Mpanga ratiba Ligi Bara atoke Ulaya?

19Jan 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mpanga ratiba Ligi Bara atoke Ulaya?

KATIKA hali ya kushangaza na kushtusha, Ligi Kuu Tanzania Bara imeingia katika mzunguko wa pili wakati baadhi ya timu bado hazijamaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza.

Inawezekana kabisa hii ikawa ni ligi ya kwanza duniani kufanya hivyo.

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ambao ndio wasimamizi wa ligi hiyo, msimu huu wameonekana kuwa na matatizo mengi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Hakuna mtu anayekataa kuwa kuna baadhi ya vitu havikwepeki kama vile Simba kucheza mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika karibuni kila wiki, hivyo viporo kwake haviepukiki.

Hapa Bodi ya Ligi inaweza ikakaa na kujitetea na kueleweka mbele ya wadau wa soka.

Lakini inakuwaje timu zinaanza mechi ya mzunguko wa pili kabla hazijamaliza mechi za mzunguko wa kwanza?

Nadhani timu zingesubiri kwanza Simba irejee halafu kila timu iliyokuwa ina kiporo chake dhidi ya Simba zicheze ndipo mzunguko wa pili uanze.

Cha ajabu zaidi ni kwamba hata Yanga na Azam zimenza kucheza michezo ya mzunguko wa pili wakati haijamaliza mechi baina yao wenyewe ya mzunguko wa kwanza, wakati klabu hizo mbili hazichezi mechi za kimataifa.

Baada ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kumalizika huko Zanzibar, ilitegemewa timu hizo zipambanane na kumaliza mzunguko kwa kwanza, lakini sivyo.

Wakati ikitajwa tatizo la timu kucheza raundi ya pili kabla ya kumaliza ya kwanza ni ratiba ya Simba kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa, je mechi ya Yanga na Azam nayo tatizo ni nini?

Kwa nini imekwepeshwa wakati timu zote zipo na hakuna timu yoyote inayoshiriki michuano yoyote ile? Huu ni udhaifu mkubwa wa upangaji wa ratiba na kuisimamia.

Vyovyote vile watakavyojitetea Bodi ya Ligi, lakini ni kama msimu huu wameivuruga ligi kutokana na kuwa na ratiba ya kienyeji, isiyozingatia haki na usimamizi.

Mfano mwanzo tu wa ligi, tuliona Yanga ikipangiwa zaidi ya mechi sita mfululizo nyumbani, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwenye historia ya soka Tanzania.

Nasema sita kwa sababu nazitoa zile ambazo ilihesabika kuwa inacheza ugenini, ingawa ilikuwa inacheza Uwanja wa Taifa na kama ukiunganisha na hizo, unapata mechi 11.

Hivi wapanga ratiba walikuwa wanashindwa kukwepesha mechi za ugenini na nyumbani?

Kwa nini timu ikicheza Dar es Salaam, ipangiwe tena na timu ambayo inatumia uwanja hapa hapa jijini?

Kingine ambacho kinaonekana wapanga ratiba wamefeli ni tangu mwanzo wa msimu, kuna baadhi ya timu kubadilishiwa uwanja.

Awali inaonekana mechi inatakiwa kuchezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, lakini ghafla tunaambiwa inachezwa Dar es Salaam kwa sababu ambazo hazitolewi ufafanuzi wa kutosha, huku ni kufanya baadhi ya mashabiki waingiwe na wasiwasi.

Moja kati ya vitu ambavyo vinasababisha hata wadhamini wasite kuingia kujitokeza kudhamini Ligi Kuu Bara ni baadhi ya vitu kama hivi, ambavyo unaweza kuita ni ubabaishaji au "mipango michafu" inaandaliwa.

Wadhamini wanataka kuona ligi imara, ushindani, yenye uwazi, haki kwa kila timu, lakini pia ikifanana kwa usimamizi kama ligi nyingine duniani.

Ligi Kuu msimu huu si tu kwamba haina udhamini, lakini imekuwa ya kuchekesha kutokana na vitu nilivyovianisha hapa, kiasi kwamba imeshaanza kupoteza mvuto kwa wapenzi wa soka na kuonekana ni ligi ya kukamilisha ratiba.

Kwa wale wapenzi wa timu bado wanazifuatilia timu zao, lakini kwa wapenzi wa soka mvuto umeshaanza kupungua na hata kwenye "vibanda umiza" kwa kuangalia mpira mashabiki wengi wamepungua tofauti na ilivyokuwa awali.

Mashabiki wengi kwa sasa wanaonekana kujazana katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Cha kujiuliza haya yote yanayofanywa ni kwa makusudi, bahati mbaya, au utaalamu mdogo?

Kama ni utaalamu mdogo wa upangaji wa ratiba, je hakuna umuhimu wa kutafuta wataalamu nje ya nchi waje kutufundisha jinsi ya kupanga ratiba vizuri na kuisimamia bila kupindisha-pindisha mechi?