Mkude, Ajibu wasiwe fimbo ya kumchapia Amunike Stars

10Jun 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mkude, Ajibu wasiwe fimbo ya kumchapia Amunike Stars

NIMEKUWA nikisikiliza habari za michezo kwenye redio, kusoma mitandao ya kijamii na hata kusikiliza mijadala kwenye vijiwe na kwenye meza mbalimbali za kuuzia magazeti juu ya kuachwa kwa wachezaji vipenzi vya mashabiki wa soka nchini,-

Ibrahim Ajibu wa Yanga na Jonas Mkude wa Simba katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.

Wachezaji hao wameachwa kwenye mchujo wa mwisho wa wachezaji waliokwenda nchini Misri kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.

Kwa vyovyote itakavyokuwa kama wachezaji hao wameachwa kwa sababu hawakufanya vema mazoezini, wavivu wa mazoezi, au watovu wa nidhamu, lakini ni kocha mwenyewe Emmanuel Amunike ndiye anayefahamu.

Baba ndiye anayejua tabia za watoto wake. Kuna mwingine hamtumi kabisa dukani kwa sababu ana tabia ya kupoteza pesa au kuchelewa kurudi. Mwingine anateuliwa kula na wageni, mwingine haruhusiwi kabisa hata kukaa nao, akiwasalimu tu inatosha. Kama kawaida ya Wabongo, tayari watu wameshaanza kulalamika ni kwa nini wachezaji hao wameachwa.

Baadhi wanaaminishwa na wenzao kuwa wangekuwapo wachezaji hao basi Taifa Stars ndiyo itafanya vizuri kutokana na uwezo wao waliouonyesha kwenye Ligi Kuu wakiwa na klabu zao.

Kukosekana kwa wachezaji hao, basi imejengeka imani kuwa Taifa Stars haitofanya vizuri, licha ya kwamba wachezaji hao wamekuwa wakichaguliwa kwenye kik0osi hicho na kuondoka, lakini hakuna kipya sana au cha ajabu sana kilichofanywa nao.

Hivi sasa baadhi ya mashabiki wamekuwa wakilalamika chinichini, lakini wengi wanasubiri Stars iondolewe kwenye michuano hiyo ili wampe makavu Amunike.

Ina maana kwa sasa Amunike angalau aombee kikosi hicho kifuzu kwenye makundi kwa kutinga 16-bora, lakini kama kikishindwa kuongoza kundi lake au kwenye nafasi ya pili, basi kazi anayo.

Ukiliangalia Kundi C ambalo Taifa Stars ipo, zipo timu za Kenya, Senegal na Algeria, kiuhalisia pamoja na kwamba mpira unadunda na chochote kinaweza kutokea, lakini wachambuzi wa masuala ya soka hawaipi nafasi Stars kufuzu kwenye kundi hilo.

Kiuhalisia hata kama Tanzania haikufuzu kwenye kundi hilo, haiwezekani kabisa lawama atupiwe Amunike kwa sababu zozote zile, ikiwamo hata kuwaacha Mkude na Ajibu, bali ni kwamba ilikuwa kwenye kundi gumu.

Sasa kuna baadhi ya mashabiki wanaonekana kutaka kutumia kigezo hicho kumlaumu na kumshambulia Amunike kwa kuwaacha Ajibu na Mkude endapo timu itafanya vibaya.

Mimi nina uhakika kuwa Stars inaweza kufanya vizuri au vibaya kwa jinsi tu itakavyojipanga na si kwa sababu ya uwapo au kutokuwapo kwa Ajibu na Mkude.

Ifike wakati mashabiki wa soka wasiwe na ushabiki na baadhi ya wachezaji, bali wawe mashabiki wa timu ya taifa, na pia hata kama timu ikitokea imetolewa basiĀ  itafutwe sababu ya kitaalamu na si kwa sababu eti Ajibu na Mkude hawakuwapo.