mwanadamu ambayo sasa inageuka kuwa janga kwake kutokana na migogoro inayoendelea nchini hadi kufikia kugharimu maisha yake.

Umefika wakati sera ya ardhi ikaangaliwa upya ili kuboreshwa kuendana na mahitaji ya Watanzania wa sasa, ili kuwaepusha na migogoro ambayo kila uchao inaibuka upya.

Nakumbuka enzi hizo ardhi ilikuwa ni mali ya umma na haikuwa na thamani na halikuwa suala la kufa na kupona kwa Mtanzania kugombea ardhi, hasa ikitiliwa maanani kuwa Tanzania ina ardhi ya kutosha kwa ajili yua matumizi ya ufugaji, kilimo, makazi na shughuli nyingine za kiuchumi kwa pamoja.

Wakati huo serikali ilipokuwa ikihitaji ardhi isiyoendelezwa kwa ajili ya miradi mbali bali ya maendeleo iliitwaa pasipo fidia yeyote kwani fidia ililipwa tu kwa maendelezo yaliyofanyika kwenye ardhi husika, lakini si watu kulipwa fidia kwa ajili ya ardhi isiyoendelezwa.

Mwaka 1999 sheria mpya ya ardhi Namba 4 na 5 zilitungwa na kupitishwa na Bunge na kwa mara ya kwanza ardhi kutamkwa kuwa na thamani. Kwa hiyo serikali inapohitaji ardhi kwa ajili ya miradi ya maendeleo inalazimika kulipa fidia mara mbili, yaani kufidia ardhi kwa bei ya soko na kufidia muendelezo uliofanyika.

Baada ya utaratibu huo sasa wananchi wanyonge wamekuwa wakiporwa ardhi yao na watu wenye fedha kwa sababu ya ardhi kugeuka bidhaa inayonunulika na kuuzika kwa mujibu wa sheria.

Kama ilivyo katika bidhaa nyingine, hujitokeza walanguzi ambao hutumia ujanja kupandisha bei ya bidhaa husika na matokeo yake ni wanyonge kupokonywa ardhi yao kwa visingizio mbalimbali na hivyo kuongeza migogoro ya ardhi nchini.

Kwa ujumla ni kwamba migogoro ya ardhi ni mingi nchini na hasa mkoani Morogoro wilaya ya Mvomero ambako Desemba mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, Mwigulu Nchemba alifika katika Kijiji cha Dihinda Kata ya Kanga kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya tukio baya la mauaji na kujeruhi binadamu na wanyama.

Wakati tukio hilo likiwa halijasahaulika vichwani mwa Watanzania, mwanzoni mwa wiki hii limebuka lingine la kujeruhiwa kwa mfugaji na kisha mifugo yake 200 ikiwamo mbuzi na kondoo kukatwa mapanga.

Tayari kuna watu ambao wamekamatwa na vyombo vya dola kuhusiana na tukio hilo wakiwamo wenyeviti wa serikali za vijiji vya Mkindo, Patrick Longomeza (52) na mwenzake wa Dihombo, Christian Thomas (50) na wananchi wengine 19 kwa tuhuma za kujeruhi mifugo mali ya mfugaji huyo.

Amekamatwa pia mtuhumiwa kinara wa uhamasishaji vijana wa Kimasai kuwapiga na kuwajeruhi wakulima wanaolima katika bonde la Mgongola, Kashu Moreto (68) kwa tuhuma za kulisha mazao na kumjeruhi mguu wa kulia, mkulima Ramadhan Juma (19), mkazi wa Dihombo.

Ninaweza kusema kuwa mgogoro wa ardhi Mvemero ni jipu hatari ambalo linahitaji kutumbuliwa haraka hadi kuondoa kiini chake ili wakulima na wafugaji waweze kuishi kwa amani. Kwa maana hiyo, kitafutwe chanzo cha mgogoro huo na kupatiwa ufumbuzi haraka.

Haitoshi kukamata watuhumiwa tu bali kinachotakiwa kufanywa ni kwenda mbali zaidi kwa kutafuta kile kinachosababisha makundi hayo kuhasimiana kiasi hicho.

Ninasema hivyo kwa sababu hata waziri Nchemba ameshakaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa tatizo sio wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima bali uhasama ambao unahitaji kutafutiwa ufumbuzi.