Michezo hii ya kubahatisha inatuharibia watoto mitaani

02Nov 2017
Yasmine Protace
Nipashe
Mjadala
Michezo hii ya kubahatisha inatuharibia watoto mitaani

PAMOJA na serikali kuagiza kisheria kwamba michezo ya kubahatisha ichezwe na watu wazima, kwa maana ya mwenye umri wa maika 18 na kuendelea, agizo hilo katika baadhi ya maeneo halizingatiwi.

Ukweli ni kwamba, kuna watoto walio na umri chini ya ruksa iliyotolewa kwa mujibu wa maelekezo hayo, nao wanashiriki kucheza, jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya sheria.

Tunaposema hilo halizingatiwi, tuna maana kuwa mchezo wa kubahatisha kwa sasa upo hadi katika makazi ya watu. Katika baadhi ya sehemu utawaona watoto walio na umri mdogo zaidi wakishiriki mchezo huo, tena kwa kujiamini zaidi. Inashangaza.

Mtu akifika katika mitaa ambayo ina mashine ya kucheza michezo hiyo, utakuta watoto wenye umri mdogo zaidi, hataa darasa la kwanza, nao wanaendelea kuucheza mchezo huo, tena kwa kupewa fedha na wazazi wao.

Utakuta wazazi wamekaa maeneo ya nje ya makazi yao ambapo kunachezwa michezo hiyo, mzazi au lezi anampatia mtoto kiasi cha shilingi 200, ili aende kubahatisha na akifanikiwa kupata fedha, anatimua mbio kwenda kununua vitafunwa na soda.

Michezo ya kubahatisha katika mashine zilizofungwa mitaani, unaanza kwa kucheza kiasi cha Sh. 200, ambapo wazazi kukitoa kiasi hicho cha fedha kwao ni kitu cha kawaida.

Sasa, tujiulize huyo mtoto anatengenezewa mazingira gani ya kielimu na mzazi wake, kama kila kukicha anashinda katika mashine hiyo kwa ajili ya kucheza mchezo wa kubahatisha, inakuwaje?

Ninachojua ni kwamba, serikali imeweka vigezo vya mtu kucheza michezo ya kubahatisha na kuna sehemu ya kigezo kinachoelekeza watoto wenye umri chini ya miaka 18, hawaruhusiwi kucheza.

Pia, hao waliopewa hizo machine kuziweka katika mitaa, wanayo elimu juu ya vigezo vya umri wa watu wa kucheza michezo hiyo au kazi yao, ni kukusanya hela bila ya kujali athari kwa hao watoto.

Kinachoshangaza, huo mchezo katika mitaa hata kuna kinamama ambao hawapo nyuma, kukiuka ustawi wa watoto wanaowalea. .
Utakuta nao wanacheza mchezo wa kubahatisha na fedha wanazozipata, wanazitumia kushiriki kwenye vikoba na matumizi mengime ya nyumbani.

Kuna haja wanaotoa hizo mashine kujenga utaratibu wa kutembea hayo maeneo na kuona wahusika wa mchezo huo, ni wale ambao wana sifa au la.

Hakutakuwapo utamaduni wa kuwatembelea watu waliopewa mashine, idadi kubwa ya watoto mitaani hawatakuwa na mawazo ya kusoma, bali mawazo ya kubahatisha kupitia michezo hiyo, ili wapate fedha za kujikimu.

Tukiangalia hii michezo ya kubahatisha katika sehemu kubwa, mahali kunakofanyika kuna askari milangoni kuwadhibiti watoto wanaopenya, ili wasiingie kucheza.

Kuwarudisha huko ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria, chini ya usimamizi wa Mamlaka na Bahati Nasibu ya Taifa. Sifa za anayetaka kucheza mchezo huo anaelezwa awe anaanzia miaka 18 na kuendelea.

Rai yangu ni kwamba, tusiwafumbie macho watoto wanaojiingiza katika michezo hiyo wakiwa na umri wa miaka michache, kwani kufanya hivyo kunaweza kukachangia mahadhurio yao shuleni kuwa duni, kutokana na watoto kukimbilia mchezo wa kubahatisha.

Wito kwa wazazi, hizo fedha ambazo wanawapatia watoto wao kwa ajili ya kwenda kucheza michezo ya kubahatisha, inaweza kuwafanya watoto kujiingiza katika matukio yasiyofaa pale ambapo wataikosa hiyo pesa.

Tukumbuke, mtu anapocheza kinachoitwa ‘mchezo wa kubahatisha,’ kuna kipindi anapata au kosa pesa inayohitajika.

Sasa, inapotokea mtoto amekosa, sidhani kama mzazi atakuwa na fedha za kumpa kila mara na kinachoweza kutokea, ni kwamba mtoto anaanza kuwa mdokozi wa hela ndogo, ili afikie lengo la kucheza mchezo wa kubahatisha ulio mbele yake.

Wazazi wanaoendekeza watoto wao kuwapatia hela za kucheza mchezo wa kubahatisha, wanapaswa kufuatilia madaftari yao kama wanafanya vizuri shuleni na mengine yanayohusu maendeleo ya watoto hao.