Mikono inapokuwasha huashiria nini?

26Nov 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Mikono inapokuwasha huashiria nini?

MPENZI msomaji, wiki moja iliyopita tuliwasikia wasomaji wetu wengi waliobahatika kusoma mfululizo wa makala za safu hii kuhusu siri iliyojificha kwenye mikono yetu, mingine ikiwasha-washa.

Ukiona mambo yanatokea waziwazi ujue kwamba tayari lipo jambo usiloliona lilishafanyika pasipo wewe kuliona au kulijua. Wewe unachukulia ni kawaida, kumbe kipo chanzo usichokijua.

Kwa mfano, kikundi cha watu kinapokaa faragha na kupanga tukio fulani baya dhidi ya mtu fulani, huku mlengwa hajui, huo ni ulimwengu wa roho. Mlengwa anashtukia anashambuliwa kisha anashangaa, kumbe tukio tayari lilishapangwa, hatua ile ya shambulio ilikuwa ni utekelezaji tu.

Mpenzi msomaji wangu, nilianza na utangulizi huo ili kukuweka sawa kuonyesha kuwa yapo mambo mengi yanatokea katika maisha yetu lakini hayakuanza siku hiyo hiyo, yalianza kitambo ila sasa yanajidhihirisha. Hata ugonjwa huanza taratibu unapochachamaa ndipo mgonjwa anashtuka.

Pia kingine, tumekuwa tunapuuzia dalili mbalimbali tukijiaminisha kuwa ni jambo la kawaida. Msomaji wangu nikuambie leo, hakuna tatizo au dalili zisizokuwa na chanzo. Wasomaji wetu ambao nilichapisha maoni na matatizo yao wiki moja iliyopita wamedhihirisha jambo hilo.

Wapo waliosema mikono yao inawasha-washa wakati mwingine kwa zamu na hawaelewi ni kwa sababu gani. Wengine wanapata pesa lakini hawafanyii kitu cha maana na pengine kuishia kwenye madeni.

Mwingine anasema  anapoteza pesa na mali zake katika mazingira tatanishi. Isitoshe, hajawahi kufanya biashara akapata faida, matatizo na mikasa mbalimbali ya kimaisha vinamuandama ikiwamo magonjwa ndani ya familia kila uchao.

Mwingine akasema; Naitwa Mario Kavindi, ni mfanyabiashara wa mbao ninazonunua. Tatizo langu nina mkosi wa kudhulumiwa mali zangu  kutokana na pato la biashara hiyo, naomba mawazo yako mama niweze kutoka hapa nilipo kimaisha.

Mpenzi msomaji, kuna mambo yanafanywa na watu wengine kuhusu wewe lakini huyaoni. Kuna vikao vinaweza kufanywa na wabaya wako lakini wewe huwaoni. Kuna wachawi wanaweza kukuchukua usiku ukiwa umelala wakakupeleka watakako pasipo wewe kujua. Vyote hivyo vinafanyika kwenye ulimwengu wa Roho (ule usioonekana).

Unaweza kuwa umevishwa kinyago kwenye mkono wako mmoja au yote lakini wewe hujui. Mikono yako inaweza kuwa imetoboka, ina mashimo yanayowapitishia maadui fedha zako lakini wewe hujui.

Hawa ndio wale wanaowashwa-washwa viganja vya mikono wakidhani eti ni dalili za mtu kumpatia pesa, kumbe ndio anaibiwa pesa zake/nyota ya utajiri. Tena wakati inapowasha ndio wakati mtu anakuwa ana pesa nyingi lakini anafanya matumizi ya hovyo hovyo sana. Hapo anaibiwa kimazingara.

Utasikia mtu anasema; leo mikono yangu inawasha, sijui nani atanipa hela. Siku au juma linapita hakuna yeyote aliyempa hata senti moja. Lakini akijichunguza, anajikuta kuwa katika kipindi cha mikono kuwasha, hata ile akiba aliyokuwa nayo ameitumia pasipo tija.

Tena linaweza kuibuka tatizo kubwa linalohitaji fedha na zisitoshe hadi akakope kwa rafiki au ndugu yake. Hizo ni hila za muovu kuhakikisha kuwa hata kile kidogo ulicho nacho unakitumia kinaisha, lengo likiwa ni kukuaibisha tu.

Ni muhimu sana tuwe na utaratibu wa kuombea mikono yetu kila siku. Tusijiamini sana kwamba tuko salama wakati maadui zetu wapo kila mahali na mbinu tofauti. Hakuna adui anayependa mpinzani wake afanikiwe na ndio maana hutafuta mbinu mbalimbali za kumuangamiza.

 Lakini ukisimama kiimani kwamba Mungu ni msikivu wa maombi yetu, hila za shetani haziwezi kushinda kamwe.

Wengine wanaota ndoto wako makaburini lakini wanapuuzia wanaona ndoto hiyo haina maana. Kumbe tayari hatma yake imeshazikwa ndio maana maisha yake yanayumba japokuwa alikuwa ni mtu wa mafanikio makubwa mwanzoni.

Wengine wanapata misukosuko ya kimaisha kutokana na imani katika koo zao. Wengine wanadhulumiwa na watu waliowaamini, kumbe kwa upande mwingine ni maadui wakubwa wa mafanikio yao.

Hakuna adui atakayependa wewe ufanikiwe. Hata kama naye amepiga hatua kubwa ya maendeleo, bado hatapenda nawe ufanikiwe kumpita yeye, achilia mbali kumfikia.

Maadui wa aina hii ndio wanaoweza kukusababishia matatizo yasiyokoma. Pia hukaa pembeni na kufurahia machungu unayopitia hata kama chanzo chake ni wao. Maisha Ndivyo Yalivyo.

  *Je, una maoni yoyote au suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]