Miji inaweza kutunza mazingira, kama ilivyokuwa kwa wenzetu

13Nov 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Miji inaweza kutunza mazingira, kama ilivyokuwa kwa wenzetu

MOJA ya mambo ya kujifunza kutoka kwa wengine ni utunzaji wa mazingira katikati ya miji sambamba na maendeleo ya miundombinu.

Muungwana alipata fursa ya kutembelea Thailand hivi karibuni, nchi ambayo imepiga hatua kubwa kwenye miundombinu ya kisasa.
Ina mtandao wa barabara za kawaida, kulipia, treni za umeme na maeneo mengine ya watembea kwa miguu.

Licha ya kuwa na barabara kubwa zilizojengwa juu zenye kupitisha magari 16 kwa wakati mmoja yanayokwenda na kurudi, lakini utunzaji wa mazingira umepewa kipaumbele.

Lengo ni kuhakisha kuna hifadhi ya mazingira inanyonya hewa chafu na kutoa hewa safi.

Katika jiji la Bangkok, kuna makutano ya barabara yasiyohesabika yenye maumbo ya kila aina, yakiwa na barabara zilizojengwa juu ya ardhi, kila moja likiwa na kipaumbele cha utunzaji wa mazingira.

Thailand ni nchi iliyoendelea ikiwa na viwanda vingi na uchumi wake unategemea pia shughuli za kilimo na biashara, bila kusahau usafirishaji. Ni kitovu cha usafiri wa anga, barabara na maji.

Kwa uwekezaji wa miundombinu na majengo mengine mengi, ilikuwa ni vigumu sana kuona misitu au eneo lililohifadhiwa vizuri ili kuleta hali ya ukijani wa kutosha kwenye jiji la Bangkok, lakini imewezekana kutokana na kuwekwa kwenye vipaumbele vyao.

Muungwana alikaa katika jiji la Bangkok kwa siku nane na siku mbili katika eneo la Prachuap Khiri Khan, mwendo wa saa nne kutoka jijini Bangkok.

Kote huko alishuhudia jitihada za utunzaji mazingira kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu unakwenda sambamba na upandaji wa miti na utunzaji wa maeneo ya misitu midogo ndani ya miji hiyo.

Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa nyakati hizi ambazo kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Ni kwa mantiki hiyo Muungwana anaasa kwamba kasi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, inapaswa kuhakikisha miti inayokatwa kupisha ujenzi inapandwa upya kwa ajili ya kutunza muonekano maridhawa na mvuto kwa jiji na miji mingine.

Jiji la Dar es Salaam halina maeneo ya misitu na miti ya kutosha kwa ajili ya kunyonya hewa ukaa inayozalishwa na shughuli za kibinadamu, badala yake linategemea misitu ya Kisarawe ambayo nayo inavamiwa na shughuli za kibinadamu.

Kama wengine walivyoweza kutunza mazingira kadri maendeleo yanavyozidi kusonga mbele, ndivyo inavyopaswa Watanzania wafanye wakitambua umuhimu wa mazingira kwa afya zao na viumbe vingine kwa ujumla.

Unapotembelea Bangkok utaona maghorofa mengi yenye urefu tofauti lakini hatua chache utaona miti mingi ambayo inasaidia kutunza mazingira na wakati huo huo inaweka madhari nzuri.

Zipo bustani nyingi za kila aina kwenye barabara zote, hakuna barabara iliyojengwa bila kuwekwa bustani, na barabara za kwenda nje ya jiji katikati kuna miti mingi ambayo inasaidia kunyonya hewa ya ukaa inayotolewa na magari.

Ni la kuiga hata kwetu kwa mfano katika eneo la Kariakoo lililomea maghorofa mengi bila ya miti, hata kama kuna eneo linaloweza kupandwa mti husika.

Kuna maeneo kwa mfano katika jiji la Bangkok yaliyo na ardhi oevu lakini yametunzwa vyema, tofauti na maeneo yetu ambayo yamevamiwa na watu wamejenga kama ilivyo eneo la Jangwani, Kinondoni, Msasani na kwingine.

Inawezekana maeneo hayo kutunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, kwa kuhimiza jamii husika kupanda miti.

Aidha, wenye maghorofa walazimishwe kupanda miti mingi nje ya maeneo yao, huku wasimamizi wa mazingira wakihakikisha hakuna uvamizi wa maeneo yanayohitaji kutunzwa kwa manufaa ya wote.

Uharibifu wa mazingira unaweza kufanywa na wachache lakini madhara yake ni kwa jamii nzima na ndiyo maana ya mabadiliko ya tabianchi tunayoshuhudia, yaani ukosefu wa mvua, mafuriko, vimbunga na mengineyo.