Morrison ni nani Yanga?

18Jul 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Morrison ni nani Yanga?

“HESHIMA apewe ajuwaye heshima.” Ni vizuri kumheshimu mtu anayewaheshimu wenzake. Hii ni methali ya kutumiwa kutushauri kuwa tunapaswa kuwaheshimu wale wanaoweza kutuheshimu. ‘Adabu’ ni utaratibu unaokubalika katika kufanya jambo; heshima, nidhamu.

Kwa hiyo heshima haiji mpaka iletwe. Maana yake heshima haiwezi kuwapo bila ya kuletwa. Methali hii pia yaweza kutumiwa kumsuta mtu anayetaka apewe heshima ingawa vitendo vyake havielekei au mwenyewe haelekei kujiheshimu.

Vilevile heshima ni kitu cha bure. Maana yake heshima hainunuliwi. Hii nayo ni methali ya kutumiwa kutunasihi tuwe na heshima na adabu.

Timu ya mpira wa miguu huwa na wachezaji 11 uwanjani wanaotakiwa kucheza kwa bidii na ushirikiano ili kupata ushindi dhidi ya timu pinzani. Haijatokea wala haitatokea mchezaji mmoja tu kuingia uwanjani ili ashindane na timu yenye wachezaji 11.

Itakuwa mshangao, kioja na kichekesho kwa watazamaji na waamuzi kuona mchezaji mmoja tu anaingia uwanjani kupambana na timu pinzani yenye wachezaji 11! Mchezo huo hautachezeshwa na timu ya mchezaji husika itawajibika mbele ya sheria za mashindano.

Pele, aliyekuwa mchezaji mahiri wa kabumbu nchini Brazil, alisifika duniani kote kwa umahiri aliokuwa nao uwanjani mpaka akaitwa ‘mfalme’ wa kabumbu duniani, lakini alihitaji msaada na ushirikiano na wachezaji wenzake. Ndio maana wahenga walisema “Kidole kimoja hakivunji chawa.” Maana yake mtu hawezi kumvunja chawa kwa kidole kimoja, lazima akihusishe na kingine.

Bernard Morrison ni mchezaji wa Yanga mwenye asili ya Ghana. Hajui maana ya ushirikiano, heshima na adabu? Au anadhani yeye ndiye mchezaji bora zaidi ya wengine woote aliowakuta Yanga? Hajui kuwa Yanga ilianzishwa mwaka 1935 wakati yeye hakujulikana kama angezaliwa?

Yanga ilikuwa na wachezaji mahiri na shupavu kuliko yeye lakini hakuna aliyejiona bora kuliko wenzake. Kama Morrison aliwadharau wachezaji wenzake wa timu zote alizochezea kwao na nchi zingine, si hapa Tanzania. Kutokuwa na adabu kwa viongozi ni huko huko lakini si Tanzania, abadan.

Asidhani kuwa yeye ni bora zaidi ya wachezaji wenzake, walimu na viongozi wa klabu iliyomsajili. Mchezaji anapotolewa ili aingie mwingine, maana yake ameumia au kashindwa kuendana na kasi ya mchezo. Anapotoka uwanjani hukaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba ila anapofanya kosa kubwa na kuoneshwa kadi nyekundu hutakiwa kwenda kwenye chumba cha wachezaji.

Morrison anatolewa uwanjani baada ya kushindwa kuendana na kasi ya mchezo, lakini anakataa kukaa kwenye benchi la wachezaji wenziye wa akiba na kwenda kwenye chumba cha wachezaji, kubadili nguo na kuondoka kabisa uwanjani huku mchezo ukiendelea!

Kuna wakati aliondoka kambini kwa kiburi na alipofuatwa alitishia kwa kisu kisha akaelekea alikokusudia. Kwa kitendo hicho alimdharau kocha, wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi wa klabu na watazamaji waliotoa fedha zao kuuangalia mchezo huo.

Nadhani viongozi wa Yanga wanaogopa kumrudi (kitendo cha kumwadhibu mtu kwa kosa alilofanya) Morrison. Kama sivyo, mbona wamekuwa kimya kwa utovu wa nidhamu anaofanya mara kwa mara? Hawajui ukimya wao unazidi kumfanya ajione yeye ni bora zaidi ya wachezaji wenzake na viongozi ambao ndio waliomsajili?

Yanga imecheza mechi nyingi na kushinda bila uwepo wake na imeshindwa akiwa mchezoni. Kwa nini anadekezwa kiasi hicho? Ameikuta Yanga na ataondoka aiache ikiitwa Yanga, sio Morrison! Utovu wa nidhamu anaofanya Yanga uwe fundisho kwa timu zinazotaka kumsajili.

Nionavyo, viongozi wa Yanga wamekuwa kimya sana kiasi cha kudharauliwa si na wanachama tu bali hata mashabiki! Tangu uongozi wa sasa uingie madarakani umekuwa kimya sana. Matokeo yake wadhamini wa Yanga, GSM sasa ndio kila kitu. Wanasajili na ndio wasemaji na watendaji!

Uongozi ni dhamana ya kusimamia jambo kwenye taasisi au penginepo; madaraka anayopewa mtu kusimamia au kuongoza shughuli. Viongozi wa Yanga hawasikiki. Wanamwogopa Morrison?

Wanashindwa kuiongoza Yanga? Kama ndivyo, kwa nini waligombea nafasi walizo nazo? Nawashauri wajiuzulu kwa heshima na taadhima badala ya kusubiri kutimuliwa kwa fedheha!

Siku Yanga (au GSM?) ilipotiliana saini mkataba na timu ya Hispania, GSM ndio iliyoonekana kuwa wenye Yanga! Matangazo yote yaliyotolewa jukwaani yalifanywa na mwakilishi wa kampuni ya GSM huku viongozi wa Yanga wakiwa wasikilizaji kama waalikwa wengine. Walikuwa wakikodoa (kitendo cha kufumbua macho na kutazama kitu kwa muda mrefu) muda wote wa matangazo!

Kulikoni? Au maji yamezidi unga kwa viongozi wa Yanga? Natahadharisha tu kwani ilisemwa “Bora kupigwa dhoruba ya dhahiri kuliko ya siri.”

[email protected]
0784 334 096