Mkuu wa Mkoa Lindi ameanza, wengine je?

18Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mkuu wa Mkoa Lindi ameanza, wengine je?

TANZANIA imepiga hatua kwenye sekta ya elimu kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwamo kuanzisha na kuongeza shule za msingi na sekondari na serikali kugharamia elimu msingi hadi kidato cha nne.

Moja ya malengo ya kuwekwa kwa mikakati hiyo ni kutaka kila mtoto awe wa kike au wa kiume, kutoka katika familia maskini ama tajiri apate elimu.

Hayo yanafanywa, kutokana na ukweli kwamba katika dunia ya leo, ili mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu, kwani ndiyo inayompa kujitambua na kuendesha maisha yake.

Vilevile elimu inampa mamlaka ya kuzikabili changamoto zinazomsonga katika maisha yake ya kila siku na pia kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka, ili kuboresha maisha yake.

Hata hivyo, kumekuwapo na tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi wa kike, ambalo ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo yao kielimu.

Mimba na ndoa hizo vinasababisha upatikanaji wa elimu kwa wote kukabiliwa na tatizo na huenda linazidi kuwa kubwa kwa vile jamii imejiweka pembeni katika vita ya kumaliza changamoto hiyo.

Lindi ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na tatizo la mimba za utotoni ambalo, sasa mkuu wake wa mkoa, Godfrey Zambi, anawataka viongozi kuchukua hatua kuhusu tatizo la mimba za utotoni.

Katika kikao cha kujadili tatizo la mimba za utotoni kilichofanyika hivi karibuni, Zambi anasema, hadi kufikia Novemba mwaka huu, mkoa ulikuwa na mimba 151, huku 43 zikiwa za shule ya msingi na 108 za sekondari.

Wajumbe wa kikao hicho wanawataka wazazi kusimamia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani, shuleni na katika jamii badala ya kuwaachia walimu na wanajamii ndiyo ifanye kazi hiyo na kusababisha watoto kukosa maadili.

Aidha, anaonyesha kukosa imani na mambo yanayofundishwa kwenye jando na unyago, na ameamua kabla ya unyago watoto wanaopelekwa wote waandikishwe kwa watendaji wa vijiji na mitaa.

Anasema kwamba msimamizi wa watoto hao afahamike, ili kumuona kama anafaa kukaa na watoto na kujua ni mambo gani wanakwenda kufundishwa na kufuatilia ufundishwaji wake, ili kama kutakuwa na upotoshaji yazuiwe.

Zambi anawaagiza viongozi katika ngazi zote mkoani humo kuwachukulia hatua wote wanaohusika na tatizo hilo na kuunda kamati za ulinzi wa mtoto kwa kila wilaya na kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu madhara ya mimba za utotoni na mambo mengine yanayoambatana na ngono utotoni.

Anawaagiza pia maofisa elimu na ustawi wa jamii kusimamia uanzishwaji wa klabu rika, katika shule na kwa shule ambazo klabu hizo zipo, basi ziimarishwe, ili kusaidia utoaji wa elimu rika kwa wanafunzi wa shule husika.

Hiyo ni baadhi ya mikakati ya kutokomeza mimba mkoani humo, halafu idadi hiyo ya mimba ni kwa mkoa mmoja tu, tatizo kama hilo hilo litakuwa la nchi nzima kutakuwa na wanafunzi wangapi wenye mimba? Nadhani kuna haja ya kuchukua hatua zaidi, ili kumaliza tatizo hili.

Ikumbukwe kuwa wasichana wanaokatisha masomo na uharibu maisha yao, wamo ndani ya jamii na ni sehemu ya jamii, hivyo ni muhimu jamii ihusike katika kukomesha mimba na ndoa za utotoni.

Kwa hali ilivyo sasa, ipo haja kwa wazazi na walezi kuzungumza na kuwaelekeza, kuwafundisha maadili mema wakiwa wadogo ili yawe ngao yao ingawa inawezekana wakayaacha, lakini ni muhimu mzazi kutimiza wajibu.

Wazazi na walezi hawana budi kuwapa watoto elimu ya makuzi, kwani ni moja ya njia ya kuwaepusha tamaa, ambazo mwisho wa siku zinaweza kusababisha wapate mimba na kukatisha masomo bila kutarajia.

Suala hili la malezi linawagusa pia walimu, kwani wao ndiyo wanaokaa na wanafunzi muda mrefu na wanaona mabadiliko ya mwanafunzi kitaaluma, kitabia, kimwenendo na kimaadili.

Walimu wasiwe sehemu ya tatizo la mimba, kwani baadhi yao huwa wanatuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao hali, ambayo ni kinyume na maadili ya kazi. Ni vyema kujirekebisha ili kuwa na mafanikio katika kampeni hii ya mkuu wa mkoa.