Mrejesho wa makala iliyopita

10Dec 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mrejesho wa makala iliyopita

MAKALA yangu ya Jumapili iliyopita imepata mrejesho kutoka kwa msomaji Msalah wa Kondoa ambaye anaeleza mambo mengi kama ifuatavyo:

“Mzee Yanga, habari za jioni. Vipi hali yako? Nimeona ujumbe wako kwa viongozi wa Simba. Nadhani ujumbe ulioutoa wa “Simba, aisifuye mvua imemnyia” (Lete Raha 4-9 Desemba, 2016) ni mwepesi sana kwao.

“Usemi unaowafaa ungekuwa: ‘Simba, anayemjua mwanga, amewanga naye.’ Mwanga huwanga usiku sana (usiku wa manane) watu wakiwa wamelala. Hivyo kumjua ni lazima uwe macho wakati huo.

“Rushwa hutolewa kwa usiri sana. Kwa hiyo nao watakuwa wanajua jinsi hiyo rushwa inavyotolewa.

“Kipa wa Simba, Juma Kaseja alimshika Ngassa wa Yanga katika eneo la ‘penalty box.’ Kosa hili kwa kipa ni kutolewa n-nje ya uwanja kwa kuoneshwa kadi nyekundu lakini haikuwa hivyo. Ikapigwa penalty, Kaseja akiwa golini. Kwa Simba, refa mzuri!

“Yanga walifungwa bao la pili na Mbeya City wakati refa akiwapanga wachezaji wa Yanga. Ni kosa ila kwa Simba, refa ni mzuri na bao walilofungwa Yanga ni halali kwa sababu tu Yanga kanyongwa. Eti m-baya wako mwombee njaa!

“Mkude au Banda kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu, kwa Simba, refa m-baya! Niyonzima kutolewa kwa kadi nyekundu, refa mzuri!”

Wahenga walisema ‘adui wa mtu ni mtu.’ Maana yake binadamu huhasiriwa na binadamu mwenzake! Aghalabu matatizo tuyapatayo husababishwa na watu tunaoishi nao siku zote.

Msalah anaendelea: “Zaidi ya hapo Mzee Yanga, mwaka 1991 katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza, Simba waligoma kurudi uwanjani kipindi cha pili, wakidai refa Hafidh Alli (marehemu) alikuwa akiipendelea Yanga!

“Cha kushangaza, Januari 1992 wakakubali kuchezeshwa na Hafidh Alli katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar. Kenneth Mkapa alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya tisa tu kipindi cha kwanza.

Refa Hafidh Alli ‘akawa mzuri sana’ na kushangiliwa na mashabiki wa Simba!”

Jioni ya siku hiyo, Msalah akanitumia ujumbe mwingine: “Hebu ukumbushe umma kuwa Simba waache kulilia bao alilofunga Hamis Tambwe wa Yanga.

“Simba walitufunga bao la ‘video.’ Mgosi alipiga mpira ukagonga mtambaa panya ukatua chini na kurudi uwanjani. Refa hakuona mpira ukivuka mstari akaendeleza mchezo.

“Wachezaji wa Simba wakamzonga refa na kumwonesha marudio kwenye skrini (screen) jinsi mpira ulivyovuka mstari, refa akalikubali bao. Kwa Simba, refa mzuri na bao lao ni la halali!”

Twaambiwa na wahenga kuwa “Mtu haoni aibu yake ila huiona ya mwenziwe.” Kwa kawaida binadamu hatuzioni kasoro zetu ila huziona za wenzetu.

Methali hii hutumiliwa mtu mwenye tabia ya kuwalaumu na kuwakashifu wenzake kutokana na aibu zao, lakini yeye hazioni zake mwenyewe.

Kwa kawaida si Simba wala Yanga inayofurahia ushindi au maendeleo ya mwenzake. Upande mmoja ukishindwa huwa chereko kwa upande mwingine.

Mambo haya huanzia uwanjani kwa kuzomeana. Timu inayoshinda, mashabiki wake hubeba mfano wa jeneza lililofunikwa kwa bendera ya timu iliyoshindwa!

[email protected]