Mnaouza dawa bandia, Nini hiyo kwa jamii ?

15Nov 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mnaouza dawa bandia, Nini hiyo kwa jamii ?

DAWA bandia ni tabu kubwa. Zinamuathiri mtumiaji pale, atakapozitumia na zina madhara makubwa kwa watumiaji.

Pia, zinapotumika hata kwa wanyama kama mifugo na mimea, napo ni changamoto, hasa pale mmea ukuaji wake hauwi mzuri na hata mfugo unapowekewa nao uweza kufariki.

Inasikitisha kuona watu wanaofanya biashara za kuuza dawa wanakuwa, sio waaminifu kwa kuuza visivyofaa kwa walaji na hata mimea.

Inakuwaje mtu apate utajiri mkubwa kupitia kuuza kitu kinachomletea madhara mtumiaji. Ikumbukwe kwamba, binadamu tuna matatizo ya kiafya na tunapokula dawa, malengo ni kupona, ili kuendelea na majukumu mengine.

Lakini, kinachotusikitisha unakula dawa tena ni feki ambazo nazo anachangia mtu kuendelea kulala kitandani.

Serikali imekuwa ikipambana na hata kuwachukulia hatua watu wote wanaokamatwa, wakijihusisha na uuzaji wa dawa bandia.

Tumekuwa tukiona misako katika maduka ya dawa ikiwamo maabara za watu binafsi, lengo ni kupambana na watu wanaojihusisha na uuzaji dawa bandia na kutoa matibabu kwa dawa zizisofaa.

Katika misako hiyo, baadhi ya maduka ya kuuza dawa na maabara za watu binafsi zilibainika kutoa huduma zisizofaa kwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.

Hivi karibuni, mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Arusha na Kilimanjaro imeonekana kuwa kinara wa uingizaji dawa nchi ikiwamo ya Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kaskazini imeripotiwa kuwa kinara wa dawa duni za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havikusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Akitangaza matokeo ya operesheni maalum ya dawa, vifaa tiba, vitenganishi, dawa asili na tiba mbadala mbele ya waandishi wa habari jijini Dar e Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Akida Khea, anasema hilo wilaya zaidi ya 33 katika mikoa 20 wameweza kukamata dawa bandia aina saba zenye thamani ya fedha za kitanzania Sh. 12,495,500.

“Katika dawa hizo, uchunguzi wetu baada ya kuzibaini tuliweza kuwasiliana na wamiliki wa dawa husika ambapo walituthibitishia kuwa ni bandia na zingine zimegushiwa maandishi” anasema.

“Tumebaini mikoa iliyo pembezoni ikiwemo Kigoma kubainika kuwa na dawa nyingi bandia pamoja na Mwanza. Pia, mikoa ya Kaskazini ikiwamo Arusha na Kilimanjaro, nayo imebainika kuwa na wingi wa dawa hizo” anasema.

Katika tukio hilo, TMDA waliwashirikisha mamlaka mbalimbali wakiwamo Jeshi la Polisi, Msajili wa Baraza la dawa asili na tiba mbadala pamoja na Tamisemi.

Mrakibu wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu ya upelelezi kitengo cha Interpol, anasema jeshi hilo linafuatilia kwa karibu, wahusika waliobainika katika kuingiza au kusambaza watachukuliwa hatua.

"Wajibu wa jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Usalama wa raia ni pamoja na afya za wananchi sisi kama Jeshi la Polisi kwa pamoja tunahakikisha usalama wa raia, unalindwa na wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria uchunguzi ukikamilika" anasema.