Mke huyu hanipendi bali simu niliyomnunulia!

03Sep 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Mke huyu hanipendi bali simu niliyomnunulia!

MPENZI msomaji, leo niwageukie vijana wetu tena kuona yale yanayowasibu katika mahusiano. Wapo wanaodhani kuwa kuoa au kuolewa ni jambo jepesi, hivyo kuwa na shauku kubwa kujitosa katika uwanja huo.

Wapo vijana wenye dhamira ya kweli kuoa na wapo mabinti walio na dhamira ya dhati kuolewa. Lakini pamoja na ukweli huo, upo mtego hapo katikati ambao wengi wao hawaufahamu.

Mtego huu ni pale vijana wanapoamua kujenga mahusiano pasipo kujipa muda wa kutosha kila mmoja kumjua mwenzake, kitabia, kujua chimbuko lake kule alikotoka kwa wazazi wake(msingi wa malezi aliyokulia).

Pasipo kudadisi hayo na mengineyo yakiwamo afya zao, ndipo pale wawili hao waliounganisha ukoo, wanajikuta wakianza kuvutana kutokana na kila mmoja au mmojawapo kuonyesha hadharani tabia zake zilizokuwa zimejificha. Eneo hili ndilo ninalotaka kulijadili kwenye makala hii leo.

Wapo vijana wengi ambao wanaingia kwenye ndoa kwa mashindano. Eti kwanini kijana fulani ambaye ni rika langu ameoa na mimi bado. Lazima na mimi nioe mwanamke yoyote atakayeonyesha nia ya kunipenda.

Kijana wa aina hii anakuwa bado hajajiandaa bali anafuata mkumbo au niseme anaiga. Mwingine tayari amejiandaa, anamtafuta msichana wake wanakubaliana wanaoana. Lakini binti mwenyewe unakuta hayuko tayari kuolewa na huyo, bali kuna kitu anakitaka kwake na siyo pendo.

 Hawa ndio vigeugeu wanaowasumbua vijana wengi kwani bado mawazo ya kupenda yamegawanyika. Yawezekana pia kwamba anaye mpenzi mwingine lakini bado ikawa ni siri yake, hivyo akakubali kuolewa na mwingine kwa malengo yake.

Hivi majuzi nikiwa dukani nanunua mahitaji, jirani na duka lile ilikuwepo huduma ya mamantilie. Walikuwepo vijana kadhaa wakijipatia kifungua kinywa majira ya asubuhi.

Yupo kijana mmoja alikuwa akisimulia wenzake jinsi alivyopasua chini simu ya mkewe kwa ghadhabu kubwa. Unajua alisimuliaje?
Alisema hivi; “Washikaji nimeamua kumrudisha mke wangu kwao kutokana na vituko vyake ambavyo vimenifika shingoni. Nimeishi naye siku 28 tu nikawa tayari nimekinahi kwa tabia zake mbaya ambazo nimevumilia sana.

“Kilichoniudhi zaidi ni kule kunitamkia wazi kwamba hanipendi bali ile simu niliyomnunulia. Kusikia vile nilimnyang’anya ile simu na kuibamiza chini kwa hasira, jambo lililomshangaza.

Si alinitamkia hanipendi bali ile simu niliyomnulia? Isitoshe simu hiyo tangu nimempatia, yeye kutwa ni kuchati na wanaume.

Hata usiku anachati, tabia ambayo ilibidi nimwambie mama yangu mzazi aniamulie kama ni sahihi. Mama naye akatuweka kikao na kumwambia kwamba tabia hiyo siyo nzuri. Hata hivyo, bibie hakukoma.

Siku moja nikamwambia twende beach tukazungumzie huko. Ilikuwa ni usiku tuko wenyewe kule ufukweni mwa bahari. Simu ikaita akawa anasita kuipokea, nikamwambia aipokee tu asiwe na wasiwasi. Wakaongea japo kwa kujing’atang’ata.

Nikashindwa kuvumilia nikamnyang’anya ile simu nikaongea na yule aliyepiga. Nikakutana na sauti ya mwanaume. Nikamuuliza wewe ni nani na kwanini unampigia mke wangu simu usiku?

Jamaa akajibu; “huyo bibie ni rafiki yangu na bahati mbaya hakuwahi kuniambia kuwa ameolewa nilidhani yuko free”. Jamaa akaomba msamaha.

Tangu siku hiyo sikuwa na imani tena na mwanamke huyu. Meseji kwenye simu yake ndio usipime. Ndipo nilipombana naye akanitamkia kwamba “wala sikuwahi kukupenda ila naipenda hii simu yako ya tachi uliyoninunulia”. Kusikia vile ndipo nikaikwapua mkononi mwake na kuibamiza chini ikawa vipande vipande, akabaki anashangaa”.

Mpenzi msomaji, alipofikia hapo nikawa nimepata picha kamili ya kisa hicho ndipo nikajiondokea zangu. Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.

Naam, kama nilivyotangulia kusema, vijana wengine au ni wa kike au wa kiume huingia kwenye ndoa kama fasheni au majaribio fulani.

Wanakuwa bado hawajawa tayari kutengeneza familia bali matamanio nje ya ndoa yanawazuzua.

Hapo inavyoonekana kijana alikuwa tayari kuanza maisha ya ndoa lakini mwenzake bado ana vitu anavitamani. Bado alikuwa na marafiki wa nje akiwasiliana nao, huku akisahau ameshaolewa na pendo lake lote anapaswa kuliweka kwa mumewe.

Hilo lilimshinda kwa sababu pendo kubwa liko nje. Pia ana tamaa ya vitu kama alivyotamka mwenyewe kwamba anaipenda simu na siyo yule aliyeinunua.

Vijana yafaa kuwa makini linapofika suala la kuingia kwenye mahusiano yaliyolenga ndoa. Kuunganisha koo siyo suala la lelemama, inahitajika utashi na dhamira ya dhati kupata chaguo sahihi.

Na zaidi ya yote, wakati unafanya maamuzi ya kuchagua, mshirikishe Mungu  aweze kukupa chaguo sahihi kwa maana maandiko yanasema; Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye;Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA”.
 
 
Je, una maoni yoyote juu ya kisa hicho? Au unalo suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]