Mgombea binafsi mwarobaini kwa hamahama ya wanasiasa

06Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mjadala
Mgombea binafsi mwarobaini kwa hamahama ya wanasiasa

KATIKA siku za hivi karibuni tumeshuhudia wimbi katika uga wa kisiasa la wanasiasa wakihama vyama vyao, kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Na kwa sehemu kubwa limehusisha viongozi wa siasa kutoka vyama vya upinzani kwenda chama tawala kwa maana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kinyume chake, yaani kutoka CCM kwenda vyama vya upinzani.

Kimsingi, wamehama Madiwani kadhaa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenda CCM, pia amehama Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenda CCM.

Na kwa upande mwingine, tumemshuhudia mbunge wa CCM akienda Chadema.

Lakini si wabunge na madiwani tu, bali tumeshuhudia viongozi wenye nyadhifa mbalimbali nao wakikumbwa na jinamizi hilo la kuvihama vyama vyao.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) pamoja na viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo katika nafasi mbalimbali ambao wakikimbilia CCM.

Ieleweke kuwa yote hiyo ni kheri kwani ndiyo demokrasia yenyewe katika uga huu wa kisiasa na katiba ya nchi inaliruhusu hilo na kimsingi sina tatizo na uamuzi wao huo katika muktadha mzima wa demokrasia nchini.

Tatizo nilionalo mimi ni matokeo ya hatua yao hiyo ambayo pamoja na mambo mengine yanasababisha kurudiwa tena kwa uchaguzi.

Uchaguzi unaowahusu wanasiasa waliohama vyama vyao wakiwa ni wawakilishi wa wananchi, kwa maana kuwa walichaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura.

Mjadala unaona kwamba kwa wabunge na madiwani ambao huchaguliwa na wananchi, kitendo chao cha kuhama chama kimoja kwenda kingine hakina maelezo mengine yoyote zaidi ya kuwa ni kitendo cha kutoheshimu maamuzi ya wananchi ya kumchagua mtu kuwa mwakilishi wao.

Inakuwa kama vile vyama ndio vinachaguliwa na sio mtu wakati ukweli ni kuwa wananchi huwa wanachagua watu walioko kwenye vyama.

Kwa hili mjadala unaona kuwa kuna umuhimu kwa ukuu wa vyama ukafifishwa kwa faida ya demokrasia.

Na ndio maana chama kinapoleta mgombea dhaifu kwenye uchaguzi wa kidemokrasia, wananchi huwa na uwezo wa kuchagua mgombea wa chama kingine ambacho kimeweka mgombea shupavu na kumuacha mgombea dhaifu.

Kwa lugha nyingine ni kwamba watu huwa hawalazimishwi kula ‘matango pori’.

Tatizo jingine la kitendo cha wawakilishi hao wa wananchi kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine ni la gharama za uchaguzi wa marudio.

Kimsingi gharama hizo huwa ni mzigo kwa wananchi ambao ndio walipa kodi kwani fedha hizo za kugharimia uchaguzi wa marudio ni kodi yao.

Mjadala unaona hili la kuingiza gharama mpya kwa walipa kodi halikubaliki na hasa ikichukuliwa kuna maeneo mengi ambao yanazihitaji fedha hizo yakiwamo ya huduma za kijamii.

Kwa mtazamo wangu ninaona hamahama hizi hazina tatizo kwa viongozi wa vyama wasio na dhamana ya kuchaguliwa na wananchi.

Wakati umefika sasa wa kuwa na mgombea binafsi kwa kuwa tatizo lililopo ni la misimamo ya vyama, na wagombea binafsi wakiwepo hawatabanwa na sheria za vyama.

Kwa hali hiyo mgombea binafsi atakuwa na mwanya wa kukosoa kwa uhuru panapohitajika na hata kuunga mkono inapobidi.

Lakini pia inaweza ikaanzishwa kanuni ya kuwalinda wachaguliwa kuwa na uhuru wa kukosoa upande wao bila hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu na vyama vyao pale anapoamini ni kwa maslahi ya wananchi ama wanapohama basi wahame na vyeo vyao.

Kwamba kama ni diwani ama mbunge wa Chadema anapohamia CCM anahama na udiwani ama ubunge wake na vivyo hivyo wa CCM anapoenda vyama vya upinzani.

Hapo hakutakuwa na gharama za uchaguzi na fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya uchaguzi na kampeni, na fedha hizo zikaelekezwa kwenye majukumu yenye tija kwa jamii na Taifa.Mwish