Michezo isifanywe uadui

21Mar 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Michezo isifanywe uadui

MCHEZO ni jambo ambalo watu au timu hulifanya kwa kushindana ili kupata mshindi. Pia ni kazi ya sanaa ambayo huigizwa kwa ajili ya kuelimisha na kuburudisha watu.

Aidha ni jambo ambalo mtu hulifanya kwa kupitisha wakati au kujifurahisha; masihara.

Kwa waliofuatilia tamthilia ya ‘Mambo hayo’ iliyorushwa na runinga ya ITV miaka ya nyuma, nadhani wanamkumbuka Mzee Kambaulaya au baba Bishanga alipokuwa na vijana kwenye michezo ya kuigiza.

Ndiye mwandishi wa makala unayosoma sasa na kila Jumamosi kwenye gazeti hili ukurasa wa 6: ‘Muungwana Lazima Nilonge.’

Nimekuwa mwanachama kindakindaki (halisi) wa Yanga tangu mwaka 1966 kwa kadi namba 447 na ya sasa ni namba 007887 (Daima mbele nyuma mwiko). Sare nne mfululizo ilizopata Yanga, baadhi ya watani (Simba) waliniita ‘mzee wa sare sare!’ Sikatai kwani ndio utani.

Mchezo wa kandanda abadan (katu) si vita au chuki baina ya wachezaji wala watazamaji wa pande zote zinazopambana.

Ni mchezo unaojenga ushupavu (tabia ya kuwa imara, ukakamavu) wa wachezaji na kuwafurahisha watazamaji, yaani wanachama wa timu na mashabiki wanaotoa fedha zao kuburudishwa nao.

Hakuna sababu ya kuchukiana, kuharibu vifaa vya uwanjani, kutukanana matusi ya nguoni na hata kupigana. Kwa nini watu wapigane ilhali wamekwenda kuburudika, kuona wachezaji wanavyopigana chenga, ‘kuvalishana kanzu’ mbwembwe zao na kufungana mabao? Hiyo ndio raha ya mchezo wa kandanda.

Nathubutu kusema kandanda ni mchezo unaopendwa zaidi duniani kuliko michezo mingine yote. Hali hiyo inathibitishwa na baadhi ya wanachama au mashabiki wa timu za Simba na Yanga wanaozirai viwanjani na pengine kupoteza maisha timu zao zinapofungwa!

Kuna mambo yanayosababisha matukio hayo. Mbali ya upenzi uliokithiri kwa timu hizi mbili nchini, pia kuna wanaowekeana madau (fedha au vitu wanavyoahidi watu kutoa kwa wanaoshindana wakati wa michezo).

Waliokubaliana kuwekeana dau ya hela, nyumba n.k. wanapoona timu yao ina dalili ya kupoteza mchezo au tayari imepoteza, ndipo hupatwa na mshtuko na kuzirai ama kufa.

Pamoja na maafa (tukio linalosababisha madhara) hayo, kuna baadhi ya wanaojiwekea nadhiri (ahadi anayoweka mtu kwa Mwenyezi Mungu ya kufanya jambo fulani vizuri au inavyopasa iwapo atafanikiwa katika haja yake) wakisahau kuwa “Ahadi ni deni na deni ujuzie.”

Maana yake ahadi ni kama deni, mtu akitoa ahadi lazima aitimize. Methali hii yatufunza umuhimu wa kutimiza ahadi tutoazo.

Mchezo wa kandanda una mambo matatu: Kushinda, sare au suluhu, na kushindwa. Timu inayoshinda ndio huzawadiwa kama walivyosema wahenga kuwa “Mcheza kwao hutuzwa.) Methali hii yatufunza kuwa mtu anayefanya jambo vizuri au inavyopasa hutuzwa au hupewa zawadi.

Starehe (jambo linalompa mtu raha) ya kandanda ni timu kucheza kwa nidhamu bila vurugu wala hasira. Je, Simba na Yanga zichezapo watazamaji hupara starehe?

Siku hizi ni nadra sana timu kumaliza mechi bila baadhi ya wachezaji wa timu zote mbili kuonyeshwa kadi za njano au nyekundu na kutolewa nnje ya uwanja. Kama mpira ni burudani na starehe, kwa nini wachezaji waumizwe kwa makusudi viwanjani?

Mchezaji unayemchezea mwenzako rafu, ukifanyiwa wewe utafurahi au utalipiza (kitendo cha kumfanyia jambo mtu kwa nia ya kurejesha ubaya aliofanyiwa) kisasi?

Tulimwona Rais John Magufuli alivyovaa siku Yanga ilivyoikaribisha Simba uwanja wa Taifa. Kwa kuwa Magufuli ni Rais wa Tanzania, alivaa shati lenye rangi na nembo za klabu zote mbili.

Alifanya hivyo kuonyesha kuwa timu zote ni za Tanzania hivyo zote zinamhusu. Hakutaka kuonesha anapendelea timu ipi kati ya Yanga na Simba ingawa binadamu hawakukosa la kusema. Eti kwa kuwa rangi na nembo ya Yanga ilikuwa upande wa kulia na Simba upande wa shoto tayari alionyesha msimamo wake ...!

Yanga na Simba ni timu za Mkoa wa Dar es Salaam unaoongozwa na kumilikiwa na mtu aitwaye Paul Makonda ambaye bila 'kumunyamunya', kiongozi huyo ni shabiki wa Simba.

Hakuna ubaya kwani kila mtu ana chaguo lake. Kwa kuwa timu zote mbili ni za mkoa anaousimamia, hakuwa sahihi kutamka maneno ya kejeli dhidi ya Yanga ilipofungwa bao 1-0 na timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC). Alisahau kuwa ofisi na makazi yake ni wilaya ya Ilala iliko Yanga?

[email protected]
0784 334 096