Mikoa ichukue mkakati wa Shinyanga kutokomeza vifo vya uzazi nchini

18Jun 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mikoa ichukue mkakati wa Shinyanga kutokomeza vifo vya uzazi nchini

NIMEVUTIWA kuandika Tulonge hii na moja za makala zilizoko katika kijarida cha elimu kwenye gazeti hili yenye kichwa cha habari kisemacho “Shinyanga yaja na sheria ndogo ili kutokomeza vifo vya uzazi” ukurasa wa 15.

Kifupi ni kwamba mkoa huo umekuja na mkakati wa kutunga sheria ndogo zitakazotekelezwa katika ngazi ya kijiji ambapo mjamzito asiyehudhuria kliniki au anayejifungulia nyumbani ama kwa mkunga wa jadi bila kwenda kituo cha afya, atatozwa faini ya Sh. 20,000.

Kwamba mkoa umekuja na mkakati huo baada ya kuona vifo vitokanavyo na uzazi mkoani humo vinaendelea licha ya jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali za kuboresha huduma ya afya mkoani humo na mikoa mingine katika ngazi ya taifa.

Kwa mujibu ya Mratibu wa Huduma ya Uzazi na Mtoto mkoani Shinyanga, Joyce Kandolo kama alivyonukuliwa na Nipashe, idadi ya vifo vya kinamama kutokana na uzazi mkoani humo kwa mwaka 2017 ilikuwa ni 73.

Na kwamba kwa mwaka jana kinamama 56 walifariki kutokana na uzazi na mwaka huu kuanzia Januari hadi Aprili wameshafariki kinamama 18.

Kimsingi idadi hii ya vifo vya uzazi katika mkoa mmoja kwa maoni ya Muungwana si ya kuvutia na hasa ikitiliwa maanani uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali kibajeti ili kuboresha miundombinu na huduma za kiafya kwa ujumla.

Tukiitalii ripoti ya muhtasari wa matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015-16 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uwiano wa vifo vitokanavyo na uzazi ni vifo 556 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai.

Kwa maana hiyo na kwa hesabu ya Muungwana, wastani wa vifo hivyo 556 kwa mikoa 26 ya Tanzania Bara ni vifo 21 kwa kila mkoa.

Sasa mkoa unapokuwa na vifo 73 kwa mwaka 2017 au 56 kwa mwaka jana, hakika ni idadi isiyopendeza.

Ni idadi ambayo kimsingi inahalalisha hatua zote stahiki za kukabiliana na hali hiyo kama hizo zinazochukuliwa na mkoa wa Shinyanga wa kuja na sheria ndogo inayolenga kutoza faini wajawazito wasiohudhuria kliniki ama wasiojifungulia katika vituo vya afya.

Kuna mambo mengi yanayosababisha vifo vya uzazi, ikiwa ni pamoja na kuzaa katika umri mdogo, utoaji wa mimba na ukosefu wa huduma za afya zinazostahili kwa kutaja baadhi.

Sasa serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kuiboresha sekta ya afya kirasilimali watu, vifaa tiba, na miundombinu yake, kwa lengo la kustawisha maisha ya Watanzania, wajawazito wakiwamo.

Serikali inafanya hivyo kwa sababu mbali na kuboresha maisha ya kinamama lakini pia inatimiza dhima ya kusukuma mbele maendeleo ya taifa, ambapo huduma bora ya afya ni moja ya viashiria vya wazi vya namna nchi inavyoendelea.

Kwamba nchi inapofanikiwa kwa mfano kupunguza vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi, ni dalili ya maendeleo yaliyo wazi yasiyohitaji mwanasiasa kusimama jukwaani na kuhubiri kwamba nchi inaendelea kwa kasi.

Kwa hali hiyo, Muungwana ana maoni kwa mikoa mingine nchini kuja na mikakati kama huu wa mkoa wa Shinyanga, yenye lengo la kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi.

Ana maoni hayo kwa sababu tatizo hili si la mkoa wa Shinyanga tu, bali ni la mikoa karibu yote nchini.

Ninasema hivyo kwa sababu kwa mujibu wa utafiti wa NBS, takribani theluthi mbili kwa maana ya asilimia 63 ya watoto nchini Tanzania wanazaliwa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya.

bado kuna asilimia 37 ya watoto ambao wanazaliwa nyumbani ama kwa wakunga wa jadi, takwimu zinazokumba takribani mikoa yote nchini.