Miaka 60 ya Uhuru imevuka salama, kilichoko ‘kazi iendelee’ mbele

10Dec 2021
Jenifer Gilla
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Miaka 60 ya Uhuru imevuka salama, kilichoko ‘kazi iendelee’ mbele

DESEMBA 9, mwaka 1961, Tanganyika ilishusha chini bendera ya mkoloni na kuipandisha ya taifa huru pamoja na Mwenge wa Uhuru, kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni ishara kuwa na taifa huru lenye kufanya mambo yao wenyewe.

Jana, Tanganyika ilitimiza miaka 60 ya Uhuru ikiwa ndani ya jina jipya la Tanzania baada ya kuungana na Zanzibar miaka 57 iliyopita. Hapo kuna mafanikio lukuki yaliyotokana na juhudi zake yenyewe, chini ya viongozi bora waliochaguliwa na wananchi kwa Uhuru.

Iwapo hujui, dodosa maudhui ya Muungano, faida zilizofikiwa na kero zinazojitokeza na kufanyiwa kazi kwa ustadi mkubwa, kuhakikisha zinapunguzwa kuelekea kumalizwa.

Katika hotuba yake juzi usiku, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele, kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata ndani ya kipindi hicho.

Aliyataja baadhi kuwa ni kulinda uhuru wa nchi na mipaka yake, kujenga umoja wa kitaifa, amani, utulivu na mshikamano wa wananchi, kuimarisha uchumi na kupunguza umaskini.

Rais alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuongeza upatikanaji na kuboresha huduma kwa wananchi, kujenga heshima ya nchi, ushawishi kikanda na kimataifa na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria nchini.

Pia alisema uchumi wa nchi umekua, hata leo hii nchi inajinasibu imeingia kwenye uchumi wa kati kabla ya mwaka uliokusudiwa (2025), huku mwaka1961 uhuru ulipopatikana, wastani wa pato la mwananchi likikuwa kutoka Sh.776 kwa mwaka, hadi Sh. milioni mbili mwaka jana, 2020.

Rais pia alijivunia maboresho ya huduma za kijamii ikiwamo elimu, akitoa mfano sasa kuna vyuo vikuu 30, kati yake 18 vikimilikiwa na serikali, mamilioni ya wanafunzi kwenda sekondari, hospitali za kibingwa zipo tano na hospitali ya taifa moja, kuimarishwa huduma ya maji na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hakika ni jambo la kujivunia, kwa kuwa bado kuna nchi zinapambana kufikia hatua ambayo Tanzania ipo kwa sasa. Lakini, ni muhimu kukumbushana kwamba, si kigezo cha kuzembea kwa kudhani kuwa kazi imekwisha, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunasongambele zaidi, hata kufikia uchumi wa juu.

Bado kuna mambo yanaonekana kikwazo katika kufikia uchumi wa juu, ikiwamo baadhi ya shughuli za kijamii kuwa duni.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema kuwa hali ya udumavu nchini bado si nzuri, akiitaka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kuchukua hatua za kukabiliana na adha hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za lishe ya mwaka 2019/2020, mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, ndiyo yenye viwango vikubwa vya udumavu kwa watoto, mfano hai Njombe ina udumavu wa asilimia 53.6, wakati uzalishaji wa mazao tani 446,491 kuwa na kiwango cha utoshelevu- (SSR) asilimia 194 na Mkoa wa  Rukwa asilimia 47.9, huku uzalishaji ni tani 943,002 na kiwango cha utoshelevu asilimia 230.

Kila mmoja kwa nafasi yake nchini, anapaswa kuwajibika na kuhakikisha tunamaliza changamoto hiyo, pamoja na nyinginezo kama athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo unaitesa dunia kwa sasa, inayoweza kuchangia ongezeko la udumavu kama isipodhibitiwa vilivyo.

Tuungane kwa vitendo na kauli ya Rais Samia Suluhu ya ‘Kazi Iendelee’, ikiwa na maana ya kuendelea pale tulipoishia kwa kasi ileile au zaidi, ili kufika pale taifa linapokusudia na kwa rehema zake Mwenyezi Mungu mwakani, tutakapoadhimisha sherehe hizi tufurahie mafanikio zaidi.