Mlevi aadhimisha siku ya mama kwa kumpa waif ulaji

18Mar 2017
Nkwazi Mhango
Nipashe
Hekaya za Mlevi wa Canada
Mlevi aadhimisha siku ya mama kwa kumpa waif ulaji

BAADA ya wana mama karibu dunia nzima kuendelea kunyonywa na mfumo dume, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni, mwezi huu, mlevi niliteua mke wangu bimkubwa almaaruf bebi kuwa mjumbe wa kigwena (mkutano wa kuamua au kupanga mipango ya maendeleo) cha walevi aka bunge la walevi

Hii ni baada ya kugundua kuwa kumbe walevi wengine huwateua bi wakubwa wa marafiki zao kuwa wanene. Mie sikungoja nistaafu ili atakayechukua kiti changu amteue mamsapu wangu.

Kama mzee K M7 pale Ug, nimeamua kumpa bikubwa maraha wakati nikiwa kwenye ulaji.

Si kama wale walioteuana na kuzusha gumzo, walevi waliridhika na mauteuzi ya mamsapu wangu kwa vile wananiamini.

Na isitoshe bebi huyu wangu ni mlalahoi ambaye hana cha asasi ya raia wala ya hiari almaarufu NGO wala kipato cha ustaafu.

Tofauti nyingine ni kwamba waif wangu amepiga shule hadi akaambiwa no more class ahead... hakuna darasa ulilobakiza.

Hii naitafsiri ili wale walioghushi vyeti au kuogopa umande wasilalamike. Nisiwape taabu maana hapa lazima mtembee na kamusi
Yeye hategemei unene wangu kuteuliwa bali kisomo chake ambacho ni wanawake wachache wanacho kwenye kaya ya walevi.

Mbali na hiyo, kutokana na mfano uliowekwa hivi karibuni kule kwa Joji Kichaka na Trumpet, si vibaya nikaanza kupiga mahesabu ya mke wangu kugombea hata urais wa walevi.

Walevi ni viumbe poa sana kama ukiwaelewa. Wanachotaka ni wewe kuwaonyesha kuwa u mnyenyekevu na asiyejitia kujua kila jambo. Wao hata ukimpa popi wako kuwa kigogo hawajali ilmradi uwape kanywaji na mapupu pale uwanja wa hyena au vipi? Wala hawana visa na visasi kama wale wachunaji ninaowasikia wakihanikiza kupambana na wabaya wao wakimsingizia God utadhani wanamtumikia kweli. Hata hivyo, walevi si kama wadanganyika wala wabongolalaland.

Hakuna kitu wasichokubali kama kuwaburuza au kuwatisha. Kwa mfano, ukimweka lupango mwakilishi wao, hawangoji kipaza sauti umchomoe. Watakutokea wenyewe na utamwachia bila kungoja mapilato wenye adabu, heshima na udhu kumchomoa baada ya wewe kuchemsha kama nilivyoshuhudia hivi karibuni.

Ukitaka maulaji yao yakushinde jifanye muimla. Ukitaka kukosana na walevi wadhulumu au kuwakingia kifua waliowadhulumu au kuvunja sheria zao. Watakutokea na michupa ima wakutie ngeu au utoke mkuku kama mbwa aliyefumwa akiiba nyama kama si paka aliyeiba maziwa.

Kama ukifanikiwa kuwaburuza walevi ujue zako zesha. Kwani, watakulia pini hadi msimu mwingine wa uchakachuaji wakupige chini. Pamoja na ulevi wao, walevi wana sifa nyingine.

Wana kumbukumbu kama tembo. Unaweza kuwaudhi ukajishaua na kujifanya wewe mungu mlevi kwao wakakushiti. Ila siku ya siku ikifika, utaona visasi vyao.

Turejee kwenye uteuzi wa bi nkubwa wangu. Guess what. Mwaka jana niliteua wajumbe wengine wa dezo. Kwa sheria za kilevi, lazima uteue angalau asilimia ya akina mama kwenye kila unaowapa ulaji. Awali nilivipa ulaji vidume vikawa vingi kuliko kina mama.

Acha akina mama waanze kunung’unika.

Si walikwenda kwa bi nkubwa ambaye wananchukulia kama shoga yao na kumpa onyo kuwa asipoteua mwanamama kutimiza matakwa ya sheria za walevi asahau ukuu mhula ujao.

Kuona hivyo, si nikaamua kumteua mamsapau wangu ingawa yeye ni tofauti na hao mashoga zake hasa ikizingatiwa anatoka kwenye ukoo ule ule wa wanene wa walevi kama wale wa kule Idodomya.

Baada ya baadhi ya walevi na wavuta bangi kuanza kulalamika kwanini nimemteua bebi au switi hati wangu sikunyamaza zaidi ya kuwapa kanywaji na kesi kuishia hapo.

Wengine walizidisha unywanywa. Kuwakata ngebe niliwaambia kuwa bebi wangu ni bonge ya supu yaani ni msupu au mzuri kwa wale wasiojua Kiswahili cha walevi. Ni supa au kwini.

Kimsingi, waliokuwa wakinitia taabu ni akina mama. Kwa vile wanaweza kudanganyana na kuwekana sawa, nilishangaa kuona walivyoridhika na mimi kumteua bi mkubwa wangu utadhani atawawakilisha makapuku waliokuwa wakinibana niteue ili kuleta uwiano wa kijinsia kwa mujibu wa katiba ya walevi. Sasa kwa vile nshamteua bi nkubwa.

Next time, nategemea kutoa ulaji kwa kitegemezi chetu kiitwacho Riziki ili kaya yangu yote iwemo kwenye njengo.

Isitoshe kama kitegemezi kitakuwa na mama yake njengoni, wale vishoka wanaosifika kufanya fujo wajaribu waone wataogopa kwa vile familia iko gado.

Hii nayo dili hasa usawa huu ambapo nasumbuliwa na malazi ambayo ni siri kuwaambia walevi hata kama wanayajua. Isitoshe mimi kwa cheo changu kama dingi wa kaya ya walevi si mjumbe wa kigwena chetu. Hivyo, sirahisi kuwapo kule kuhamisha mali zangu zisiliwe na vishoka, mafisi na vispring chickens vya kirume kama alivyofanyiwa nzee Madais alipokuwa lupango. Hayo tuyaache.

Kwanini tusiagane? Bye.