Miaka 60 ya Uhuru na kazi ziendelee

08Dec 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Miaka 60 ya Uhuru na kazi ziendelee

MIONGONI mwa sifa ambazo Tanzania inapata katika miaka ya mwanzo ya uhuru, ni kwenye diplomasia ya ukombozi Kusini mwa Afrika hatua hiyo ikihusisha mikakati ya kushawishi kuwapo na mtangamano wa Afrika.

Wakati huo Mwalimu Julius Nyerere, akijikita kuendeleza mshikamano, kutatua migogoro katika nchi hizo na kusimamia sera zake za nje na kufanikiwa kuzifanya kuwa karibu.

Tanzania inapotimiza miaka 60 ya uhuru, ina mengi iliyofanya hata nje ya mipaka, ikiwamo kuhifadhi wapigania uhuru na kuongoza mapambano ya uhuru Kusini mwa Afrika; Msumbiji, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Namibia na Angola.

Si hapo tu, bali pia imepigania umoja wa Afrika kwa kuanza na mtangamano wa kikanda kama kuanzishwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na pia kurejesha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977.

Pamoja na hayo, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Tanzania imepokea na kuhifadhi wakimbizi kutoka mataifa jirani ambao nchi zao zimekumbwa na migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kesho Watanzania watakuwa wanahitimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa nchi yao, uliopatikana Desemba 9, mwaka 1961, wakiwa wamoja na wenye kuvumiliana katika mambo mbalimbali kama itikadi tofauti za kisiasa.

Hali hiyo inatokana na misingi ya amani ambayo imekuwapo kabla na baada ya uhuru, ambayo imesimamiwa na viongozi waliopita na sasa inaendelezwa na waliopo madarakani kwa manufaa ya Watanzania.

Lakini, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopokea mageuzi ya kisiasa mwaka 1992 na inayaendeleza kwa amani ingawa zipo kasoro kadhaa zinazolalamikiwa na vyama vya upinzani.

Pamoja na kuwapo kwa kosoro bado kumekuwapo na umoja, huku viongozi wa vyama hivyo wakitafuta zaidi kuwapo kwa meza ya mazungumzo ili kupata muafaka kumaliza tofauti.

Wakati huu ambao nchi inaadhimisha miaka 60 ya uhuru, ni vyema kuendelea kuwa na utaratibu wa majadiliano ili kuapata mufaka kwa njia ya mazungumzo ambao kimsingi unaendelea kuwafanya Watanzania kuwa wamoja.

Wakati wa kusherehekea uhuru pale panapohitajika kuongeza kasi kwa ajili ya kumaliza malalamiko ya kisiasa au kero za Muungano, basi ingependeza kama itaongezwa ili kuendelea kuimarisha umoja wa Watanzania wote.

Kwa kuwa nchi imetimiza miaka 60 huku watu wake wakiwa wamoja, basi si vibaya kama kasoro ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwenye siasa na hata katika muungano zikafanyiwa kazi.

Ninaamini kwamba, kila Mtanzania kwa nafasi yake, ana mchango katika kuhakikisha mambo ambayo anadhani yanaweza kusababisha umoja ukasambaratika yanapatiwa ufumbuzi.

Kila mmoja anaweza kushirikiana na viongozi wa umma kwa kutoa ushauri au mchango wa kumaliza tofauti za kisiasa kati ya vyama vya upinzani na serikali, kutokana na kwamba wote wanajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania.

Hivyo, kwa hali hiyo haina haja kugombea fito na kusababisha kutokuwapo kwa umoja ambao umedumu kwa miaka 60 ya uhuru sasa bila kuwapo vurugu za kisiasa.

Kama ambavyo nchi ilipokea mageuzi ya kisiasa bila vurugu, ni vyema kuyaendelezwa, na ndivyo hata katika suala la muungano kama ambavyo umewafanya Watanzania kuwa wamoja, nao uendelee kuimarishwa.

Jambo la muhimu katika kufanikisha hayo yote ni kila mmoja kufanya sehemu yake kwa kuepuka kugawanywa kwa tofauti za kisiasa au kwa namna yoyote ile inayoweza kusababisha watu kutokuwa wamoja.