Miaka 60 ya uhuru, huduma afya zilikuwa kule, leo hapa

09Dec 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Miaka 60 ya uhuru, huduma afya zilikuwa kule, leo hapa

LEO ni kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, mwaka 1961, lakini miaka michache jina hilo likabadilika na kuitwa Tanzania, kutokana na muungano wake na Zanzibar.

Ndani ya miaka hiyo 60 ya Uhuru, Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwamo ya afya, hasa kutokana na huduma za afya kuongezeka na kusogezwa karibu na wananchi.

Mfano mmojawapo ni kwamba wakati nchi inapata uhuru, kulikuwapo na vituo 1,343 vya kutoa huduma za afya ngazi zote na sasa vimeongezeka na kufikia 8,537, jambo ambalo kimsingi ni la kujivunia.

Serikali inamiliki asilimia 64 ya vituo hivyo, huku mashirika ya dini yakiwa yanamiliki asilimia tisa na watu binafsi asilimia 27, ambapo mtandao wa huduma za afya umepanuka na kusogea zaidi karibu na wananchi.

Kwa sasa kuna zahanati 724, vituo vya afya 926, hospitali za wilaya 178 na hospitali 151, za kibingwa ngazi ya mikoa zikiwa 28, ngazi ya kanda zipo sita, za ubingwa maalum ni tano na hospitali ya taifa moja.

Hatua hiyo ya kuongezeka huduma za afya, inaonyesha ni namna serikali imedhamiria kumwondoa adui maradhi kwa wananchi wake, ili Watanzania waweze kuwa na afya njema.

Kuwa na afya njema kunamwezesha mtu kufanya kazi zake kwa ufanisi na hatimaye kujiletea maendeleo kwa kuinua uchumi wake na wa taifa, hivyo vyema kufurahia ongezeko la huduma za afya.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni alipokuwa anaelezea mafanikio ya Wizara ya Afya katika miaka 60 ya uhuru, Waziri Dk. Dorothy Gwajima alifafanua mengi zikiwamo takwimu za zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Ninatambua kuwa kila kwenye mafanikio, hapakosi changamoto, ni kweli kuwa baadhi ya zahanati, vituo vya afya hakuna watumishi wa kutosha na pia vifaa tiba, lakini ni muhimu kutambua kuwa kuongezeka kwa huduma za afya ni hatua na pia kupata watumishi wa kutosha pia ni hatua nyingine.

Muhimu Watanzania wajivunie kilichoko, huku hatua zaidi za kuboresha huduma za afya zikiendelea kuchukuliwa, kwani siyo siri kwamba huduma za afya zimeongezeka nchini.

Tunaposherehekea miaka 60 ya uhuru, ni muhimu kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu pale anapotakiwa, kwani kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa mwaka 1964, 'Inawezekana, Timiza Wajibu Wako', kila mmoja atimize.

Hata kwenye suala la ujenzi wa zanahati, vituo vya afya na hospitali, wananchi wanaweza kushirikiana na serikali kwa kutoa nguvu kazi zao au fedha kwa ajili ya ujenzi huo katika maeneo yao.

Waliotambua umuhimu huo wamekuwa wakishirikiana na serikali katika ujenzi huo, ambapo baadhi ya wilaya zinakaribia kuwa na zahanati kwa kila kijiji, kutokana na wananchi kushiriki kikamilifu.

Si vibaya kila mmoja akatumia falsafa ya Mwalimu Nyerere ya 'Inawezekana, Timiza Wajibu Wako' na kufanya sehemu yake kwenye ujenzi wa zahanati katika kijiji chake kama mkakati wa kumwondoa adui maradhi.

Watanzania wakiendelea kuungana na kushirikiana na viongozi wao kwa dhati, lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi linaweza kufanikiwa kwa kishindo na kuwafanya wasitembee umbali kufuata huduma hiyo.