Mradi Bonde la Msimbazi ufuate utaalam kuondoa ubabaishaji

14Nov 2021
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Mradi Bonde la Msimbazi ufuate utaalam kuondoa ubabaishaji

NOVEMBA 10, mwaka huu, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi zilitangaza kuwa ziko katika hatua ya maandalizi ya mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kwa kutumia fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Mradi huo utatekelezwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Manispaa za Kinondoni, Ubungo na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na Wakala wa Barabara (TANROADS).

Kwa mujibu wa tangazo hilo, mradi huo unatarajiwa kusaidia kukabiliana na mafuriko kwa kuwa itajengwa miundombinu itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kupeleka maji baharini bila kutuama au kufurika katika maeneo ya bondeni.

Aidha, miundombinu hiyo itajumuisha kuimarisha kingo za mto katika maeneo korofi ili kudhibiti mmomonyoko wa udongo kwa maeneo ya kati na mwanzo wa Mto Msimbazi, kujenga makinga mchanga katika maeneo ya kimkakati, kujenga vituo na karakana za kutunza mto.

Kupitia mpango huo, kutakuwa na kazi ya kuhamisha waathirika wa mafuriko katika maeneo ya mabondeni, kuchimba na kupanua mto kuanzia barabara ya Kawawa hadi Daraja la Salender.

Pia yatajengwa matuta yenye vimo tofauti kwa ajili ya kuruhusu maji kupita kwa usalama katika kipindi cha mafuriko, kuruhusu matumizi mbalimbali ya ardhi ikiwamo City Park na uendeshaji wa maeneo ya makazi na biashara.

Lengo la tangazo hilo ni kuujulisha umma na wadau wa bonde kuwa timu za wataalam kutoka taasisi husika pamoja na wataalam washauri zinazofanua upembuzi yakinifu na usanifu zitapita katika baadhi ya maeneo ili kufanya mashauriano na wadau kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano, mahojiano na dodoso.

Hatua hiyo ni ya kupongezwa sana kwa kuwa sasa suluhisho la kudumu la bonde hilo litapatikana na sasa zile kelele za kila kipindi cha mvua hazitasikika tena.

Pia maisha ya watu wa bonde hilo yataimarika kwa kuwa hawatakuwa na hofu hata ikinyesha mvua kubwa kiasi gani au ikinyesha kwingine na kuleta udogo na uchafu mwingine ambao lengo ni kuelekea baharini.

Nawaza kwa sauti kuwa mradi huu ni mzuri lakini ni lazima utekelezwe kwa kiwango kikubwa sana ili nchi ione umuhimu wa wataalam.

Mradi huu unatukumbusha barabara ya mwendokasi ambayo katika eneo hilo ambako ni bondeni hapakuinuliwa ili barabara ipige juu ya daraja, badala yake ilipita kawaida kama eneo ambalo halina tatizo lolote.

Pia imejengwa karakana na kituo kikubwa cha mabasi ya mwendokasi ambacho kukiwa na dalili ya mvua tu wafanyakazi na watumiaji wengine wanaanza kukimbia kwa kuwa hata kama mvua imenyesha Kisarawe, basi tope na uchafu mwingine unasafirishwa kupitia Mto Msimbazi kuelekea baharini.

Kilichosikika kwenye mradi huo ni kuwa wataalam hawakusikilizwa na walilazimika kubadilisha mchoro wa awali, hali iliyowafanya hata wananchi wa kawaida kabisa ambao hawajasomea ujenzi na uhandisi kujiuliza kwamba wataalam hao hawakuona hapo ni bondeni na wahakikishe barabara inapita juu?

Kila mvua kubwa inaponyesha Dar au Kisarawe, uwe na uhakika mawasiliano kati ya upande mmoja na mwingine yanakatika kwa kuwa barabara haipitiki huku magari na miundombinu ikiharibika sana.

Sasa unakuja mradi mpya wenye lengo la kuboresha ambao unatumia fedha za Watanzania, ninaposema fedha za Watanzania ni kwa kuwa huu ni mkopo nchini inaingia ambao wanaoishi na ambao hawajazaliwa watawajibika kuulipa, ndiyo maana lazima tufuatilie matumizi na bidhaa itakayopatikana.

Haitarajiwi makosa yaliyofanyika kwenye mwendokasi yafanyike kwenye mradi huu, bali tuone thamani ya fedha na nchi kuwa na wataalam waliosoma katika ngazi mbalimbali kuanzia shahada ya kwanza hadi shahada ya uzamivu.

Ni muhimu wakajifunza kutoka nchi zilizoendelea namna zimejenga miundombinu yake kwenye maeneo kama hayo kiasi cha kuwa kivutio kikubwa cha watalii.

Kwenye nchi zilizoendelea, kuna vivutio vingi ambavyo huwafanya watu kusafiri kwenda kwenye halmashauri, manispaa na majiji kujipati fedha lakini kwetu mito imekuwa maumivu kwa kuwa mtu akiona wingu limefunga angani naye anajiandaa kufungasha kupisha maji.

Lazima mipango miji ifanye kazi kwa ustadi mkubwa pasipo kuingiliwa na wanasiasa kwa kuwa bado inakumbukwa jinsi bomoabomoa ilivyokuwa ngumu kwa kuwa wako waliokuwa wanatetea, lakini swali linakuwa inakuwaje wanaachwa wanajenga kiasi hicho?

Tuone thamani ya fedha na miundombinu bora.