Mkakati unaomuepusha mtoto ukatili uanzie ngazi ya familia

26Jul 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mkakati unaomuepusha mtoto ukatili uanzie ngazi ya familia

MIKAKATI ya kumlinda mtoto dhidi ya matukio ya kingono, kuna kila sababu ya jamii kushiriki kutoa ushirikiano.

Kama jamii itatoa ushirikiano kwa vyombo husika juu ya matukio ya kingono, hapana shaka matukio hayo yanaweza kumalizika kirahisi.

Hivi karibuni wadau wa semina za jinsia na maendeleo iliyoandaliwa na asasi ya GNP Mtandao, walizungumzia mikakati ya kumlinda mtoto dhidi ya ukatili uliopo wa kingono.

Kupitia semina hiyo, wadau washiriki walitoa maoni yao namna ya kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa kingono unaoendelea katika jamii.

Pelis Charles, ni kati ya wadau wa GDSS anayesema kuwa, wazazi wanatakiwa kufuatilia mienendo ya watoto watokapo shule na nje ya hapo.

Anasema kuwa wazazi, hata wanapokuwa katika baadhi ya shughuli zao kama mjumuiko wa vikoba, wanapaswa kujadili masuala ya ukatili  na kamwe, sio kujadili masuala ya pesa.

Charles, anaongeza kuwa wazazi mara zote wanapaswa kujenga utamaduni wa kuzungumza na watoto wao na kuwaeleza namna  ya kujilinda na ukatili wa kingono.

Grace Muhaba ni mwalimu katika shule ya sekondari iliyopo jijini Dar es Salaam, anasema kuwa shuleni kake wanashudia jinsi wanafunzi wanavyolalamika kuhusu ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa.

Pia, anaeleza haja ya wazazi kuwachunguza watoto wanaotoka shule, hali kadhalika wasichana waliowaajiri kutumikia majukumu majumbani.

Kwa mujihu wa Grace, sule zilizopo nchini zinapaswa kuwa na katuni na vipeperushi vingi vyenye ujumbe wa kukabili matukio ya ngono katika jamii zao.

 

Kelvin Godwin, ni mwanafunzi wa shule ya sekondari  Mabibo, anayewashauri wazazi wawe karibu na watoto na wawe wanawachunguza iwapo wameshafanyiwa ukatili wa kingono.

Lingine analoshauri wazazi kuwa marafiki wa watoto wao, ili waweze kuzungumzia kwa uwazi adha za   masuala yanayohusu ngono.

Anna Sangai, ni Ofisa wa Programu, Harakati na Ujenzi wa Nguvu za Pamoja wa TGNP Mtandao, anasema kuwa bila elimu ya kijinsia, itakuwa ngumu kwa wanafunzi wa kike kuyafikia malengo yanayowakabili.

Anaongeza kuwa, katika kumlinda mtoto na matukio hayo, TGNP Mtandao imezindua kampeni ya kuwalinda  watoto, ikitoa namna maalumu za kuwasiliana nao.

Anna, anashauri wazazi kuwa wanapaswa kutumia majumuiko wa siku ya vikoba, kujadili  masuala ya jinsia katika mjumuiko wa vikoba na vyema wakaishia kuijadili masuala ya pesa, kabla ya kuacha kuzungumzia yanayohusu ukatili wa kingono kwa watoto.

Amina Juma, ni mdau mwingine anayesema kutolewa elimu kutaisaidia jamii kutoa ushirikiano, pale tatizo litakapotokea anasema kuwa, matukio ya kingono yanapotokea, baadhi ya familia zinamalizana na hali hiyo. Hiyo inasababisha aliyefanyiwa jambo hilo kukosa haki yake.

Anasema, mila na desturi mbovu kwa baadhi ya watu imechangia panapotokea matukio hayo wamekuwa pande zote mbili kumalizana.

 

Wito wake anasema kuwa vipeperushi visambazwe katika shule ambayo vinaonyesha ujumbe unaozungumzia ukatili.