Motisha ndio chachu ya ufaulu kuongezeka

19Mar 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Motisha ndio chachu ya ufaulu kuongezeka

MOTISHA ina maana nyingi katika hamasa ya mwanadamu, katika mtazamo wa kusukuma kasi yake kutamani na kupenda kitu fulani.

Kuna ushahidi mwingi kwamba katika eneo na mazingira ya aina yoyote yale, mtu anapopata msukumo wa motisha, basi anasimamia katika kasi na mwamko mkubwa wa kuwajibika kikazi au shughuli aliyo nayo na daima mabadiliko hushuhudiwa.

Motisha inaweza kupatikana katika sura nyingi; ama kwa maneno, pesa na zawaida ya aina nyingine popote, ambayo inaugusa utashi binafsi wa mtu.

Hilo ndilo mtu akirudia katika mustakabali wa maana hiyo ya motisha katika masomo shuleni ambako wamejaa wanafunzi wa umri mdogo, basi kila inapotolewa motisha hizo, inawasaidia sana walimu na wanafunzi kubadilika kielimu.

Ukizungumzia motisha kwa wanafunzi, hii inawasaidia wanafunzi kujituma kusoma na kufanikisha hata ufaulu kuongezeka kila mwaka.
Motisha inapotolewa kwa wanafunzi, unawapa matarajio ambayo ndani ya utashi wake wa uanafunzi, mhusika huyo anaguswa nayo.

Mara nyingi tu tumekuwa tukiona baadhi ya shule zinafanya vizuri katika mitihani yao na katika orodha zinazotajwa kufikia mafanikio hayo, motisha kwa walimu na wanafunzi ina nafasi yake.

Motisha zinapotolewa na wamiliki wa shule au viongozi wa maeneo jirani, wazazi na walezi wanaohusika moja kwa moja au wako jirani na mustakbali huo, wote kwa pamoja wanaguswa iwe kwa kuiga kushiriki moja kwa moja.

Inasikitisha sana tunapoona baadhi ya wazazi, wanashindwa hata kuwapa watoto wao motisha na pesa wanapokuwa nazo, pindi wanapofanikisha taaluma.

Katika baadhi ya maeneo, pesa zilizopo hasa katika jamii zinazokumbatia aina fulani za tamaduni, si cha kushangaza kuona kiasi chote cha pesa kinaingizwa katika shughuli za utamaduni wa ngoma.

Hapo hapo, pia inasikitisha kumuona mzazi anashindwa kumpa mtoto wake zawadi, pindi anapofanya vizuri masomoni, lakini pesa anazokuwa nazo anazipeleka ngomani kwa mambo yasiyo na tija kwa mwenendo wa maisha yake.

Katika hilo, kuna busara zote zinazopaswa kuelekezwa kwa walimu kupewa haki hiyo kutokana na kutoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu.

Tukipanua maana ni kwamba hata viongozi wa serikali ya mtaa, wakiwamo madiwani na wengineo wanapaswa kujenga utamaduni wa kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wa kata zao.

Kutolewa motisha hizo kuna maana kubwa katika saikolojia ya mwalimu, kuelekea kupatikana matokeo mazuri shuleni.
Matokeo mazuri, siku zote ni zao la motisha na juhudi za moja kwa moja kwa anayefundisha na anayefundishwa.

Pia, nikienda mbali zaidi, juhudi hizo za moja kwa moja zinapatikana katika sura ya uwajabikaji wa pande hizo mbili; mwalimu na mwanafunzi.

Wanafunzi wanapofanya mitihani, wakafaulu na wakapewa motisha stahiki, daima itasaidia kuboresha sekta ya elimu katika eneo tajwa.

Tumekuwa tukiona shule zinafanya vibaya, uongozi unakutana na kujadili nini kifanyike. Baada ya kugundua kufanyika, ndio hapo motisha zinaanza kutolewa kwa wanafunzi husika.

Motisha tumekuwa tukiziona katika sura ya madaftari, pesa taslimu na wengine kupewa punguzo la ada na hata kusoma bure.

Sasa tukiifanya katika mtazamo wa kanuni, ni jukumu la wazazi kuhakikisha wanawapa watoto motisha na sio kutegemea wafadhili au viongozi wengine.