Mkataa kwao mtumwa hasa

03Dec 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Mkataa kwao mtumwa hasa

MTU anayekataa kwao huwa mtumwa mahali anapoishi. Twakumbushwa umuhimu wa kuzikumbuka asili zetu au tutokako. Twapaswa kuwaonea fahari wazazi wetu au hata mataifa yetu.

Lugha ni mpangilio wa maneno yanayotumiwa na watu wa jamii fulani katika mawasiliano; mtindo anaotumia mtu katika kujieleza.

Lughawiya ni taaluma inayoshughulikia uchambuzi wa lugha katika nyanja mbalimbali kama vile sarufi, maana, matamshi na matumizi.

Maana moja ya neno ‘baraza’ ni kikundi cha watu aghalabu (kwa kawaida) wenye mnasaba (uhusiano baina ya watu, vitu au mambo; hali ya jambo) na shughuli maalumu, walioteuliwa kusimamia shughuli iliyo katika jamii.

Hapana shaka mamlaka zinazosimamia Kiswahili zilizoundwa ili kuelekeza utaratibu mzuri wa matumizi ya maneno ya Kiswahili. Pia, kusahihisha matumizi mabaya ya maneno yanayokosewa au yasiyo ya Kiswahili.

Nathubutu kusema zinashindwa kutimiza wajibu wake. Kwa sababu hiyo, baadhi ya vyombo vya mawasiliano vinatumia maneno yasiyostahili , yanayopaswa kuishia kwenye mazungumzo ya mitaani.

Pia, huchanganya maneno ya Kiingereza na Kiswahili ingawa ni ya Kiswahili. Lahaula (neno linalodhihirisha mshangao au sikitiko).
Mfano, kuna chombo maarufu cha habari ambacho kinaonekana kupitiliza katika matumizi ya mchanganyiko huo.

“Ninukuu machache ; “Next Unai Emery hali ni tete pale ….” Kimsingi ‘next’ ni neno la Kiingereza lenye maana zaidi ya moja, lakini kwa muktadha huu ni –enye kufuata. Ni neno ambalo ufahamu wake huo wa Kiingereza, unawafikia wachache waliobahatika kudodosa tafsiri yake.

Pia, linginelo la Kiswahili liliandika: “ShowBiz… yarudishwa kitaani.”

‘ShowBiz’ ni maneno mawili na si moja kama lilivyoandikwa. Huandikwa ‘show biz’ na maana yake ni biashara au shughuli za burudani. Kwa matumizi aliyohitaji neno ‘burudani’ lingekidhi haja.

Kwa nini wachanganye Kiswahili na Kiingereza? Au tunatumia tusichokielewa vizuri ?

Ebo (neno la kuonyesha mshangao au kuonya; tamko linaloonyesha hisia ya dharau inayotokana na kukasirika au kutoridhika). Hawajui kuwa “Cha wenyewe huliwa na wenyewe?” Maana yake kitu cha wengine huwafaidi wao wenyewe.

Sentensi ifuatayo ina maana gani? “Baada ya majirani zao Tottenham kula kichwa cha kocha wao, sasa zamu ya …..” He … ‘walikula kichwa cha kocha wao’ wakiangaliwa tu bila kuchukuliwa hatua za kisheria?

Ukurasa wa mbele wa gazeti hilo iliandikwa kwa herufi kubwa: “Simba Kufuru.” Hueleza mara kwa mara kuwa maana sahihi ya neno ‘kufuru’ ni sema au amini jambo kinyume cha mafunzo ya dini yako, dharau dini yako.

Hata hivyo neno hilo laendelea kutumiwa kinyume kabisa cha maudhui (wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema) yake.

“… apandwa na mzuka… ” ndivyo ilivyoandikwa na gazeti hilo hilo. ‘Mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo. Kiumbe asiyeonekana na anayedaiwa kuwa humwingia mtu kichwani na kusema anayotaka kupitia mtu huyo ambaye kwa wakati ule ni kiti cha pepo.

… alipungwa na nani? Mbona kichwa hicho ni tofauti na yaliyoandikwa? Tena ikaandikwa: “… anautamani usukani wa Ligi Kuu … baada ya chama lake, …kupanda hadi nafasi ya pili …”

Husemwa: ‘chama changu au chake; vyama vyetu,vyao.’ Si sahihi kusema au kuandika chama ‘langu’, chama ‘letu’, chama ‘lake’, chama ‘lao.’

Huo ni uchafuzi mkubwa wa lugha inayotegemewa kuwa mwalimu wa lugha ya Kiswahili duniani.

Katika mtizamo huohuo kuna lililoandikwa “… anakiwasha tu Sauzi.” Hapo kuna la kushangaza, jina moja limeandikwa mara mbili katika matamshi tofauti Huu ni upotoshaji wa majina ya watu na kadhia (jambo linalojiri ; tukio la kuhuzunisha) hii imekuwa ikitokea mara kwa mara.

“Anakiwasha tu …” maana yake nini? Kama mwandishi anafahamu maana yake asidhani wasomaji wote wanaelewa. Waandishi wanapaswa kuandika yanayoeleweka ili wasomaji wayaelewe vyema.

Ndiyo maana kila niandikapo hueleza maana sahihi ya baadhi ya maneno ninayodhani hayaeleweki na baadhi ya wasomaji. Maana ya ‘Kosoa’ (kosoana, kosolewa, kosoleka) ni kitendo cha kumrekebisha mtu.

Maneno ‘lakini’ na ‘pia’ hayatumiwi pamoja ingawa viongozi wetu, wabunge na mawaziri huyachanganya mara kwa mara wanapoongea na wananchi kueleza mambo yaliyofanyika, yanayofanyika na yatakayofanyika.

Kwa mfano: “Serikali imejenga reli ya kisasa ‘lakini pia’ inajenga madaraja ya juu ili kupunguza msongamamo wa magari.”

Maana ya ‘lakini’ ni tamko la kuonyesha kasoro ya jambo. Neno linaloonyesha uwepo wa upungufu, kasoro au hitilafu; isipokuwa, ila. Mfano: “A alitaka kusomea urubani lakini baba yake (Mungu amrehemu Inshallah) alimkataza.”

‘Pia’ ni neno lenye maana tano lakini kwa ukosefu wa nafasi nitaeleza maana moja tu. Kwa muktadha (mazingira ya msamiati katika sentensi yenye kuonyesha uhusiano) huu ni ‘vilevile’, ‘pia.’

Kwa mfano, “pia,vilevile A ni miongoni mwa waliohudhuria.”

Msemo: Muambaa na upwa hali ugali mkavu.

[email protected]
0784 334 096